Makala

Umuhimu wa kuingia maabadini mapema kabla ya mahubiri, mafundisho kuanza

January 29th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

WAKATI wa ibada, misa, na mafundisho ya kidini, baadhi ya washirika na waumini hufika katika maeneo ya kuabudu wakati padre au mhubiri anaendelea kulisha walioko chakula cha kiroho.

Kimsingi, wanafika wakiwa wamechelewa, na ni jambo linaloonekana kutatiza shughuli za mhubiri.

Si mara moja au mbili umeshuhudia wengine wakiingia hekaluni kwa viatu vinavyotoa sauti, hususan vyenye visigino virefu; stiletto.

Ni hatua ambayo hulazimu mhubiri kusitisha mahubiri, ili hekalu kutulia.

Kwa upande wa Waislamu, huvua viatu wanapoingia msikitini.

Kwa hakika, ni kitendo kinachoudhi ikizingatiwa kuwa ni siku maalum kumshukuru Mwenyezi Mungu, na inashuhudiwa mara kwa mara.

Kulingana na Padre Paul Kanyi wa Kanisa la Katoliki la Madre Teresa, Parokia ya Zimmerman, Nairobi, inapaswa kufahamika hatuendi katika maeneo ya kuabudu kwa ajili ya mtu yeyote yule ila kwa minajili ya Mwenyezi Mungu.

Padre Kanyi anasema siku ni saba kila wiki, na ni moja pekee imetengwa kuenda kanisani.

“Isitoshe misa ni ya saa chache tu, kwa nini usifike mapema kabla ibada kuanza?” anahoji.

Katika mchakato huo, suala la kujipanga mapema linajumuishwa ambapo kasisi huyo anasema Mola ni Mungu mwenye mpangilio, kutokana na neema zake kwetu.

“Huwa amepangia kila mmoja mema, licha ya changamoto zisizokosa kuibuka. Zinajiri kuweka kwenye mizani imani zetu,” Padre Kanyi anaeleza.

Hebu jisaili, siku unayofika hekaluni ukiwa umekawia ingekuwa anayorejea Yesu, ungemuwahi?

Padre huyo anasema hakuna jambo linaloridhisha Mwenyezi Mungu kama kuona moyo wako u tayari kumpokea pamoja na mafunzo yake. Kufuatia hilo, Kanyi anaeleza ni muhimu katika kila jambo kutangulia na Mungu na kufunga na Mungu.

Ubatizo ni mojawapo ya hatua inayotiliwa mkazo kanisani, ni utakaso unaoosha dhambi, kwa mujibu wa mafunzo ya Yesu Kristu ambaye pia alibatizwa kwa ajili ya dhambi zetu sisi.

“Katika kanisa la Kikatoliki, kabla kubatizwa kuna mafunzo ambayo mmoja hupitia, na yamefafanua suala la kuheshimu misa,” Padre anasema.

Kwenye muktadha unaowiana na huo, iwapo umefika kanisani padre akiwa ameanza ibada, kwa njia ya kukariri ishara ya msalaba, hupaswi kupokea Sakramenti ya mkate uliotakaswa.

Ni kauli inayotiliwa mkazo na Padre Charles Kinyua, akihimiza umuhimu wa washirika kufika mapema, ikiwezekana dakika kumi kabla ya misa kung’oa nanga.

“Kwa mfano, ikiwa ibada inaanza saa tatu kamili, ni vyema uwe umewasili dakika 10 kabla. Muda huo kwaya hutumbuiza kwa nyimbo za kutuliza nyoyo na kutuandaa kushiriki misa,” anafafanua Kinyua.

Kwa mfano, nchini Rwanda inasemakana washirika hufika kanisani dakika kadha kabla mhubiri kuanza misa.

“Tulishangaa kuona washirika kule, Rwanda, hufika dakika ishirini kabla padre kuingia. Muda huo nyimbo za kumshukuru Mungu huhinikiza hekalu, ni waadilifu,” mwenyekiti wa kwaya ya Madre Teresa akaambia washirika Jumapili iliyopita, baada ya kufanya ziara ya kipekee nchini Rwanda mapema mwaka 2020 pamoja na kundi la wanakwaya kadhaa.

Alisema hadhi ya usafi nchini huyo ni ya kupigiwa upatu, mengi ya maeneo waliyozuru yakiwa ni nadhifu.