Makala

UJUZI NA MAARIFA: Fundi aliye na ujuzi wa kuunda ua wa seng’enge

January 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

CORNELIUS MUTISYA na CHARLES WASONGA

NI saa mbili asubuhi.

Tunafika katika soko la Kaviani lililoko katika eneo bunge la Kathiani, Kaunti ya Machakos tukiwa katika pilkapilka zetu za kikazi mitaani kama ilivyo kawaida yetu. Kwa upeo wa macho yetu, tunawaona jamaa wawili wakiendelea kuezeka ua wa seng’enge kuzunguka shamba la Kitheka Mulinge, mwanawe Jenerali mstaafu, Jackson Mulinge huku watu wakiwazingira wakiajabia kazi yao ashirafu. Tulikata kauli nasi kufika eneo hili ili kushuhudia ujuzi wa mafundi hao.

Katika mahojiano, Pius Mutiso Munyao alituarifu kwamba, aliingilia kazi ya kuezeka nyua za seng’enge yapata miaka 20 hivi iliyopita baada ya kuhudumu katika duka moja la jumla mjini Kathiani lililomilikiwa na Jenerali Jackson Mulinge huku akisubiri kuajiriwa katika Jeshi la Kenya (KDF). Hii ni kwa sababu marehemu Mulinge alikuwa na ushawishi mkubwa katika asasi hiyo ya ulinzi.

“Badala ya Marehemu Mulinge kunipeleka jeshi kama vijana wengine wa eneo la Kathiani, alinishauri nijifunze taaluma ya kuezeka ua wa seng’enge ili niwe nikihudumu katika mashamba yake makubwa katika maeneo ya Kathiani, Athi River na Kangundo,” asema Munyao.

Fundi huyu azidi kuarifu kwamba, Jenerali Mulinge alimuunganisha na wajuzi wengine wa kazi hii na akapata ujuzi zaidi. “Kutangamana kwangu na wajuzi hao kulinifaa si haba. Nilijinoa kikamilifu. Sikujuta kwa kukosa kupelekwa kuhudumu katika KDF,” asema fundi huyu. Munyao asema kwamba, alipohisi amebobea kikamilifu, alianza kujitegemea na hapo mkoko ukaanza kualika maua. Aliibuka kuwa fundi mkuu wa kuezeka nyua za seng’enge katika mashamba yote ya marehemu Mulinge.

Aidha, Mulinge alikuwa pia akimpeleka kwa marafiki zake awaezekee nyua za seng’enge katika mashamba yao na akawa johari la thamani na fahari kuu janibu za Ukambani. Sifa zake zilizagaa kote mithili ya cheche za moto nyikani katika kona zote za Ukambani.

“Niliweza kupata pesa za kukimu familia yangu kupitia kazi hii. Hii ni kwa sababu, licha ya mafundi kuwa wengi, naenziwa mno kutokana tajriba yangu ya miaka mingi,” aeleza Munyao.

Kwa wastani fundi huyu hutoza Sh8,000 kwa kuezeka ua katika shamba la ukubwa wa ekari moja. Hata hivyo, ada hii inaweza kupanda hadi kufikia Sh10,000 ikiwa shamba liko katika eneo lenye milima na mabonde.

“Ada hii huwa ya gharama ya kazi pekee kwa sababu kawaida mwajiri ndiye hununua vitu vyote vinavyohitajika katika kazi kama vile nguzo, seng’enge, na misumari maalum ya kuezeka ua,” asema Munyao.

Baadhi ya changamoto ambayo fundi huyu hupitia ni kwamba baadhi ya wateja wake wenye mapato ya chini humlipa kwa awamu huku wengine wakikawia kwa muda mrefu kabla ya kulipa.

“Kwa hivyo, nyakati zingine mimi hulazimika kutumia pesa zangu kuwalipa watu wangu wa mkono endapo tajiri atakawia kulipa. Mimi hulazimika kuvumilia usumbufu huu ili nisipoteze wateja kwa washindani wengine, anaeleza.

Mteja mwingine wa Munyao ni Beth Kitheka ambaye ni mkazi wa Kathiani. Anasifia ustadi wa Munyao katika kazi hii.

“Huyu ni fundi aliyekomaa na mwenye ujuzi ya kipekee ambao mafundi wengine wenye umri mdogo hawana,” asema Beth, mama wa watoto watatu na mwalimu katika shule moja ya upili Machakos.

Pius Munyao anawashauri vijana wawe waaminifu kwa waajiri wao na watapata ufanisi usiomithilika na kuwa kielelezo chema katika jamii.

“Kama sikuwa mwaminifu kwa Jenerali mstaafu Mulinge ningekuwa wapi sasa,” auliza gwiji huyu.

Munyao ana mpango wa kuwafunza vijana taaluma hii ambayo haina mafundi wengi janibu za Ukambani ili waweze kujichumia mapato na kujiruzuku maishani mwao badala ya kutegemea kazi za ofisi ambazo zimeadimika kama wali wa daku.

“Vijana wafahamu kuwa kazi ni kazi, mradi mja awe na ari na hamasa ya kutekeleza wajibu wake kwa bidii,’’ anashauri.