KINA CHA FIKIRA: Tufurahikie hatua ya wenzetu kupigia upatu Kiswahili ughaibuni
Na KEN WALIBORA
WELEDI wa Kiswahili mara nyingi hupata milango ya rehema pahali wasipopatarajia.
Watangazaji wa Kiswahili mathalan wamejikuta wamegura kwao Afrika Mashariki wakenda kwenye vituo vya matangazo katika nchi ambako hawakuwahi kufikiria wataishi na kufanya kazi.
Watangazaji wa asili ya huku kwetu wamejikuta Japan, Moscow, India, Afrika Kusini, Marekani, Ujerumani na Uingereza kutokana na weledi wao wa Kiswahili. Ndiyo maana majina kama Billy Omalla, Fred Manju, Carol Robi, Mohamed Ghassany, Osman Miraji, Mohamed Ramadhani, Ramadhani Ali yametikisa mawimbi ya idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani DW kwa miaka na mikaka.
Raha iliyoje kuwasikia weledi hao wakibainisha uhondo wa Kiswahili ughaibuni katika redio za kimataifa! Hawa ni mabalozi wakubwa wa Kiswahili na kitovu chake cha Afrika Mashariki.
Lipo kundi jingine la weledi ambao nao wametoa mchango mkubwa kwa kuwa mabalozi wa Kiswahili. Hawa ni walimu wa Kiswahili waliozagaa kote duniani, wengi wao wakiwa na usuli wa huku kwetu Afrika Mashariki. Watu wa asili ya huku wamefundisha na wanafundisha Kiswahili katika asasi mbalimbali Japan, Korea Kusini, Marekani, Meksiko, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Ubelgiji, Ujerumani na nchi nyingine nyingi.
Hivi karibuni Prof Hermas Mwansoko amekuwa profesa mgeni huko China, Prof Kitheka wa Mberia huko Korea Kusini na Prof Fikeni Senkoro huko Namibia. Sote sisi tunapaswa kufurahikia na kushangilia jitihada za wenzetu kukipigia upatu Kiswahili kwa ufundishaji wao miongoni mwa wanafunzi wa ughaibuni.
Ninasisitiza kwamba sharti tufurahie mafanikio yao ambayo kwa kweli ni yetu. Wenzetu wanapokwenda ughaibuni kutangaza Kiswahili redioni au kufundisha Kiswahili madarasani tusiwaonee gere. Gere ndiyo adui mkubwa wa mafanikio ya utanuzi wa Kiswahili kwenye ulingo wa dunia yenye utandawazi. Mara nyingi gere hukitwa kwenye msingi wa utaifa, hisia zilizopindukia za utaifa ambazo huziba macho na kutokuona uzuri, ufundi na wema wa wa mtu ila taifa lake.
Taifa hilo limeibuka tena wakati wa tangazo la nafasi ya ajira ya ufundishaji wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha St. Lawrence Marekani. Chuo hiki ndiko alikowahi kufundisha Khalid Kitoto, Hamisi Babusa na kwa sasa Rachael Maina, wote kutoka Kenya. Hili la mkururo wa walimu kutoka Kenya kuwa ndio wanaoajiriwa kufundisha Kiswahili St. Lawrence, limezua rabsha na rangaito miongoni mwa watu waliolemazwa na utaifa. Palitokeza maoni kwenye ukumbi mmoja wa kijamii mtandaoni yaliyodai kwamba hilo si haki, yaani si haki kwa chuo hicho kuendelea kuajiri Wakenya tu.
Majibizano yaliyofuata yalikuwa na mihemko na ghaghabu na ghamidha si haba. Mimi sikusema lolote, langu jicho kama kawaida katika masuala yanayoibua mizozo ya aina hiyo mtandaoni. Hata hivyo, nilifarijika kuona Watanzania wengi wakipinga maoni haya yaliyojikita katika utaifa. Hili linathibitisha kwamba ingawa tuna mipaka ya kitaifa, weledi wengi hawajalevywa na kasumba ya utaifa.
Tunajenga nyumba moja mbona tunapigania fito?