• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 4:10 PM
Shujaa yakutanishwa na miamba Afrika Kusini katika duru ya Los Angeles

Shujaa yakutanishwa na miamba Afrika Kusini katika duru ya Los Angeles

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya almaarufu Shujaa imetiwa katika kundi gumu la duru ya tano ya Raga za Dunia itakayofanyika mjini Los Angeles nchini Marekani mnamo Februari 29 hadi Machi 1.

Shujaa, ambayo ilisikitisha katika duru ya nne ilipovuta mkia mjini Sydney nchini Australia mnamo Februari 2, itapepetana na washindi wa duru ya ufunguzi Afrika Kusini pamoja na Jamhuri ya Ireland na Canada katika mechi za Kundi B.

Vijana wa Paul Feeney, ambao waliwasili nyumbani kutoka Australia mnamo Jumanne, wamewahi kufika nusu-fainali nchini Marekani mara mbili; mwaka 2008 na 2010.

Hata hivyo, ziara yake ya mwisho nchini Marekani ilikuwa mbovu ilipokamilisha kampeni yake katika nafasi ya 11 kwa alama tano.

Shujaa itaanza kampeni yake dhidi ya Afrika Kusini mnamo Februari 29 saa nne na dakika 35 asubuhi, kisha ilimane na Ireland mnamo Machi 1 saa saba na dakika 31 asubuhi kabla ya kumaliza mechi za makundi dhidi ya Canada saa nne baadaye.

Duru ya Marekani inarejea mjini Los Angeles kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006. Pia, mfumo wa kawaida wa timu mbili bora kutoka kila kundi kuingia robo-fainali utarejelewa baada ya kuondolewa katika duru mbili zilizopita mjini Hamilton nchini New Zealand na Sydney, Australia.

Shujaa inashikilia nafasi ya 11 kwa alama 26. Afrika Kusini ni ya pili kwa alama 67 nazo Ireland na Canada zimezoa alama 33 kila mmoja katika nafasi za tisa na 10, mtawalia.

Msimu huu, Shujaa ilipigwa 17-12 na Afrika Kusini katika mechi za makundi mjini Dubai mnamo Desemba 5, 2019, ikalemewa 17-5 mjini Cape Town nchini Afrika Kusini katika mechi ya robo-fainali mnamo Desemba 15, 2019, na kuduwaza miamba hao 36-14 katika mechi za makundi za Hamilton mnamo Januari 26, 2020.

  • Tags

You can share this post!

Watoa mwito BBI ihusishe maoni ya vyama kadhaa vya kisiasa

RIZIKI: Utingo aliyejipanga akawekeza kwenye biashara ya...

adminleo