KIU YA UFANISI: Ukosefu wa karo ulimvunja moyo, akapata faraja katika uhudumu bodaboda
Na HASSAN POJJO
HAKUWEZA kuendelea na elimu ya chuo kikuu kutokana na ukosefu wa karo baada ya kukamilisha elimu yake ya shule ya upili katika shule ya Migadini Complex na baadaye akaajiriwa katika duka moja mtaani.
Alinaq Juma Mwakaju, mzaliwa wa kijiji cha Kilibasi eneobunge la Kinango, Kaunti ya Kwale alijikuta akiwa katika njia panda baada ya matamanio yake ya kujiunga na chuo kikuu kugonga mwamba.
Alifanya kazi ya duka kwa kipindi cha mwaka mmoja na alikuwa akilipwa Sh9,000 kwa mwezi pesa ambazo alijiwekea ili aweze kubadilisha maisha yake ya baadaye.
Alifanikiwa kukusanya Sh108,000 katika kipindi cha mwaka mmoja na akajinunulia pikipiki yake na kuanza kazi ya bodaboda.
Anasema kuajiriwa katika kazi ya duka kulimsaidia kuchanga pesa na kujinunulia pikipiki ambayo kwa sasa inampatia kipato kizuri kila siku.
Alinaq anasema kwamba ni vyema mwanadamu kuwa na malengo kila mara anapokuwa katika dunia ili Mungu anapofungua njia aweze kutimiza akitakacho moyoni mwake.
“Nilikuwa nimekata tamaa katika maisha baada ya kuona kwamba wazazi wameshindwa kupata pesa za kuendelea na elimu yangu katika chuo kikuu, lakini nilijipa moyo na nitaanza kutafuta ajira ili niweze kutekeleza yaliyokuwa ndani ya moyo wangu,” asema Alinaq.
Mwanzoni katika biashara ya bodaboda maisha yalikuwa magumu lakini baada ya muda alianza kuona faida. Aidha, anasema kwamba wakati kazi ni mbaya hupata kiasi cha Sh1,500 na 2,000 na kama ni nzuri hupata kati ya 2,500 hadi 3,000 kwa siku na kutengeza kati ya Sh60,000 na 90,000 kwa mwezi.
Anawataka vijana pale wanapopata fursa wafanye kozi zingine ili kujiongezea ujuzi na kufungua nafasi zingine za kazi.
Ni kijana ambaye amesomea masuala ya compyuta hivyo anawasihi wanabodaboda kufunguka macho na kuipenda kazi yao na kutoruhusu watu kuidharau.
Alinaq anasema kwa muda mfupi aliofanya kazi ya pikipiki ameweza kupata mafanikio na anatarajia kununua tuktuk ili aweze kujiboresha zaidi kibiashara na kimaisha.
“Ni jambo la kusikitisha kuona baadhi ya watu ama vijana wanaharibu sifa na kazi ya bodaboda kwa kujihusisha na visa vya kihalifu, hili ni jambo ambalo halifai na ninaomba vyombo vya usalama viweze kutukagua kila mara na atakayepatikana na tabia kama hizo achukuliwe hatua za kisheria,” anasema Alinaq.
Anasema kwamba katika kazi hiyo wanapitia changamoto nyingi ambazo wanakumbana nazo wanapokuwa katika mazingira yao ya kazi.
Ametaja kwamba ni lazima waendesha bodaboda wote waweze kuheshimu na kufuata kanuni na sheria za barabarani na muongozo wa maafisa wa trafiki ili kuepuka usumbufu usiokuwa wa lazima kwa maafisa hao.
Amewataka vijana kuacha tabia za kuchagua kazi ikizingatiwa kwamba hali ya uchumi wa nchi inategemea uwajibikaji wa vijana ambao ndiyo nguvu kazi na rasilimali.