Ni rasmi James Nyoro ndiye Gavana wa Kiambu
Na SAMMY WAWERU
JAMES Nyoro ameapishwa rasmi Ijumaa awe Gavana mpya wa Kaunti ya Kiambu ambapo kiapo kimesimamiwa na Jaji John Onyiego na sherehe ikiongozwa na Dkt Martin Njogu Mbugua.
Nyoro ambaye amekuwa Naibu Gavana amechukua hatamu siku chache baada ya bunge la seneti kupitisha kuvuliwa wadhifa kwa aliyekuwa Gavana Ferdinand Waititu anayekabiliwa na mashtaka ya ufisadi.
Sherehe ya kiapo imefanyika baada ya kuahirishwa Alhamisi.
Ijumaa, Januari 31, 2020, imenakiliwa katika kumbukumbu za Kenya baada ya Nyoro kutwaa wadhifa huo ikiwa ni baada ya kukamilika hatua zilizo rasmi za kumbandua Waititu.
Kwenye hotuba yake baada ya kulishwa kiapo kuwa gavana watatu Kiambu, Nyoro ameahidi kutatua matatizo yanayozingira wakazi wa kaunti hiyo.
Katika hotuba yake na iliyosheheni ahadi chungu nzima, pia ametaja kuwa hakuna atakayebeba msalaba wa mwingine.
Nyoro ametangaza kwamba kwa muda wa wiki mbili zijazo atabuni tume maalum ya kiushauri, itakayojumuisha wazee waliojitolea kuendeleza kaunti hiyo.
“Tume hiyo itasaidia kutoa ushauri kimaendeleo,” akasema.
Nyoro anakuwa gavana wa tatu wa Kiambu baada ya kuchukua mikoba kutoka kwa Waititu ambaye alimbandua bwanyenye William Kabogo mwaka 2017 katika uchaguzi mkuu.
Bw Waititu aliyewania wadhifa huo kwa tiketi ya chama tawala cha Jubilee, alizoa jumla ya kura 353,604 dhidi ya mpinzani wake William Kabogo, aliyepata kura 69,916 na ambaye alikuwa gavana wa kwanza Kiambu.
Waititu alifanikiwa kutwaa kiti hicho, chini ya vuguvugu la United 4 Kiambu lililojumuisha mgombea mwenza James Nyoro, Kasisi Kariuki Ngari maarufu kama Gakuyo na mbunge mwakilishi wa sasa Kiambu Gathoni Wa Muchomba.
Hata hivyo, mambo yalimharibikia Waititu alipoanza kutajwa kuhusishwa na sakata za ufisadi, ufujaji wa mali ya umma, ikiwa ni pamoja na utumizi mbaya wa mamlaka na ofisi.
Mradi wa Kaa Sober, na ambao Waititu alidai ulilenga kunusuru vijana waliotekwa na unywaji wa pombe kupindukia Kiambu pamoja na kuwatafutia ajira, ulikuwa mmoja wa uliosemwa kufuja mali ya umma.
Masaibu chungu nzima yaliibuka, gavana huyo akachunguzwa na tume ya maadili na kupambana na ufisadi, EACC, ofisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma, DPP ikachukua usukani na kumfikisha mahakamani baada ya kumpata na hatia.
Ni kupitia idara ya mahakama ambapo Waititu alipewa breki kuingia ofisini. Isitoshe, bunge la Kaunti ya Kiambu likamng’atua baadaye.
Kilele cha mchakato huo kikawa kutiwa muhuri mapema wiki hii na bunge la seneti, ambapo maseneta 28 walipiga kura kumuondoa ofisini. Aidha, 11 ndio walihisi Waititu anapaswa kuendelea kuhudumu kama gavana.
Wakati hilo likithibitishwa, Waititu si gavana wa Kiambu, Rais Uhuru Kenyatta naye amezindua ujenzi wa barabara Nyandarua akiweka wazi kuwa serikali yake haitasaza mafisadi.
Akizungumza kwa mafumbo, kwa lugha ya Gikuyu, na yaliyoonekana kulenga Waititu, kiongozi wa taifa amesema kila mmoja atakayepatikana na hatia kuhusishwa na ufisadi, ajitayarishe kubeba msalaba wake mwenyewe.
“Ulichaguliwa kufanyia Wakenya kazi lakini si kufuja mali yao. Ukila, ulisherehekea na mkeo, beba msalaba wako mwenyewe,” amesema Rais Kenyatta, akionya kuwa wembe uo huo utatumika kwa mafisadi wengine.
Akasisitiza: “Hii ni Kenya nyingine, si ile ya zamani.”
Baada ya kuchaguliwa kuhudumu awamu yake ya pili na ya mwisho, Rais aliweka wazi atatilia mkazo vita dhidi ya ufisadi, chini ya serikali ya Jubilee. Oparesheni ya ufisadi pia ni miongoni mwa ajenda zilizojadiliwa kwenye salamu za maridhiano kati yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga, na ambazo zilizaa jopokazi la maridhiano nchini (BBI).
Viongozi kadha serikalini, wakiwamo magavana na waziri wamejipata kuandamwa kwa tuhuma za ufisadi, ufujaji wa mali ya umma na utumizi mbaya wa mamlaka na ofisi.