YUKO SANA! Ole kubakia licha ya mashabiki kuchemka
Na MASHIRIKA
MANCHESTER, Uingereza
MASHABIKI wa Manchester United wanataka Ole Gunnar Solskjaer atimuliwe licha ya kocha huyo kuomba muda alainishe mambo baada ya “mashetani wekundu” kupoteza 2-0 dhidi ya Burnley, Jumatano.
Ripoti za mtandao wa Sky Sports jana zilisema kwamba usimamizi wa klabu hiyo umeafiki kusimama na kocha huyo hadi timu ipate matokeo mazuri.
Chris Wood na Jay Rodriguez waliona lango mara moja kila mmoja United ikiaibishwa mbele ya mashabiki wake uwanjani Old Trafford.
Vijana wa Solskjaer walikosa ubunifu. United inatamani sana kukamilisha msimu katika nafasi za kuingia Klabu Bingwa Ulaya msimu huu. Hata hivyo, timu hiyo sasa iko katika nafasi ya tano kwa alama 34, alama sita nje ya mduara huo wa nne-bora.
Na, mashabiki wa United sasa wameongeza sauti wakitaka kocha huyo kutoka Norway aachishwe kazi.
Walianza kuchemka baada tu ya dakika ya 60, huku United ikiwa chini mabao mawili na ikikodolea macho kupewa dozi sawa na iliyopokea kutoka kwa Liverpool mnamo Januari 19.
“Simama kama unachukia familia ya Glazers,” mashabiki wa upande wa Stretford End waliimba, huku mashabiki wa sehemu zingine za uwanja pia wakiinuka kutoka viti vyao kuonyesha kuudhika kwao.
Zilikuwepo nyimbo zingine, moja mbaya sana iliyoelekezewa wamiliki wa United na pia Afisa Mkuu Mtendaji Ed Woodward. Baada ya kipenga cha mwisho kulia, mashabiki walipiga kelele za kuonyesha masikitiko yao.
Ni mara ya kwanza kabisa United ilipoteza dhidi ya Burnley uwanjani Old Trafford tangu mwaka 1962. Burnley haikuwa na ushindi uwanjani humu katika mechi 21 zilizopita.
Mara ya mwisho Burnley ilikuwa imevuna ushindi Old Trafford ilikuwa Septemba 22 mwaka 1962 ilipowika 5-2.
Vijana wa Solskjaer walipigiwa upatu kufanya vyema Jumatano. Matarajio yalikuwa makubwa, hasa walikuwa wamekanyaga Burnley 2-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza Desemba 28 mwaka jana.