Tanzia: Rais Mstaafu Daniel Arap Moi amefariki
Na BENSON MATHEKA
RAIS Mstaafu Daniel Toroitich Arap Moi, 1924 – 2020, amefariki; Rais Uhuru Kenyatta ametangaza mapema leo Jumanne.
Amefariki katika Nairobi Hospital ambako amekuwa akitibiwa mara kwa mara.
Rais Kenyatta ametangaza kuwa Mzee Moi, alifariki Jumanne asubuhi.
Msaidizi wa kibinafsi wa Mzee Moi, Lee Njiru pia amethibitisha kuwa Rais huyo wa pili wa Kenya ameaga dunia.
Akitoa tangazo, Rais Kenyatta amemtaja Mzee Moi kama kiongozi aliyejitolea kuwakuza na kuwaandaa viongozi wengine si tu nchini Kenya, lakini pia nje ya mipaka ya taifa.
“Rais Mstaafu Daniel Toroitich Arap Moi amefariki mapema leo (Jumanne) katika Nairobi Hospital ambapo familia yake imekuwepo,” inasema sehemu ya tangazo la Rais Kenyatta.
Katika salamu zake za pole, kiongozi wa nchi amefariji wanawe Moi, jamaa pana na marafiki kwa jumla katika kipindi hiki kigumu.
Bendera ya Kenya katika maeneo yote ya umma nchini na katika majengo ya balozi za Kenya katika mataifa ya kigeni itapeperushwa nusu mlingoti kuanzia leo Februari 4, 2020, hadi jioni siku ya mazishi.
Rais Kenyatta anatarajiwa kutoa taarifa kamili hivi punde.
Mzee Moi amekuwa akilazwa katika Nairobi Hospital tangu mwaka 2019.
Alitawala Kenya kwa miaka 24 tangu 1978 hadi 2002.
Aliingia mamlakani 1978 baada ya kifo cha aliyekuwa Rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta.
“Licha ya dua zao Moi aliongoza kwa miaka 24, miezi minne na siku nane,” alisema Bw Njiru, mmoja wa watu ambao waliaminiwa sana na Rais Moi.