Mibabe wa Super 8 walivyomenyana
Na JOHN KIMWERE
KAMPENI za kuwania taji la Super Eight Premier League (S8PL) msimu uliopita zilishuhudia ushindani mkali kabla vikosi vilivyopigiwa chapuo kufanya kweli kuteleza na kukosa taji hilo.
Mbio za kipute hicho zilishuhudia vita vya kufa mtu baina ya mabingwa watetezi, Jericho Allstars, Meltah Kabiria FC, Mathare Flames, Githurai Allstars iliyokuwa inashiriki ngarambe hiyo kwa mara ya kwanza bila sahau wasomi wa Chuo Kikuu cha Ufundi cha Kenya (TUK). Kampeni za kipute hicho zilionekana kuwasha moto zaidi kuliko muhula uliyopita.
Githurai Allstars na Jericho Allstars zilitifua kivumbi kikali ambapo zilikuwa zikitwaa usukani wa mechi hizo moja baada ya nyingine.
Kocha wa Mathare Flames wakati mmoja alinukuliwa akisema, Walipania kutwaa ubingwa wa kinyang’anyiro hicho baada ya kumaliza katika nafasi ya pili mara mbili kisha kuibuka nafasi ya tatu simu uliyotangulia.
Hatimaye Meltah Kibiria ilifanya kweli na kuibuka wafalme wa kipute hicho kwa kuzoa alama 61, moja mbele ya Githurai Allstars.
Nao wanasoka wa TUK waliteleza na kufunga tatu bora kwa kuzoa alama 53, nne mbele ya Mathare Flames huku MASA kwa kuvuna pointi 51 ikimaliza ya tano. Jericho Allstars iliyokuwa mabingwa watetezi ilimaliza katika nafasi ya sita kwa kukusanya alama 50.
Mathare Flames iliyopatikana katika mtaa wa Mathare Area 4, Nairobi ilianzishwa mwaka 2004 na kujitwika jukumu la kukuza vipaji vya wanasoka chipukizi mitaani.
Mathare Flames imenoa makucha ya wachana nyavu wengi tu ambapo baadhi yao hushiriki soka la kulipwa katika mataifa ya bara Ulaya kama Derick Johana Omondi ambaye husakatia IF Brommapojkama nchini Sweden.
Pia wapo wengine zaidi ya wanane ambao hupigia klabu za Ligi Kuu ya KPL akiwamo Alphonce Ndonye (Mathare United), Robinson Kamura Mwangi (AFC Leopards) na Bernard Ongoma (Ulinzi Stars) zote Ligi Kuu ya KPL.
Pia imepalilia Kennedy Otieno-Spitfire FC(Ligi ya Taifa Daraja la Pili),James Mandela na Julius Gitau wote-Naivas FC (Ligi ya Taifa Daraja la Kwanza) na Victor Oduor Kwena-Bidco United (Supa Ligi ya Taifa-NSL).
Hata hivyo kocha huyo wa Mathare Flames, anasema anaamini kipute hicho kitaonyesha ushindani mkali zaidi misimu uliyopita.
”Bila kuweka katika kaburi la sahau napongeza Extreme Sports ya Hussein Mohamed ambayo huandaa mechi za kipute hicho,” alisema meneja wa Mathare Flames, Cainaib Webere.
Kinyang’anyiro hicho kimetoa fursa kwa wachezaji wengi tu kutambua talanta zao na kusajiliwa kuchezea timu za ligi za juu hapa nchini.
Baadhi ya wachezaji wa Shaurimoyo Blue Stars iliyopandishwa ngazi kushiriki kipute cha Super Eight Premier msimu ujao.