Habari

Taifa laendelea kuomboleza vifo vya wanafunzi 14 Kakamega

February 4th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CAROLINE WAFULA

WAZAZI na viongozi mbalimbali wako katika Shule ya Msingi ya Kakamega ambapo Jumatatu kulitokea mkasa wa mkanyagano uliosababisha vifo vya wanafunzi 14 na kusababisha majeraha kwa wengine kadhaa.

Wazazi waliopoteza watoto wao nao Jumanne asubuhi wamefika katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kakamega kutambua miili ya wahanga.

Waliofariki ni wavulana watano na wasichana tisa. Kati ya hao, 12 walikuwa wanafunzi wa darasa la tano na wawili wa darasa la nne.

Ingawa bado hakuna ripoti ya kuelezea wazi kilichotokea, baadhi ya wanafunzi wamedai mwalimu fulani alikuwa akiwaharakisha waende nyumbani jioni na hivyo kusababisha mtafaruku.

Waziri wa Elimu George Magoha, Katibu Belio Kipsang na Gavana wa Kaunti ya Kakamega Wycliffe Oparanya wamefika shuleni humo Jumanne asubuhi ambapo wametathmini hali.

Wengine waliofika shuleni hapo ni Seneta wa Kaunti ya Kakamega Cleophas Malala, aliyekuwa seneta Dkt Boni Khalwale na msemaji wa serikali Cyrus Oguna.

Viongozi hao wamekutana na wakuu wa usalama wa kaunti na maafisa wa elimu na vilevile usimamizi wa shule.

Mara baada ya mkutano, viongozi wamewahutubia wazazi na wanafunzi.

Waziri Magoha amewafikishia waliowapoteza wapendwa wao salamu za pole kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta.

“Ninaleta hapa salamu za pole kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta na serikali yote kwa jumla,” amesema Prof Magoha.

Akaongeza: “Nimekuwepo katika hii shule nzuri na kushuhudia wanafunzi wakiteremka taratibu kutoka kwa ngazi za madarasa haya ya ghorofa.”

Pia ameelezea kushangazwa kwake na kilichotokea.

“Mimi ni Mkristo na ninataka ukweli wote kuhusu kilichotendeka ubainike. Aidha, ni matumaini yangu kuwa wanafunzi mlio hapa mtaendelea na masomo yenu bila tatizo lolote; tayari nimeingia katika madarasa manne na walimu wanafanya kazi ya kuridhisha,” amesema Magoha huku akiwafariji wazazi na kuwataka wote washirikiane kufanikisha shughuli za elimu.

Ingawa hivyo, amesema wameafikiana wanafunzi wapumzike kwa siku chache za wiki hii.

“Tutafungua vituo vya habari na nasaha kwa kipindi hiki matumaini yetu yakiwa ni kufungua shule hii Jumatatu wiki ijayo. Serikali itaendelea kuipiga jeki shule hii kuhakikisha ufanisi,” amesema.

Naye Gavana Oparanya ameelezea huzuni uliomvaa Jumatatu alipoingia katika mochari ambapo miili ya wanafunzi 13 ilikuwa imewekwa. Mwanafunzi mwingine alifariki baadaye akipokea matibabu.

“Tuna huzuni kupoteza wanafunzi wasiokuwa na hatia. Hii serikali ya kaunti itahakikisha inafanya kila iwezalo ili walioangamia wazikwe kwa heshima wanayostahili na naiomba pia serikali kuu itusaidie,” amesema Oparanya.