• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
SEKTA YA ELIMU: Serikali iipige jeki elimu ya watoto wenye ulemavu

SEKTA YA ELIMU: Serikali iipige jeki elimu ya watoto wenye ulemavu

Na CHARLES WASONGA

INGAWA serikali imeazimia kufikia azma ya elimu kwa wote kwa kuendelea kufadhili mpango wa elimu bila malipo idadi kubwa ya watoto wenye mahitaji maalum hawafaidi kwa mpango huo.

Uchunguzi umeonyesha kuwa baadhi ya wazazi “huwaficha” watoto walemavu majumbani kwa misingi ya imani potovu kwamba hamna thamani yoyote kumpeleka mtoto mlemavu shuleni.

Wengine hukatiza masomo yao mapema kwa sababu ya umasikini kwani wazazi wao hushindwa kumudu gharama ya mahitaji katika shule chache za masomo maalum.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi punde kutoka wizara ya Elimu, takriban watoto 100,000 wenye mahitaji maalum kutokana na ulemavu bado hawajasajiliwa shuleni. Serikali nayo haijaelekeza rasilimali za kutosha katika sekta ya elimu ya watoto walemavu.

Kwa mfano, kuna uhaba mkubwa wa walimu na vifaa hitajika katika takriban shule 2,000 za msingi za msingi za watoto walemavu.

Hii ndio maana, kwa mfano katika mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka jana shule za msingi za walemavu ziliwasilisha jumla wa watahiniwa 2,118 pekee.

Na mnamo 2018 ni walemavu 2,097 walifanya mtihani huo kote nchini.

Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule hizo (SSHAK) Arthur Injenga anasema miongoni wa watahiniwa wa KCPE kutoka shule hizo mwaka jana ni wanafunzi 1,089, pekee waliofaulu kujiunga na shule za upili.

“Inasikitisha kuwa idadi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika vyuo vikuu 70 vya umma na vya kibinafsi ni 645 pekee,” akasema alipohutubu katika mkutano wa chama hicho uliofanyika Nairobi

Akaongeza: “Taasisi za kutoa elimu maalum zinakabiliwa na uhaba wa vifaa vya mafunzo kwa sababu ni ghali mno hali inayochangiwa na hatua ya serikali kutoza ushuru wa juu kwa bidhaa hizo hasa zinazoagizwa kutoka mataifa ya nje”.

Bw Injenga alisema picha kidogo ambazo shule hizo hupokea kwa ajili ya kununua vifaa vya masomo hutumwa kuchelewa.

Kwa mfano, katika mwaka wa kifedha wa 2018/ 2019 sekta ndogo ya masomo maalum ilitengewa Sh400 milioni pekee ilhali iliwasilisha bajeti ya Sh900 milioni.

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Nchini (Knut) Wilson Sossion ambaye ni miongoni mwa wajumbe waliohudhuria mkutano huo katika Taasisi ya Mafunzo Maalum (KISE) aliitaka wizara ya elimu kukabiliana na changamoto zinazokabili elimu ya watoto wenye mahitaji maalum.

Aliitaka serikali kuanzisha mpango wa elimu bila malipo kwa watoto wenye mahitaji maalum kutoka kiwango cha chekechea hadi vyuo vikuu.

“Serikali imekuwa ikiwabagua watoto walemavu kwa muda mrefu sana. Ubaguzi huu unapasa kukoma kwa serikali kuanzisha mpango wa masomo bila malipo kwa watoto hawa kuanzia katika shule za nasari hadi vyuo vikuu.

Hii ndio njia ya kipekee itakayowezesha watoto wenye changamoto za kimaumbile kupata fursa ya kusoma,” akasema Bw Sossion.

Vile vile, Bw Sossion aliitaka Tume ya Kuajiri Walimu Nchini (TSC) kuajiri walimu zaidi katika shule za walemavu.

“Changamoto ya uhaba wa walimu itapungua ikiwa TSC itaajiri walimu 5,000 katika shule hizo mwaka huu kuongezea walimu 10,560 walioko sasa. Mishahara na mazingira ya utendakazi wa walimu hao pia yanafaa kuboreshwa,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

KAULI YA MATUNDURA: Mgogoro wa ushairi wa Kiswahili...

MBURU: Uhuru, Ruto na Raila hawajajitolea kutetea raia

adminleo