Utawala wa Moi ulivyojaa giza
Na BENSON MATHEKA
WAKENYA wanapoendelea kuomboleza kifo cha aliyekuwa rais wa pili wa Kenya Daniel Toroitich Arap Moi, baadhi ya walioteswa na serikali yake wamekiri kuwa hawaombolezi mauti yake.
Wanasema kuwa Moi aliwatendea unyama usio kifani na aliaga dunia akiwa hajawaomba msamaha.
Mbunge wa Kangema Muturi Kigano, mwanasiasa Koigi Wamwere na mwanahabari Munene Kamau wameeleza kuwa wangali na machungu kwa mateso waliyopitia chini ya uongozi wa Moi.
Bw Kigano, ambaye alikuwa kati ya waliofungwa jela kufuatia jaribio la mapinduzi la Agosti 1, 1982 ana machungu kuhusu utawala wa Moi akisema waathiriwa hawawezi kusahau maovu aliyowatendea.
“Moi alikuwa dikteta na adui wa watu werevu na wasomi. Wakati wa utawala wake, wengi walikufa na wengine wakapata majeraha ya kudumu,” asema Bw Kigano.
“Moi angeomba msamaha kwa makosa mengi ya kukusudia na kutokusudia aliyofanya wakati wa utawala wake wa miaka 24,” asema Bw Wamwere, kauli ambayo mwanaharakati Wachira Waheire, ambaye pia alifungiwa na kuteswa katika Nyayo House anaunga mkono
“Sitaki kuwa mahali pamoja na Moi huko mbinguni,” Bw Wamwere alisema Jumanne baada ya kifo cha Moi kutangazwa.
Mwanahabari Munene Kamau, ambaye alikamatwa 1987 na kufungiwa Nyayo House ambako aliteswa kwa siku kadhaa akidaiwa kula njama ya kupindua serikali, alisema jana kuwa hajamsamehe Moi kwani hakuwahi kumuomba msamaha.
Mbunge wa Kangema Muturi Kigano, mwanasiasa Koigi wa Wamwere na mwanahabari Munene Kamau ni baadhi ya waliojitokeza wazi kusema hawaombolezi wakikumbuka masaibu waliyotendewa wakati wa utawala wa Moi.
Katika utawala wa Mzee Moi waliotetea haki za binadamu, demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa, uhuru wa kujieleza, uhuru na habari, kutangamana na kukosoa serikali waliwindwa kama simba awindavyo swara katika kila pembe ya nchi.
Baadhi walifungiwa katika seli maalumu za mateso Nyayo House na Nyati House jijini Nairobi walikofanyiwa kila aina ya unyama na maafisa wa usalama.
Kulingana na Bw Kamau waliwekwa vyumba vyenye giza vikiwa vimeloa maji, kupigwa kila mara, kunyimwa chakula miongoni mwa mates mengine.
WALIOLENGWA
Waliolengwa zaidi ni wanasiasa, mawakili, wahadhiri, wanahabari, wanaharakati na viongozi wa vyama vya wanafunzi wa vyuo vikuu.
Wanahistoria wanasema japo alihubiri ‘Umoja, Amani na Upendo’ katika filosofia yake ya ‘Nyayo’, Moi mwenyewe hakuizingatia hasa kwa watu aliohisi walikuwa tisho kwa utawala na maslahi yake.
Miongoni mwa wanasiasa waliojuta kwa kukosoa utawala wake alikuwa Masinde Muliro, ambaye alikuwa mshirika wake katika chama cha Kenya African Democratic Union (Kadu) wakati wa kupigania uhuru.
Bw Muliro alikufa katika hali ya kutatanisha 1992 muda mfupi baada ya kuwasili kutoka Uingereza wakati harakati za kupigania mfumo wa vyama vingi vya kisiasa zilikuwa zimepamba moto.
Wengine walioonja makali ya Moi ni Jaramogi Oginga Odinga, George Anyona, Raila Odinga, Kenneth Matiba, Charles Rubia na Wamwere.
Wanasiasa hao walikamatwa na kutupwa kizuizini kwa muda mrefu bila kufunguliwa mashtaka kwa kupigania demokrasia na mfumo wa kisiasa wa vyama vingi.
Raila pia alihusishwa na jaribio la kupindua serikali la 1982 ambapo alikamatwa na kutupwa kizuizini kwa miaka sita akiteswa. Kwa jumla Raila alikamatwa na kuzuiliwa jela mara tatu chini ya utawala wa Moi.
Mwaka huo wa 1982, baba yake Jaramogi na Anyona walikamatwa kwa kujaribu kuunda chama cha kisiasa kilichofahamika kama Kenya African Socialist Alliance (KASA) kupinga Kanu.
Jaramogi alizuiliwa nyumbani naye Anyona akawekwa kizuizini hadi 1984 alipoachiliwa lakini akakamatwa tena 1990 pamoja na mhadhiri wa Edward Oyugi, Ngotho Kariuki na Njeru Kathangu.
