Michezo

GOLD COAST AUSTRALIA: Kibarua kizito kumbwaga Nijel Amos mita 800

April 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

KIBARUA kizito kitakachowasubiri Alhamisi alasiri Wakenya Jonathan Kitilit na Wycliffe Kinyamal nchini Australia ni jinsi ya kusuka njama itakayofaulu kuyazima makali ya mtimkaji mahiri wa Botswana, Nijel Amos katika fainali ya mbio za mita 800 kwa upande wa wanaume.

Amos, 24, aliwahi kumnyamazisha David ‘The King’ Rudisha ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 800 kwa kuitawala fani hiyo kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola iliyoandaliwa jijini Glasgow, Scotland mnamo 2014.

Amos aliishindia Botswana medali ya kwanza katika Michezo ya Olimpiki kwa kujizolea nishani ya fedha katika Olimpiki za 2012 zilizondaliwa jijini London, Uingereza alishikilia uongozi wa Kundi la pili kwenye mchujo wa mbio hizo mnamo Jumanne kwa kusajili muda wa dakika 1:45.12.

Kitilit alifuzu kwa fainali ya leo baada ya kutawala Kundi la kwanza la mchujo wa nusu-fainali kwa muda wa dakika 1:47.27 mbele ya Jake Wightman wa Scotland aliyeambulia nafasi ya pili kwa muda wa 1:47.43.

Kinyamal aliongoza mchujo wa Kundi la tatu la nusu-fainali kwa muda wa dakika 1:45.56 mbele ya Mwingereza Kyle Langford ambaye pia alifuzu baada ya kuibuka wa pili kwa muda wa dakika 1:45.61.

Mtimkaji Cornelius Tuwei alikosa tiketi ya fainali na hivyo kukatiza ndoto za Kenya za kunyakua angalau nishani tatu kwenye mbio hizo za mita 800 baada ya kuzidiwa maarifa na wapinzani wake kwenye mchujo wa nusu-fainali.

Tuwei alimaliza wa tatu kwa muda wa dakika 1:47.10 nyuma ya Luke Mathews aliyesajili muda wa dakika 1:46.53.