REDIO: Mawimbi haya yanafaa kuvumisha Kiswahili, si kukiua
NA STEVE MOKAYA
Kwa miaka na mikaka sasa, redio imekuwa ni chombo pendwa zaidi cha mawasiliano kwa watu mbalimbali: matajiri kwa maskini; wakubwa kwa wadogo, wazee kwa vijana.
Kipenzi hichi cha wengi kinapendelewa sana kwa sababu kina uwezo wa kufika kule vyombo vingine vyamawasiliano haviwezi kufika.
Redio huvuka mipaka, husikika juu milimani, chini mabondeni na hata maeneo ya mashambani. Na kutokana na hali ngumu ya uchumi, redio huwa mwokozi mtegemewa, ikilinganishwa na runinga ama hata tarakilishi.
Watu wengi sana hutegemea redio kupata maarifa, kupata taarifa za mambo mageni na yanayoendelea,na hata kuelimishwa.
Hata hivyo, sehemu hii ya redio katika jamii imekabiliwa na changamoto kabambe katika siku za hivi karibuni, na iwapo jambo halitafanywa, huenda tukapoteza chombo kipenzi, na rafiki mwaminifu kwetu.
Tangu kuzinduliwa kwake humu nchini, redio imekuwa na vipindi vya kuelimisha jamii, na vinavyoelekeza, na kuzingatia na kukuza mshikamano wa jamii kwa jumla.
Ila, siku hizi, vituo vingi vya redio, hasa vile vilivyochipuka katika siku za hivi nkaribuni, vimeanza kuacha mkondo huu.
Vituo hivi vina vipindi vinavyotumia lugha iliyo na upungufu mkubwa wa heshima. Mazungumzo na mijadala inayoendeshwa kwavyo ni ya kuogofya na mzazi na mwanawe hawawezi kuskiza wakiwa pamoja, kwa sababu ya aibu.
Isitoshe, lugha itumiwayo ni yenye kuvunja sheria zote za lugha. Vingi vya vituo hivi hutumia lugha ya sheng’ badala ya kuzingatia lugha za taifa ama lugha za mama.
Ni kutokana na matumizi ya lugha hii ya sheng’ ambapo tunashuhudia hata wanafunzi wa chekechea wanashindwa kuzungumza kwa lugha sanifu.
Ikumbukwe kuwa baadhi ya matumizi ya redio ni kuelimisha umma. Je, mawimbi ya redio zetu yanapofunza wasilikizaji kujua sheng’ zaidi ya lugha za taifa, yanatekeleza jukumu lake?
Kiswahili kinazidi kukua kila uchao, na haitachukua muda mrefu kabla iwe lugha ya bara Afrika. Tayari, mataifa kadhaa, kama vile Afrika Kusini na hata Libya yameanza mitaala inayozingatia Kiswahili shuleni na vyuoni mwao.
Hata Wazungu wameanza kujifunza Kiswahili sanifu. Iwapo mataifa ya kigeni yako mbioni kujifunza lugha hii tukufu, mbona vituo vyetu vya redio vinazidi kufanya kinyume? Tuwe makini kabla makubwa hayajatufika jameni.
Jambo jingine la kuvunja moyo ni miziki inayochezwa katika redio zetu siku hizi. Miziki hii ya kizazi cha sasa, haina maadili kamwe.
Badala yake, imejaa maneno yenye kukuza ngono za kiholela, ulevi na ujeuri. Vijana wanaoimba miziki hii hawajali hawabali kuhusu matokeo ya nyimbo hizi, na vituo vyetu vya redio vinawapa motisha ya kuzidi kutunga uchafu, kwa kucheza nyimbo zao mara kwa mara.
Midundo katika miziki hii ya kisasa ni ya kupeleka damu mbio, na hata ina uwezo mkubwa wa kuathiri afya zetu, hasa uwezo wa kusikia vyema.
Itakuwa kazi bure wakati viongozi wetu wanaposhinda wakihamasisha jamii dhidi ya mimba za mapema, ilhali redio inafanya kinyume haswa cha hamasisho hizi.
Fauka ya hayo, taarifa za habari za redio siku hizi zina ufupi mno wa habari. Bila shaka, wasikilizaji hawapati kujua kwa kina kile kinachoendelea ulimwenguni.
Vituo vingi vya redio vimetenga dakika kama tano na kumi pekee kwa taarifa za habari na matukio. Kusema ukweli, dakika hizo ni chache mno, ikizingatiwa mambo yanayotukia katika pembe mbalimbali za taifa na hata ulimwengu.
Isitoshe, mbali na kutangaza habari fupi mno, nyingi ya taarifa hizi huwa ni za kuatua moyo- taarifa za maafa, vifo na maradhi tu.
Jameni, ni ukweli kuwa taifa letu halina mambo mazuri ya kutupa matumaini? Ni lazima tu tuwe tukiambiwa taarifa za uvamizi na majambazi na ufisadi.
Mbona redio zetu zisiangazie matukio mazuri, yanayofanywa na watu wa kawaida?
Vituo vyetu vya redio vinafaa virudi nyuma na kutathmini jinsi mambo yalivyokuwa hapo awali, na vifanye bora kuliko enzi hizo.
Redio yafaa ituhamasishe jinsi ya kujikuza kimaisha, na kiuchumi. Yafaa ituhamasishe na kutuelimisha jinsi ya kuzingatia usafi na afya bora, na jinsi ya kuishi kwa amani na kuzingatia maadili mema.
Kadhalika, redio yafaa ituburudishe, japo kwa njia inayokuza utamaduni wetu pamoja na kushikilia maadili mema. Ipo kazi ya kufanywa.
Redio, kazi kwako!