Waliteswa na kuzuiliwa kwa miaka saba kwa madai ya kuchapisha jarida na habari zilizopigwa marufuku wakiwa na “nia ya kupanga kupindua serikali”.
Mnamo 1990, Moi aliagiza Matiba na Rubia wakamatwe kwa kupigania utawala wa vyama vingi vya kisiasa. Wakati huo, Rubia alikuwa waziri katika serikali ya Moi ilhali Matiba alikuwa amejiuzulu uwaziri na kugeuka mwanaharakati.
Akiwa kuzuini, Matiba alishikwa na kiharusi kutokana na mateso aliyopitia, tatizo ambalo lilimsumbua na kuathiri afya na maisha yake hadi alipokufa miaka miwili iliyopita.
WANGARI MATHAI
Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, mhadhiri, mtetezi wa mazingira na mwanasiasa Prof Wangari Mathai naye alikuwa na maisha magumu chini ya utawala wa Moi kwa kupigwa, kuzuiliwa na kuaibishwa.
Bi Maathai aliingia kwenye orodha ya ‘maadui’ wa Moi kwa kutetea Msitu ya Karura jijini Nairobi usinyakuliwe na vibaraka wa Moi walikotaka kujenga nyumba za kuishi pamoja na mabustani ya Uhuru na Jevanjee.
Juhudi zake zilitambuliwa kimataifa alipotunikiwa tuzo ya Nobel mnamo 2004, miaka miwili baada ya Moi kustaafu.
Wanaharakati wengine waliojipata mashakani kwa kukosoa Moi na kutetea demokrasia na haki za binadamu ni wahubiri Askofu Alexander Kipsang Muge wa kanisa la Kiangilikana, ambaye alikufa kwenye ajali ya barabarani 1990, ambayo serikali ya Moi ililaumiwa kuhusika.
Kasisi Timothy Njoya wa kanisa la PCEA naye alipewa kichapo cha mbwa na kuvunjwa mkono na wahuni waliofahamika kama “ Jeshi la Mzee”, ambao walikuwa wametumwa na serikali. Kasisi Njoya alikuwa akiongoza maandamano dhidi ya serikali jijini Nairobi.
Wamwere naye alilazimika kwenda uhamishoni ng’ambo kuhepa masaibu ya utawala wa Moi.
Wahadhiri Ngugi wa Thiong’o, Profesa Anyang’ Nyongo, Maina Kinyatti na Dkt Willy Mutunga ambaye baadaye alihudumu kama Jaji Mkuu wa kwanza katiba ilipobadilishwa 2010 pia walikula pilipili ya utawala wa Moi.
Mawakili waliojipata mashakani kwa kutetea waliokamatwa kwa kupinga Moi ni Gibson Kamau Kuria aliyekamatwa 1987, John Khaminwa, Mohammed Ibrahim, ambaye kwa wakati huu ni Jaji wa Mahakama ya Juu na Kiraitu Murungi ambaye kwa sasa ni gavana wa Meru.
Hali ilikuwa mbaya hivi kwamba mnamo 1987 Kiraitu na Kuria walilazimika kwenda uhamishoni Ulaya.
Paul Muite naye alihangaishwa na polisi na wakati mmoja alikimbilia hifadhi katika ubalozi wa Amerika kuepuka kutiwa mbaroni.
Katika utawala wake, Moi alikadamiza uhuru wa wanahabari na waliochapisha habari zilizokosoa serikali yake walikamatwa, kuteswa na kuzuiliwa korokoroni.
Baadhi ya wanahabari walioteswa wakili Gitobu Imanyara, mwanzilishi wa jarida la Nairobi Law Monthly aliyekamatwa 1987 alipoandika habari za kukashifu serikali.
Wanahabari wengine walioonja ghadhabu za Moi walikuwa Philip Ochieng na marehemu Wahome Mutahi waliokuwa wafanyakazi wa gazeti la Daily Nation.
Wahome alikamatwa wakati mmoja pamoja na ndugu yake Njuguna Mutahi aliyekuwa mfanyakazi wa KBC.
Otieno Makonyango, aliyekuwa mhariri wa gazeti la The Standard alikamatwa baada ya jaribio la mapinduzi la 1982 naye Bedan Mbugua aliyekuwa mhariri wa jarida la The Beyond alikamatwa na kuzuiliwa kwa kuandika habari kuhusu manufaa ya mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.
Moi hakusaza viongozi wa wanafunzi wa vyuo vikuu aliolaumu kwa kutumiwa na wapinzani wake. Miongoni mwa waliojipata kizuizini ni pamoja na Ntai wa Nkuraru, Mwandawiro Mgagha, James Orengo, Kabando wa Kabando na Wafula Buke.
Mwandawiro wakati mmoja alikuwa mbunge wa Taita Taveta, Kabando akachaguliwa Mukurwe-ini, Nkuraru akaishi uhamishoni Uingereza kabla ya kuaga naye Buke aliendeleza shughuli zake za uanaharakati.