• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
BIDII YA NYUKI: Alikosa kazi ya hoteli, akaamua kuchuuza chipsi

BIDII YA NYUKI: Alikosa kazi ya hoteli, akaamua kuchuuza chipsi

Na GRACE KARANJA

BAADA ya kukamilisha elimu ya shule ya upili hakufanikiwa kujiunga na chuo kikuu kwa sababu ya ukosefu wa karo.

Alifanya vibarua hapa na pale sio kuwaoshea nguo baadhi, kulima katika mashamba na pia kwa wakati mwingine kuajiriwa kama kijakazi mjini Nairobi. Kwa wengi aliowafanyia kazi waliridhishwa na utendakazi wake huku wengi wakimshauri kufanya kozi ya upishi kwani kipawa chake kilijidhihirisha.

“Hata nikiwa nyumbani wazazi walipenda nikipika walisema chakula changu kilivutia ila sikugundua nilikuwa na kipawa cha upishi. Baada ya shule ya upili nifanya vibarua vingi lakini kilichojitokeza ni wengi kusifia jinsi nilivyopika. Wengine hata waliniita tu niwapikie wanilipe na niende nyumbani na ikawa hivyo nikajua kwamba talanta yangu ambayo ingenifaa maishani ilikuwa ni kupika,” anasema.

Hata hivyo, alipoolewa maisha yalimwendea mrama. Ukosefu wa vibarua huko mashinani ukawa mtindo. Lakini kwa bahati ya Mungu wazazi wakampa habari za matumaini ya kuanza maisha tena. “Habari za kurudi shule kusoma kozi ya upishi ilinipa uhai tena kutokana na yale niliyopitia. Hata hivyo, familia yangu iliporomoka kufuatia kurejea kwangu chuoni. Sikujali, nilijua ninajenga maisha yangu ya usoni,” anaeleza kwa masikitiko Alice.

Licha ya kukamilisha masomo yake katika chuo cha taaluma ya Mapishi cha Walton Hospitality College kilichoko mjini Embu na stashahada ya taaluma ya masuala ya upishi na huduma za mikahawa mnamo mwaka wa 2018, jitihada zake za kusaka kibarua hazikufaulu kwa zaidi ya mwaka mmoja.

“Nilifikiri nikimaliza chuo nitapata kazi lakini hakuna, si rahisi katika enzi hii kupata kibarua cha ile kazi umefuzu labda kwa aliye na bahati. Cha muhimu nikutokufa moyo na kuangalia vile unaweza kutumia masomo yako kujiajiri mwenyewe hasa katika fani hii ya mapishi na huduma za mikahawa,” anasema Alice Wambui mzaliwa wa kijiji cha Ngatho, Kaunti ya Murang’a.

Anasema masomo kwa mtoto wa kike yanafaa kutiliwa maanani na kueleza kwamba sasa ana maisha tofauti na ya awali wakati hakuwa amesoma. Anahofia watoto wa kike ambao hawajapata nafasi ya kuendelea na masomo kwani anaeleza machungu aliyopitia na hadi wakati alitengwa.

Kulingana na Alice, bidii katika kazi yoyote ile ni nguzo ya mafanikio katika maisha. Licha ya kusaka kazi na kukosa baada ya kukamilisha masomo aliamua kwenda katika kibanda cha mwanabiashara mmoja kwa jina Stephen kilichoko Makongeni, Thika ndani ya kituo kipya cha mabasi.

Stephen hupika chipsi na kuuza katika kituo hicho cha mabasi. Hata hivyo, alimwahidi kwamba angempa kazi endapo atauza kifungu kimoja cha Sh50 na hapo ampe Sh10. Alice aliamua kufanya hivyo na sasa anajivunia kuwa na kazi licha ya kuwa kuzunguka akiwasaka wateja ni kibarua kigumu.

“Mimi huchukua vifungu vya chipsi mkahawani, nazunguka katika kituo hiki cha Makongeni na maeneo yaliyo karibu, na sikosi chakula na matumizi yangu na watoto wangu. Mwanzo niliona kama Sh10 ni chache lakini nilivyoendelea kujifunza kuzungumza na wateja nikaona ni kazi inayoweza kumwajiri mtu,” anaeleza.

Kwa siku moja wakati kuna shughuli nyingi hasa wikendi na siku ambazo wanafunzi wako likizoni anaweza kupata kati ya Sh500 au 600 pesa ambazo anasema zinamtosheleza kimaisha. Pia siku zingine huwa ziko chini anaweza kupata Sh100 lakini anasema hajawahi kukosa chochote.

You can share this post!

BIASHARA MASHINANI: Anakuza pilipili kichaa Salgaa na asema...

Utawala wa Moi ulivyojaa giza

adminleo