• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
AKILIMALI: Matikitimaji yampa kipato eneo hatari kwa wizi wa mifugo

AKILIMALI: Matikitimaji yampa kipato eneo hatari kwa wizi wa mifugo

ONYANGO K’ONYANGO na ELMER MAGEKA

ENEO la Bonde la Kerio halijajulikana kwa amani kwa miaka mingi kutokana na wizi wa mifugo na ukosefu wa usalama kwa jumla ambao umesababisha maisha na mali kupotea.

Ni jambo lililoathiri vibaya maendeleo ya kijamii na kiuchumi eneo hili kame.

Mkoa ambao umetajwa kuwa ‘Kosovo ya Kenya’ kwa sababu ya mashambulio ya kulipiza kisasi unakumbwa na mabadiliko ya kiuchumi kutokana na amani iliyoko baada ya majambazi waliosababisha kukosekana kwa usalama kuadhibiwa vikali na shughuli za pamoja za vyombo vya usalama.

Baada ya kuwa mwathiriwa wa ujambazi, Daniel Suter, mkulima mwenye umri wa miaka 33 kutoka Kabetwa huko Tot, kaunti ndogo ya Marakwet Mashariki aliamua kujiingiza kwenye kilimo cha matikiti maji kujikimu kimaisha.

Baba huyu wa watoto wanne anasema alianza kilimo cha aina hii mnamo 2012 baada ya kushambuliwa na wezi wa mifugo walioiba ng’ombe watano na mbuzi 50 waliokadiriwa kuwa na thamani ya Sh250,000.

“Baada ya kushambuliwa mwaka 2012 na kuibiwa ng’ombe na mbuzi wangu wote, nilikuwa na huzuni sana kwa sababu nimekuwa nikifanya ufugaji tangu nilipomaliza masomo ya Sekondari.

“Ukulima kwangu hukatishia tamaa wezi wa mifugo kwa sababu majambazi hao hawawezi kuchukua kile kilicho shambani,” alielezea Suter.

Alianza kama mkulima mdogo kwa shamba lenye ekari moja na nusu kabla ya kuongeza kiwango kikubwa ambacho alitumia hadi Sh30,000 baada ya miezi mitatu ambayo alisema alitumia kumudu familia yake.

Anaona uwekezaji huo hauna hasara ukilinganisha na ufugaji uliowaweka hatarini kushambuliwa mara kwa mara kwenye ‘bonde la kifo’ kutokana na mauaji yaliyotokana na washambuliaji wenye silaha

Mjasiriamali huyo mchanga anasifia wazo la kuwekeza katika kilimo cha aina hii kama njia mojawapo ya kukabili ukosefu wa usalama ambao umekuwa ndoto katika eneo hilo kwa miaka mingi.

“Uwekezaji wa aina hii kwenye udongo ni salama kidogo kuliko kufuga ng’ombe ambao wanaweza kuibwa mara moja na wezi kama nilivyotendekewa miaka minane iliyopita,” anasema.

Suter anaongezea kuwa licha ya kutokwenda shule zaidi ya Kidato cha Nne, hajutii kwa sababu kilimo cha tikitimaji ni uwekezaji wa faida ambao vijana wengi hawajatambua.

Mkulima Daniel Suter afunika matikitimaji katika shamba lake kijijini Kabetwa, Elgeyo-Marakwet kabla ya kusafirisha Januari 13, 2020. Picha/ Jared Nyataya

Anaendelea kusema kuwa kutoka kwa ardhi yake ya ekari tatu sasa, anapata zaidi ya matunda 3,500 ya tikitimaji ambayo anauza katika kila mkoa kwa Sh150 kila tunda moja huku akijizolea takriban Sh500,000 baada ya miezi miwili hadi mitatu.

“Hivi sasa ninapata matunda 4,000 ya tikitimaji ninayouza katika kituo chetu cha Kabetwa kati ya Sh50-200, na hii ni bora zaidi kuliko kucheza kamari na ng’ombe ambao wanaweza kuibwa wakati wowote,” anaongeza.

Anasema kuwa kiwanda cha kuongezea thamani maembe kilichoanzinshwa hivi karibuni huko Tot, Kaunti ya Elgeyo Marakwet ikiwa pia kinaweza kushughulikia matikitimaji na matunda mengine mbali na maembe, itakuwa vyema zaidi kwa watu wengine wanaolima mmea huu katika mkoa huo.

“Ikiwa kiwanda cha msembe cha Tot kinaweza pia kukubali tikitimaji, mimi na wakulima wengine wa aina hii katika eneo hili linalojulikana kwa ujambazi tutafaidika sana kwa kuongeza thamani ya bidhaa zetu na upatikanaji wa soko tayari sio kama sasa,” aliiambia Akilimali.

Anawasihi vijana kutoka mkoa huo kuwekeza katika “kilimo kikubwa” ili kumaliza ujambazi.

Suter anaongeza kuwa kurejea kwa amani kumefungua fursa kwa waathiriwa wa ujambazi kuwekeza katika shughuli zenye kuleta mapato bora kwa maisha yao.

“Ningependa kuwapa changamoto vijana wenzangu wajiunge na kilimo ili mkoa wetu uweze kufurahia amani kama sehemu zingine za nchi. Ujambazi huu unapaswa kuwa jambo la zamani,” anasema.

Licha ya kupata riziki kutokana na kilimo cha tikitimaji katika eneo lenye ukame, Suter anasema kwamba wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na hali mbaya ya hewa.

“Aina hii ya kilimo huwa ngumu kwa sababu inahitaji mvua ya wastani, kama vile mwaka jana wakati mvua ilikuwa nyingi, ilisababisha mimea kuoza. Hii hufanya kilimo hiki kuwa kigumu sana kwa sababu ya gharama. Wakati mwingine mimi hutumia zaidi ya Sh30,000 kwa dawa za wadudu,” anasimulia.

Uhaba wa maji ni ndoto nyingine kwa wale wanaohusika katika kilimo katika mkoa wa Kerio Valley.

Suter anasema mifereji ambayo ina umbo ya beseni lililotobolewa na kuundwa kutoka kwa mawe na mbao inasimamiwa na koo tofauti.

Mkulima huyo kutoka eneo linalokabiliwa na ujambazi anaiomba serikali iwajengee mabwawa ya maji ili waweze kumwagilia mashamba yao.

You can share this post!

Uhuru azungumza kuhusu BBI Amerika

KIU YA UFANISI: Ukosefu wa karo ulimvunja moyo, akapata...

adminleo