Makala

Muthurwa: Kituo cha mabasi kilichogeuka jinamizi jijini Nairobi

January 31st, 2020 3 min read

Na BENSON MATHEKA

KILIPOFUNGULIWA rasmi miaka 13 iliyopita, kituo cha mabasi cha Muthurwa jijini Nairobi, kilinuiwa kuegeshwa magari ya uchukuzi wa umma, hasa yale ya kutoka sehemu za Mashariki mwa jiji la Nairobi.

Lengo la Serikali kupitia kwa aliyekuwa waziri wa Serikali za wilaya wakati huo, Bw Uhuru Kenyatta, lilikuwa kupunguza misongamano ya magari katikati mwa jiji kwa muda, huku azma kuu ikiwa ni kuwahifadhi wachuuzi waliokuwa wakiendesha shughuli zao katikati mwa jiji.

Miaka mitatu baada ya kuzinduliwa, ndoto hio ilianza kugeuka na kuwa jinamizi kwa wamiliki wa magari ya uchukuzi wa umma, madereva na wakazi wa jiji, huku habari zikidai kwamba huenda eneo kilikojengwa lilikuwa limeuziwa mstawishaji wa kibinafsi.

Hali katika kituo hicho ni mbaya mno huku kikikosa mpangilio maalumu na utaratibu wa usimamzi. Barabara zimejaa mashimo, kiwango cha usafi ni duni na hakina mpangilio wa kuegesha magari kutoka mitaa tofauti iliyoko mashariki wa jiji.

“Haya ni matatizo ambayo yamekikumba kituo hiki tangu mwanzo,” George Githinji mwenyekiti wa tawi la Mashariki mwa jiji la chama cha wenye matatu, MOA aliambia ‘Taifa Leo’ 2010.

Kufikia sasa, hali haijabadilika.

Hali mbovu katika kituo cha mabasi cha Muthurwa, Nairobi. Picha/ Benson Matheka

Serikali iliwaagiza wenye matatu kutoingiza magari yao katikati mwa jiji, na badala yake kuyaelekeza katika kituo hicho nao wanasema changamoto zimeendelea kuwaandama.

Wanasema kutokana na umbovu wa barabara, wenye matatu wamelazimika kuungana na kuwalipa vibarua, kwa minajili ya kukarabati baadhi ya sehemu zilizoharibika.

Kinachowauma ni kwamba vibarua wanaokarabati barabara hizo hukamatwa na maafisa wa baraza la jiji licha ya baraza hilo kupuuza wajibu wake wa kuteng’eneza miundo msingi.

“Sisi wenye magari tunakumbwa na hasara, kwani hali hii pia, inatulazimu kukarabati magari yetu yakiharibika angalau kila wiki, huku tukilazimika pia kununua vifaa ambavyo huharibika kila wakati,” mmiliki mmoja wa matatu aliambia Taifa Leo ilipozuru kituo hicho mapema wiki hii.

Kulingana naye , asilimia 30 ya mapato ya wenye matatu zinazoegeshwa katika sehemu hii, hutumika kukarabati magari yao. Gharama ambayo anasema ingepungua, iwapo serikali ya kaunti ingewajibika vilivyo.

“ Wamiliki wa matatu, wanalazimika kutumia rasilmali nyingi kushughulikia hali ya magari yao, ili waendelee kuwa katika biashara hii. Ni lazima kila matatu ikaguliwe na serikali kila mwaka, kabla ya kupewa leseni ya kuendelea kuhudumu katika sekta ya umma,”aeleza.

Wamiliki hao wanasema hali mbovu ya maeneo ya kuegesha magari, husababisha msongamano wa magari katika kituo hicho na hivyo kuwafanya abiria kususia kuyapanda kwa hofu ya kuchelewa kufika nyumbani.

“Misongamano husababishwa na barabara mbovu. Wakirekebisha barabara na kuzipanua misongamano itapungua na itakuwa afueni kwetu,” asema.

Kutokana na tatizo hili, matatu nyingi zinazoelekezwa Muthurwa hukosa wateja, na hivyo kuchukua muda mwingi kabla ya kuanza safari. Hii hupunguza hata zaidi mapato kwa washikadau na kufanya wakaidi sheria na kuingia kati kati ya jiji.

Hali mbovu katika kituo cha mabasi cha Muthurwa, Nairobi imeathiri shughuli nyingine kama vile biashara ya mboga na matunda. Picha/ Benson Matheka

John Maina, mwanachama wa shirika la wenye matatu la Outering Matatu Association (MOA) asema badala ya kupunguza misongomano na kuimarisha sura ya jiji, matokeo yamekuwa kinyume.

Kituo hicho cha magari ni kidogo mno na hakiwezi kutoshea matatu zote zinazohudumu mashariki mwa jiji. Fauka ya hayo, wachuuzi wamevamia sehemu moja ya kituo hicho na kunyima madereva nafasi ya kuegesha magari. “Wachuuzi wengi wamevuka mipaka na kunyakua sehemu zilizotengewa magari kutoka mitaa fulani, na hivyo kuathiri pakubwa mpangilio wa magari kuingia na kutoka kituoni. Hii ni sababu nyingine ya kutokea msongamano hapa,” alisema Bw Githinji.

Kulingana na Bw Maina, hali hii husababisha abiria wengi kuhofia kuyapanda magari yanayoegeshwa katika sehemu hii, na badala yake huabiri magari yanayoruhusiwa kuingia katikati mwa jiji.

Ajabu ni kwamba wachuuzi walionyakua sehemu zilizotengewa kuegesha magari wamefanya hivyo machoni mwa walinzi na maafisa wa serikali la jiji.

“Hapa ni hali ya mwenye nguvu mpishe. Ukilalia macho hutapata kitu. Lazima utoe kitu kidogo,”asema mchuuzi mmoja tulipomuuliza walivyoweza kuuzia bidhaa katika sehemu ya kuegesha magari.

Licha ya kukumbwa na changamoto hizi, wamiliki wa magari, hawapingi kuhudumu kutoka eneo hili, katika harakati za kupunguza idadi ya magari jijini. “Tunachohitaji ni huduma. Tunalipa kodi kwa serikali ya jiji na tunapaswa kupata huduma bora,” asema Maina.

“Pia itakuwa haki iwapo magari fulani hayatapendelewa na kuruhusiwa kuingia katikati mwa jiji, huku mengine kama yetu yakilazimishwa kubabea abiria hapa,”aliongeza