Makala

AKILIMALI: Baada ya kuchoshwa na ualimu aliamua kuzingatia ukulima

February 1st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na SAMMY WAWERU

KATI ya 2008 hadi 2010 Raphael Ngari alihudumu kama mwalimu wa shule moja ya upili kaunti ya Embu, ambapo alifunza Somo la Bayolojia na Kilimo.

Kulingana na Ngari, mshahara aliopata ulikuwa kiduchu kiasi cha kujipata akikopa kila mara katikati ya mwezi.

Anasema alihangaika si haba, kwa kile anataja kama “mahitaji kuzidi kwa kiwango kikuu pato langu”.

Wakati akiwa katika sekta hiyo, alikuwa akifanya kilimo muda wa ziada.

“Nilikuwa nikipanda mboga na nyanya ili kupiga jeki mapato yangu,” Ngari anasema.

Baada ya kuchoshwa na kutekwa nyara na madeni kila mwezi, Ngari aliamua kuchukua hatua nyingine. “Mwaka wa 2011 niliamua kuacha ualimu ili niingilie shughuli za kilimo kikamilifu,” amadokeza.

Ni hatua anayosema ilisimangwa na kukejeliwa, hasa na walimu wenza na vijana wa rika lake. Kilimo kinachukuliwa kama shughuli inayofanywa na wazee hususan baada ya kustaafu na watu wasio na uwezo, na kwa mujibu wa maelezo yake hayo ndiyo mafumbo aliyosemwa nayo.

Kijana huyo hata hivyo alitia maskio yake pamba, na kufuata moyo, waama kipendacho moyo dawa. Kwa mtaji wa Sh160, 000 alizokusanya kusanya kupitia kilimo cha ziada na akiba kiasi ya ualimu, aliingilia kilimo cha mahema, maarufu kama ‘greenhouse’.

Aliunda kivungulio chenye ukubwa wa mita 8 kwa 30, akalima pilipili mboga.

Zao hilo huanza kuvunwa miezi mitatu baada ya upanzi, na kuendelea kwa muda wa takriban miezi tisa mfululizo.

Ngari anaiambia ‘Taifa Leo’ kwamba alivuna mazao yaliyompa kima cha Sh125,000.

“Nilikadiria hasara ya Sh35, 000, sikufa moyo,” anasema mkulima huyo.

Ili kunoa bongo, Ngari alipata mafunzo ya kilimo bora cha mahema, kupitia taasisi ya kilimo na ufugaji nchini, Karlo. Kulingana na Jessica Mbaka, kutoka Karlo tawi la Thika, kilimo cha vivungulio kinahitaji umakinifu na mkulima anayekielewa.

“Si mimea yote inayozalishwa kwenye mahema. Nyanya, pilipili mboga, giligilani na spinachi hufanya vyema kwenye hema,” aeleza afisa huyo, akiongeza kusema kuwa mkulima anapaswa kujua namna ya utunzaji wa kivungulio na mazao.

Raphael Ngari alinolewa makali, na anasema 2012 alipanda nyanya zilizompa faida zaidi ya Sh300, 000. Ni kupitia mapato hayo, aliweza kuongeza vivungulio viwili zaidi.

Kijiji cha Mukangu, kilichoko eneo la Manyatta Kaunti ya Embu, wenyeji wamezamia kilimo cha majanichai, kahawa na macadamia. Aidha, pia kuna wanaolima mboga kama vile spinachi, kabichi na sukuma wiki.

Taswira hiyo ni tofauti na ya Ngari, ambapo amejituma katika kilimo cha pilipili mboga za rangi ya kijani, ambazo ni nyekundu, manjano na za kijani.

Kila kivungulio kikiwa na kimo cha mita nane kwa 30 mkulima huyo anasema kinasitiri karibu mipilipili 864.

Wakati wa mahojiano alisema mpilipili uliotunzwa vyema una uwezo kuzalisha kadri ya kilo tano.

Alisema kilo moja ni kati ya Sh80 – 200. Ngari alisema, gharama ya kuzalisha kivungulio kimoja ni karibu Sh45, 000. Gharama hiyo inajumuisha; mbegu, mbolea na fatalaiza ya kunawirisha mazao, dawa dhidi ya magonjwa na wadudu na leba. “Fatalaiza na dawa ndizo ghali sana,” akalalamika.

Licha ya pandashuka hizo zisizokosa katika shughuli za kilimo, mkulima huyo anasema mapato anayopokea yanapiku kwa kiwango kikuu mshahara aliopata kama mwalimu. Isitoshe, waliompiga vijembe, ndio sasa wanamuendea kupata mafunzo ya kilimo cha mahema.

Katika ruwaza yake ya miaka mitano ijayo, Ngari anapania kuongeza vivungulio vitatu zaidi, ili akimu mahitaji ya wateja wake wa pilipili mboga anaosema oda zimempiku.