Sura nne za Nyayo
Na WANDERI KAMAU
RAIS wa pili wa Kenya, hayati Daniel Moi ametajwa kuvaa sura nne tofauti katika kipindi cha miaka 24 aliyotawala Kenya hadi alipoaga dunia Jumanne wiki hii.
Kulingana na wachanganuzi wa siasa, sura ya kwanza ya Mzee Moi ilidhihirika kati ya 1979 hadi 1981, 1982 mpaka 1991, 1992 hadi 2002 na 2003 hadi 2020.
Wanasema kwamba ubadilishaji huo wa sura ulitokana na matukio yaliyomlazimu kutumia mitindo tofauti kulingana na nyakati na changamoto zilizomkumba.
Kati ya 1979 na 1981, Mzee Moi anatajwa kuwa kiongozi mwema ambaye alikumbatiwa na Wakenya kwa mikono miwili kila pembe ya nchi.
Ni wakati huu ambapo Mzee Moi aliahidi kuendeleza “nyayo” za Mzee Jomo Kenyatta kupitia Falsafa ya Nyayo, ambayo ilikuwa na kauli mbiu ya “Amani, Upendo na Umoja”.
Kulingana na Prof Peter Kagwanja, katika kipindi hicho Mzee Moi aliwaamini wanasiasa wengi ambao walikuwa washirika wa karibu wa Mzee Kenyatta, kwani hakukuwa na dalili zozote za chuki dhidi yake.
“Huu ndio wakati Mzee Moi alidhihirisha sura yake bora zaidi kama mwanasiasa. Hali ya uchumi iliimarika sana kutokana na uthabiti wa kisiasa uliokuwepo. Kila Mkenya alihisi kulikuwa na mwanzo mpya,” asema Prof Kagwanja.
Hata hivyo, kipindi hicho cha utulivu kilifika kikomo Agosti 1, 1982 kufuatia jaribio la baadhi ya wanajeshi kupindua serikali yake.
Ni kuanzia hapo ambapo Mzee Moi alibadilisha sura na kugeuka dikteta aliyeshuku yeyote aliyekosoa uongozi wake ama kudhaniwa kuwa na nia ya kuchochea upinzani dhidi yake.
Ni katika kipindi hiki ambapo Mzee Moi aliwatesa wanasiasa, wanahabari, wahadhiri, wanaharakati na mawakili wengi waliokuwa wakihimiza utawala wa kidemokrasia na haki za Wakenya.
Mzee Moi alitumia maafisa wa usalama kukabili makundi ya kisiasa yaliyochipuka kuukosoa uongozi wake yaliyoongozwa na wasomi na wanaharakati wa kisiasa kama Prof Ngugi wa Thiong’o, Maina wa Kinyatti, Katama Mkangi kati ya wengine.
Wakati shinikizo za kuitisha vyama vingi vya kisiasa zilipozidi, Mzee Moi alilazimika kusalimu amri na kuruhusu mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.
Hatua hiyo ilimlazimu kubadilisha sura yake iliyoshuhudiwa kati ya 1992 na 2002.
Wadadisi wanasema kuwa kwa kukubali kushiriki uchaguzi wa 1992 na uwepo wa vyama vya kisiasa kama Ford-Kenya, Ford-Asili, Democratic Party, Moi alikoma kuwakabili wapinzani na wakosoaji wake na kuonekana kukumbatia demokrasia kwa kiwango fulani.
“Kwa kukubali uwepo wa vyama vingi, Moi aliiepushia Kenya hatari ya kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe ama mapinduzi ya kijeshi,” asema Bw Javas Bigambo.
Sura mpya ya Moi aliyekumbatia demokrasia ilidhihirika 2002 alipong’atuka uongozini baada ya Kanu kushindwa na muungano wa Narc na kukabidhi madaraka kwa amani kwa Mwai Kibaki.
Sura ya nne ya Mzee Moi ilikuwa kati ya 2003 hadi alipofariki, ambapo anatajwa kuwa kiongozi aliyeendesha maisha yake kwa utulivu na uungwana mkubwa.
Wadadisi wanasema kuwa ni kutokana na utulivu huo, ambapo viongozi mbalimbali wa kisiasa walikuwa wakizuru kwake kuomba ushauri na miongozo ya kisiasa.
“Katika kustaafu kwake, tunaona mwanasiasa ambaye aliendesha maisha yake kwa uungwana mkubwa, kiasi cha kuombwa ushauri na wanasiasa wengine hata waliokuwa wapinzani wake alipokuwa madarakani. Hili pia lilidhihirisha ubora wake kama kiongozi aliyeheshimika hadi alipofariki,” asema Bw Bigambo.