KINA CHA FIKIRA: Shime Wana-Afrika Mashariki tujimilikishe Kiswahili, lugha ino azizi
Na KEN WALIBORA
KISWAHILI kinaelekea kupata utanuzi mkubwa Uganda.
Nilikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakisikitishwa sana na ati ati ya serikali ya Uganda kukisukuma mbele Kiswahili nchini humo.
Nililalamika katika safu hii na kwengineko kwamba utendaji wa serikali ya Uganda unakwenda kinyume na matamko na sheria rasmi. Mathalan nikilalamika kwamba baada ya kuwapa mafunzo ya ufundishaji wa Kiswahili walimu wengi kabisa wa shule za msingi, serikali ya Uganda ilikuwa imewaacha kwenye mataa.
Walimu hao wa Kiswahili walikuwa miongoni mwa watu waliotamaushwa mno nchini humo kwa kupewa mafunzo na kuhiniwa ajira.
Ni furaha ilioje kubaini kwamba hiyo sasa yamepita! Walimu hao wamekwisha ajiriwa na ufundishaji wa Kiswahili katika shule za msingi kuanza. Hili ni jambo la kutia moyo sana. Endapo watoto wa Uganda watakumbushanishwa na Kiswahili mapema katika safari yao ya elimu na maisha, basi hakitakuwa tena lugha baidia, lugha ya kigeni kama kinavyodhaniwa na vizazi vingine vya Uganda.
Sijui kama niliwahi kusema hapa au bado, ila siku moja alinishauri kijana mmoja sokoni huko Kampala nisiwahi kusema Kiswahili kwa vile nitafikiriwa kuwa mkora. Sitaki kusema kwamba maoni ya kijana yule yanayawakilisha maoni ya Wanauganda wote, ila maoni haya yanaashiria udhaifu wa kimtazamo.
Mtazamo hasi kama huu unaweza tu kung’olewa mizizi endapo watu wa Uganda watakutanishwa na Kiswahili mapema. Wataona mshabaha kati ya lugha zao na Kiswahili na hatimaye kufikia mkataa kwamba Kiswahili ni chao pia na kujimilikisha.
Kiswahili ni lugha ambayo si vigumu kwa mtu yeyote anayetaka kufaidi uhondo wake kujimilikisha. Wengi wetu tumejimilikisha Kiswahili na kupata tija kwa hilo. Labda watu waliojimilikisha Kiswahili zaidi ya wote ni Watanzania.
Si kweli kwamba Kiswahili ndiyo lugha ya asili ya kila Mtanzania. Zamani Watanzania walikuwa na lugha zao mbalimbali (na bado zipo), kama vile Kizaramo cha Mwalimu Nyerere, Kinyamwezi cha Prof Hermas Mwansoko na Kihaya cha Prof Mugyabuso Mulokozi.
Ila sasa baadhi ya Wazaramo, Wanyamwezi na Wahaya hawawezi kabisa kusema lugha zao za awali. Kiswahili ndio wenzo wao wa mawasiliano, utambuzi na ujitambuzi. Kwa mantiki ya safu hii leo, tunaweza kusema kwamba Watanzania wamejimilikisha Kiswahili.
Wamekifanya chao kindakindaki. Kwa kweli kwa hili wamepindukia, ndio maana wataalamu kama Tigiti Sengo wangeweza kusema bila kupepesa macho kwamba Kiswahili ni lugha ya Tanzania yenye asili ya kuko huko.
Pindi Wanauganda watakapojitambua wao ni nani nao wanajimilikisha Kiswahili na kudai kwamba Kiswahili ni lugha ya Uganda yenye asili kuko huko.
Mchakato huu utajirudia kwengineko kama Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, na kuamsha mwamko wa kukienzi na kukipigania Kiswahili. Zingatia kwamba nimeepuka kutaja Kenya. Sababu ni kwamba Kenya nayo hudai usuli wa Kiswahili katika mwambao wake. Tatizo lao ni undumakuwili na kutoukumbatia vilivyo ujimilikishaji.