• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 8:12 PM
BIASHARA MASHINANI: Anakuza pilipili kichaa Salgaa na asema zinamsukuma vyema

BIASHARA MASHINANI: Anakuza pilipili kichaa Salgaa na asema zinamsukuma vyema

Na SAMUEL BAYA

UMBALI wa kilomita tatu kabla ya kukifikia kituo cha biashara cha Salgaa, eneobunge la Rongai, Kaunti ya Nakuru, utaona wakulima wengi wakiendeleza aina mbalimbali za ukulima.

Katika mashamba hayo ambayo wakulima hukodisha kwa ajili ya kilimo, utagundua kwamba kuna aina mbalimbali za ukulima unaoendelezwa hapa, almradi tu kila mtu anajichumia riziki na kuzisaidia familia zao.

Tukiwa hapa, ndipo tunavutiwa na mkulima mmoja ambaye amekuwa akiendeleza kilimo cha pilipili kali almaarufu mtaani kama ‘pilipili kichaa’.

Francis Muraya amekuwa akilima mboga katika kipande cha ekari mbili za ardhi. Zaidi anashughulika katika ukulima wa sukumawiki, kabeji, pilipili hoho, pilipili kali, spinach na mboga aina nyingine kama maharagwe na kunde.

“Nilianza ukulima miaka 15 iliyopita nikiwa katika eneo la Munyeki, Nakuru. Nilivutiwa na jinsi majirani zangu walivyojitahidi katika kilimo na mimi nikafurahia na kuamua kuingilia shughuli hiyo,” akasema Muraya.

Kwa sababu hakuwa na kazi yoyote wakati huo, Muraya aliwaza na kutambua kuwa ni kupitia kilimo ndipo alipokuwa na fursa ya kunawiri kimaisha. Hakurudi nyuma tena hadi leo hii.

“Kwa sababu sikuwa na kazi, niliamua niingilie ukulima tu nikijaribu kujipa shughuli mwaka wa 2002. Sikuwahi kupata mafunzo yoyote ya ukulima lakini kwa sababu niliona wenzangu wakiendelea na kilimo, niliwaiga na leo hii ninashukuru kilimo kimegeuka uti wa mgongo katika maisha yangu,” akasema.

Aliambia ukumbi huu kwamba alipoanzia katika eneo la Munyeki, mwanzoni kulikuwa na changamoto kwa sababu hakukuwa na shamba kubwa kama ilivyo katika eneo la Rongai.

“Hali ilikuwa ngumu kwa sababu nikiwa Munyeki, nilianza na nusu ekari lakini sikutaka kubakia huko. Nilikuja katika eneo hili la Rongai na kukodi ekari sita ambazo ninazilima mpaka sasa,” akasema.

Baba huyo wa watoto wanne alisema kwamba baada ya kuhamia eneo la Rongai na kupata shamba hili kubwa, akaamua kuchanganya ukulima wa mboga bila kusita.

Kwa mkulima ambaye alianza tu kwa kilimo cha kubahatisha bila msingi thabiti, Muraya amepaa na kujitokeza kuwa mmoja wa wakulima maarufu wa kaunti ya Nakuru kutokana na uwezo wake wa kuzalisha chakula kwa wingi.

“Ukulima una faida kubwa na nimejionea mwenyewe kwa macho yangu mawili. Sikuanza na chochote lakini leo hii, nimefaulu kununua ploti, nimenunua ng’ombe, ninalipa karo na kila kitu kinaelekea vile vilivyotamani,” akasema.

Kama biashara yoyote ile, kilimo hakikosi changamoto na Muraya ameshuhudia yote hayo kwa miaka hiyo ambayo amekuwa katika biashara hii.

“Kuanzia Januri hadi mwezi wa Aprili, biashara huwa nzuri sana. Soko la mboga huwa juu na hata kwa siku unaweza kuuza hata Sh200,000,” akasema.

Hata hivyo, wakati ambapo hakuna soko, biashara huteremka sana na Muraya huuza tu kama Sh3,000 kwa siku.

“Kuanzia mwezi wa tano hadi mwezi wa Agosti huwa hakuna soko wakati huo na hapo mapato huteremka na kuwa kidogo kabisa,” akasema.

Wakati wa kiangazi, yeye hupata wateja kutoka maeneo mbalimbali ya kaunti ya Nakuru na hata katika kaunti jirani ya Baringo.

“Wakati kuna kiangazi na mboga ziko na uhitahji, wengi hufurika hapa kununua mboga kutoka maeneo mbalimbali nchini. Wengine wanatoka katika maeneo Eldoret, Kisumu, Kisii, Mogotio.

Baadhi ya zao la pilipili zikiwa zimechunwa katika shamba la Bw Muraya karibu na kituo cha biashara cha Salgaa kwenye barabara kuu itokayo Nakuru kuelekea Eldoret. Picha/ Samuel Baya

Hata hivyo wengi wanatoka mjini Nakuru kwa sababu wako karibu na mimi,” akasema.

Kwa sasa kilo moja alisema inauzwa kwa Sh50 lakini awali, bei ya pilipili huwa iko juu.

“Wakati mwingine kilo moja huuzwa hata kwa Sh100 lakini mara nyingi hili hutegemea msimu. Wakati ambapo pilipili zinakuwa nyingi, bei yake hushuka lakini zinapoadimika basi bei hupanda na kuwa juu,” akasema.

Katika shamba hilo, Muraya huwa anagawanya mara tatu kupanda aina mbalimbali za mboga kama mviringo.

“Ninagawanya shamba hili kwa mara tatu na kupanda mboga aina mbalimbali. Hilo linanisaidia katika kuongeza mapato yangu,” akasema.

Hajasomea kilimo lakini alisema kuwa motisha wake ilikuwa ni kuingilia kilimo tangu akiwa mdogo na hajutii kwa sasa.

“Sijaenda katika semina yoyote ya ukulima ila tumekuwa tukipata mafunzo kutoka kwa kampuni za kuuza madawa. Hutufikia kila msimu na kutufundisha kila aina ya madawa ambayo tunafaa kuweka kwa mimea yetu,” akasema.

Katika eneo la Salgaa, yeye pamoja na wakulima wengine huwa wananunua mabomba ya kupigia maji.

“Kununua hizi paipu ni Sh2,000 kwa futi 20 na jenerata nimenunua kwa Sh50,000 na tunakodisha shamba kwa Sh10,000 kwa mwaka. Hii ni changamoto kubwa kwa wakulima.

“Tunatumia jenereta na paipu hizi kupiga maji kutoka kwa mto ulioko karibu hadi katika mashamba yetu,” akasema.

Kwa mkulima anayeanza, hali hii huwa ngumu ila kwa Muraya, lazima ujikaze ukitaka kufanikiwa katika maisha.

  • Tags

You can share this post!

UBUNIFU WA KIUCHUMI: Anaendeleza kilimo cha kitunguu maji...

BIDII YA NYUKI: Alikosa kazi ya hoteli, akaamua kuchuuza...

adminleo