Jinsi nyumba za mawe zinavyodhibiti mikasa ya moto mitaa ya mabanda
Na SAMMY KIMATU
UTAJAPO moto, nywele za wakazi katika mitaa ya mabanda ya Mukuru na mingine kwingineko katika kaunti ya Nairobi husimama.
Kutokana na kushududiwa kwa msururu wa visa vya moto kutokea mitaani, vifo vimeripotiwa, waathiriwa hupoteza mali isiyohesabika huku maendeleo yakivurugwa.
Badaa ya kuona wiki baada ya wiki, mwezi baada ya mwezi na mwaka baada ya mwaka nyumba zikiteketea, mwakilishi wa Wadi ya Landi Mawe alileta hoja ya kunusuru wakazi.
Bw Herman Azangu almaarufu Kaimosi aliomba watawala kuruhusu ujenzi wa nyumba zinazoweza kudhibiti moto.
Ndiposa katika mkutano wa usalama ulioongozwa na wakati huo mkuu wa tarafa ya Makadara, Bi Margaret Mbugua, Bw Azangu alitoa kauli yake kuhusu ongezeko la visa vya moto mitaani ya mabanda ya Mukuru.
Mkutano huo ulifanyika katika eneo la Kambi Moto katika mtaa wa Mukuru-Kaiyaba ulioko katika kaunti ndogo ya Starehe mwaka 2010.
“Tafadhali madamu uliye mkuu wa tarafa yetu ya Makadara, serikali ituruhusu kujenga kwa mawe mtu akiwa na uwezo ndiposa kukiwa na moto tusipoteze maisha na nyumba nyingi,” akasema Bw Azangu.
Viongozi mbalimbali walitoa kauli zao na kuzungumzia jambo hili kwa kila mkutano uliofanywa wa hadhara.
Na baada ya miezi michache, wakazi wakaanza kujenga nyumba za mawe.
ZIlizokuwa za mwanzo mwanzo zilikuwa ni nyumba zilizojengwa za orofa moja.
Aidha, siku zilivyoendelea kusonga mbele, watu waliiga mtindo huo na kufuata njia hiyo ya kujenga kwa mawe.
Kutoka orofa ya kwanza wamiliki wa nyumba waliendelea kujenga nyumba hadi orofa ya pili na baadaye ikafika orofa ya nne.
Kabla ya nyumba za mawe kujengwa mitaani, nyumba zilikuwa zikijengwa kwa kutumia mabati.
Na kutokana na hali ilivyo kimazingira, aliyekuwa kwa kipindi fulani mkuu wa wilaya ya Makadara, Bw Suleiman Chege aliwakosoa wakazi kuhusu masuala ya nyumba.
Bw Chege, katika mikutano yake ya hadhara , alisema katika mitaa ya mabanda hakuna jina house (nyumba) na badala yake ni mabanda.
Vilevile, yeyote kujiita Landlord ni makosa na badala yake ni structure owner (mwenye kibanda/mabanda).
“Hii ni kwa sababu kisheria, na kupitia kwa wizara ya ardhi na masuala ya nyumba na ujenzi, haya ni makaazi duni, hayana namba ya ploti wala hakupeanwi hati miliki ya mashamba,” Bw Chege akanena.
Hali ilikuwa hivyo hadi pale mambwanyenye walianza kununua nyumba za mabati na kuzijenga tena kwa kutumia mawe.
Chambilecho wahenga, barabara ndefu haikosi kona, wapangaji hugharamika kulipa zaidi nyumba zikijengwa kwa mawe.
“Kodi ya nyumba ya mabati ni kuanzia Sh2,000 na Sh3,500 ikiwa haina na ikiwa ina stima mtawalia. Ikijengwa kwa mawe, kodi huwa ni kati ya Sh5,000 na Sh6,000 kwa kila mwezi,” akasema Bw Cosmas Mumo ambaye ni fundi wa stima.
Baadhi ya wakazi waliohojiwa na ‘Taifa Leo’ walisema tangu nyumba zijengwe kwa mawe, visa vya moto vimepungua kwa zaidi ya asilimia 90.
Zaidi ya hayo, visa vya moto vinavyotokea, kuta za nyumba za mawe hupunguza ndimi za moto na kuzuia moto kuenea na nyumba zaidi haziteketei.
Vilevile, kuna wamiliki wa nyumba ambao wamejawa na tamaa ya kupindukia huku wengine wakijenga chini ya nyaya za stima zenye nguvu nyingi yenze uzito wa 11kv.
Wengine wamesukuma na kubana mto Ngong baada ya kumwaga mchanga na kupanga magunia yaliytojazwa mchanga kutoka mtoni kisha mkondo wa maji hubadilishwa na nyumba kujengwa juu.
Jambo jingine linalochangia kuwa na ongezeko la nyumba za mawe mitaani ya mabanda ya Mukuru ni kwamba ardhi mitaani imenyakuliwa kiasi cha kutowachia watoto nafasi ya kuchezea.
“Wachana na uwanja wa watoto kuchezea mitaani hii, ukiwa na mkasa wa moto, huwa hatuna mahali pa kuokolea mali yetu kwa sababu wamejenga mpaka verandah za nyumba,” Bw Charles Mati akasema.
Kando na hayo, ongezeko la uhamiaji wa watu kutoka mashambani hadi mijini pia umechangia pakubwa.
Kutokana na mfumko wa uchumi, bei ya kununua nyumba ya mabati vijini imeenda juu kutoka Sh50,000 hadi Sh120,000 kwa kila nyumba iliyojengwa ya ukubwa wa futi kumi kwa kumi (10’’X 10’’) na mara nyingine futi tisa kwa tisa.
“Ukifanikiwa kununua zile nyumba za kitambo zilizokuwa za futi 10 kwa 10, uko pazuri kwa sababu nafasi ya nyumba yako itakuwa kubwa ikilinganishwa na unaponunua za vyumba vidogo,” mbwanyenye mmoja aliyeomba tusiandike jina lake akasema.
Baadhi ya wamiliki wa nyumba za mawe waliohojiwa walikiri kwamba ni hali ya kutafuta na ikiwa nyumba zenyewe zitakuja kubomolewa, hawawatajuta bora walikusanya faida ya kodi kwa miaka kadhaa.
‘’Yule atakutwa nyumba yake ikiwa haijarudisha pesa za gharama yake huyo ndio bahati yake itakuwa mbaya kwa sababu Nairobi tulikuja kutafuta pesa na wala sio kutafutana,” Mmiliki mmoja wa nyumba za mawe akasema wakati wa mahojiano.