SHANGAZI AKUJIBU: Nasubiri kupata kazi kwanza kisha nitafute mpenzi

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Mimi ni mwanafunzi wa mwaka wa mwisho katika chuo kikuu. Mimi sina mpenzi ingawa wengi wa marafiki zangu wameshapata. Nimeshindwa kuamua iwapo ninafaa kuwa na mpenzi sasa ama ninafaa kusubiri hadi nitakapoweza kujitegemea kimaisha. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Mapenzi na ndoa ni halali kwa yeyote ambaye ametimiza umri wa miaka 18 kwa sababu anachukuliwa kuwa mtu mzima. Hata hivyo, ninaamini kuwa tunda la uhusiano wa kimapenzi ni ndoa kisha familia. Kwa sababu hiyo, ni bora zaidi kwa mtu, hasa mwanamume, kuingia katika uhusiano wa kimaisha anapopata kazi ya kumwezesha kujitegemea kimaisha yeye mwenyewe na pia kutunza familia.

 

Kidosho wa zamani anadai tulizaa naye lakini siamini

Kwako shangazi. Nilikutana juzi na msichana tuliyekuwa wapenzi na tukaachana miaka miwili iliyopita. Ana mtoto na anadai ni wangu lakini sina hakika. Nishauri

Kupitia SMS

Kama alikuwa mpenzi wako na hamjaonana kwa muda huo inawezekana kuwa mtoto ni wako ama pia awe wa mtu mwingine. Jinsi pekee ya kujua ukweli ni kupimwa hospitalini.

 

Alinipagawisha sana kabla sijajua ni kiruka njia, sasa ananitisha

Shikamoo shangazi! Tafadhali naomba unisaidie. Nimeoa na ninafanya kazi mbali na nyumbani. Nimekuwa katika uhusiano kimapenzi na mwanamke fulani kwa miezi miwili sasa na nimegundua ana uhusiano na wanaume wengine. Nimeamua kumuacha na sasa anatishia kunidhuru. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Unafaa kujilaumu wewe mwenyewe kwa masaibu yoyote ambayo huenda yatakupata kutokana na vitisho vya mwanamke huyo. Sababu ni kwamba ulianzisha uhusiano huo ukijua ni haramu kwa sababu una mke. Pili, unamlaumu mwanamke huyo kwa kuwa na wanaume wengine ilhali wewe pia una uhusiano naye licha ya kwamba una mke. Pambana na hali yako.

 

Nimekata tamaa kungoja jibu lake ni miezi sita sasa

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 29 na bado sijapata mpenzi. Kuna mwanamke fulani ambaye ameteka hisia zangu na nimemwambia. Huu sasa ni mwezi wa sita nikimfuata na ananiambia bado hana jibu la ombi langu. Je, nisubiri hadi lini?

Kupitia SMS

Muda ambao umempa mwanamke huyo kufikiria kuhusu ombi lako unatosha na inashangaza kwamba kufikia sasa hana chochote cha kukwambia. Kuna uwezekano mkubwa kuwa hakutaki lakini anashindwa kukwambia. Sasa ni juu yako uamue iwapo utampa muda zaidi ama utaachana naye utafute mwingine.

 

Fitina za rafiki yake zilifanya nimuache, natamani kumrudia

Kwako shangazi. Nilimuacha mpenzi wangu baada ya rafiki yake wa karibu kuniambia alikuwa na uhusiano na mwanamke mwingine. Nilimuuliza akasisitiza kuwa hana mwingine lakini sikumwamini. Nimechunguza na kuthibitisha kuwa habari hizo zilikuwa za uongo. Natamani sana kumrudia mpenzi wangu lakini sijui nitaanzia wapi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Utajilaumu mwenyewe kwa kuchukua hatua kutokana na udaku. Licha ya mpenzi wako kukuhakikishia kuwa hakuwa na mwingine, uliamua kumwamini rafiki yake ingawa hukuwa na ushahidi wowote kuhusu habari hizo. Ungesubiri kwanza ufanye uchunguzi wako ili kujua ukweli wa madai ya rafiki yake. Iwapo unajua hajapata mwingine, mtafute umuombe msamaha kisha umwelezee nia yako ya kutaka mrudiane.

 

Mahanjamu hayapo tena ilhali ni miaka miwili tu, nifanyeje?

Hujambo shangazi? Nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili sasa. Lakini naona mapenzi yake kwangu yamepungua ni kama kwamba hana hisia kwangu tena. Inawezekana amepata mwingine?

Kupitia SMS

Iwapo amepunguza mahaba yake kwako bila wewe kumkosea, kuna kitu kinachoendelea maishani mwake na hasa inawezekana amenaswa kimapenzi na mwanaume mwingine na anaona vigumu kukwambia. Ni muhimu ujue mapema msimamo wake usije ukaendelea kupoteza wakati zaidi kwake.

Habari zinazohusiana na hii