Michezo

RAGA ZA DUNIA: Shujaa yaanza vibaya kampeni yake ya duru ya tatu

January 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya raga ya wachezaji saba kila upande ya wanaume ya Kenya almaarufu Shujaa imeanza kampeni yake ya duru ya tatu ya Raga za Dunia vibaya mjini Hamilton, New Zealand, Jumamosi.

Shujaa, ambayo inanolewa na raia wa New Zealand Paul Feeney, ilitupa uongozi wa alama 19-5 ikipoteza 24-19 dhidi ya Uingereza katika mechi yake ya kwanza ya Kundi B kabla ya kukabwa 12-12 na timu alikwa Japan katika mechi yake ya pili.

Dhidi ya Japan, Alvin Otieno aliweka Kenya kifua mbele 5-0 baada ya kupachika mguso bila mkwaju dakika ya pili. Hata hivyo, Japan ilijibu na dozi sawia kupitia kwa Kippel Ishida dakika ya tisa.

Kisha, Daniel Taabu alirejesha Kenya mbele 12-5 alipopachika mguso na mkwaju wa mguso huo, lakini Japan ikapata alama za kusawazisha kupitia mguso wa Dai Ozawa ma mkwaju kutoka kwa Yoshikazu Fujita dakika ya 12.

Katika mechi ya ufunguzi, Collins Injera, ambaye wakati mmoja alikuwa mfungaji wa miguso mingi kwenye ligi hii ya duru 10, alisherehekea kucheza duru yake ya 80 tangu aanze kuwakilisha Kenya mwaka 2007.

Aliongoza Shujaa kuingia uwanjani katika mechi ambayo William Ambaka alifunga miguso miwili katika kipindi cha kwanza. Ambaka alitimka karibu mita 70 kufunga mguso wa kwanza baada ya kuwachenga walinzi wa Uingereza. Taabu alikosa mkwaju wa mguso huu.

Uingereza ilisawazisha 5-5 kupitia mguso wa Ollie Lindsay-Hague kabla ya Injera kuchangia katika mguso wa pili wa Ambaka baada ya kupasia Billy Odhiambo mpira ambaye kisha alipeana pasi kwa Ambaka na kupata mguso chini ya milingoti. Taabu aliongeza mkwaju.

Sekunde chache baadaye, Kenya iliongeza mwanya 19-5 baada ya nahodha Andrew Amonde kufunga mguso wa tatu ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Taabu.

Kenya ilikamilisha kipindi cha kwanza kwa kufungwa mguso na mfungaji wa miguso mingi duniani kwenye raga hizi, Dan Norton na kuenda mapumzikoni alama saba mbele ya Waingereza hao.

Shujaa ililegea katika kipindi cha pili na kujutia kufanya hivyo kwani Uingereza iliinyima mipira na kuifunga miguso miwili pamoja na mkwaju mmoja bila jibu.

Yalimwa mechi saba mfululizo

Kenya iliingia mchuano huu bila ushindi dhidi ya Uingereza katika mechi zote sita ilikutana nao nchini New Zealand tangu mwaka 2004. Vilevile, Shujaa sasa imelimwa na Uingereza katika mechi saba mfululizo tangu duru ya Singapore mwaka 2018.

Vijana wa Feeney waliingia mechi ya Japan wakiuguza kuchapwa 26-17 walipokutana mara ya mwisho nchini Uingereza mwezi Mei 2019. Hata hivyo, ilikuwa mara ya kwanza kabisa Kenya na Japan zilikutana nchini New Zealand.

Baada ya mechi mbili za kwanza za makundi, ambapo pia Afrika Kusini ililimwa 21-19 na Uingereza baada ya kuchabanga Japan 31-5, Uingereza inaongoza kundi hili kwa alama sita.

Afrika Kusini imezoa alama nne, Kenya tatu nayo Japan iko mkiani kwa alama sawa na Kenya, lakini imefungwa alama nyingi. Kenya itakamilisha mechi zake za makundi usiku wa kuamkia Januari 26. Timu zitakazoshinda makundi yao zitaingia nusu-fainali.

Kundi A linaleta pamoja New Zealand, Marekani, Scotland na Wales, Canada, Ufaransa, Ireland na Uhispania zinapatikana katika Kundi C nazo Argentina, Australia, Fiji na Samoa zinaunda Kundi D.