KAULI YA MATUNDURA: Msukumo mpya wa mahakama ya EAC kupigania sera ya lugha Kenya

Na BITUNGI MATUNDURA

Hivi majuzi, mwalimu wangu – Prof Inyani Kenneth Simala, ambaye ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika ya Mashariki alituma ujumbe kwenye ‘Ukumbi wa Kiswahili’ kuhusu amri ya Mahakama ya Afrika ya Afrika Mashariki kutupilia mbali kesi ya kupinga Muungano wa Tanzania, Zanzibar.

Kamisheni hii ni asasi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo imetwikwa jukumu la kushirikisha na kukuza matumizi ya Kiswahili katika ukanda huu kama lingua franca. Stakabadhi aliyotutumia Prof Simala ilikuwa arifa kwa wanahabari iliyotolewa na mahakama hiyo mnamo Machi, 8,2018.

Kesi hiyo iliwasilishwa na Bw Rashid SalumAdiy– kupinga uhalali wa Muungano huo. Katika kesi hiyo, Bw Rashid, pamoja na raia 39,999 vilevile waliitaka mahakama hiyo isikize kesi hiyo kule Zanzibar – kumaanisha kwamba ilihitajika ihamishe makao yake makuu kutoka Arusha hadi Zanzibar.

Aidha, mahakama hiyo ilipinga ombi la Bw Rashid kutaka atumie lugha ya Kiswahili katika Mahakama hiyo. Ombi hili pia lilikataliwa kwa msingi kwamba Ibara 46 ya Mkataba ulioidhinisha kubuniwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua Kiingereza kuwa ndiyo lugha rasmi ya Jumuiya hiyo.

Hatua hii iliibua ukweli usiofahamika kwamba, ingawa lugha ya Kiswahili inakubalika bayana kuwa ya taifa nchini Tanzania, Katiba ya nchi hiyo bado haijafumbata urasmi huo. Stakabadhi aliyoituma Prof Simala iliibua mdahalo katika ‘Ukumbi wa Kiswahili’ kuhusu hali ya sera ya lugha nchini Kenya.

‘Ukumbi wa Kiswahili’ ni kundi la WhatsApp linalowaleta pamoja wanataaluma wa Kiswahili – wengi wao kutoka Kenya.

Prof Mwenda Mukuthuria wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara ‘alishtuka’ kwa msingi kwamba, hakutegemea kipengee kama hicho – cha kuharamisha matumizi ya Kiswahili katika mahakama ya Jumuiya kuwepo kwenye Katiba.

Kwa mujibu wa mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAM), lugha rasmi ni Kiingereza; Kiswahili kikitwikwa jukumu la matumizi mapana. Prof Kimani Njogu, ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kupigania masuala ya sera ya lugha Kenya alisema kwamba, bila kubadilishwa kwa Ibara ya 46 ya Mkataba huo kisheria,Kiswahili kitaendelea kuwekwa pembezoni katika matumizi yake mahakamani.

Alikiri kwamba ipo kazi kubwa ya uraghbishaji inayohitajika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanikisha hali hiyo. Ila mtaalamu huyu anaonya kwamba mikakati kabambe inahitajika katika suala hili. Mikakati hii inapaswa kuwekwa na kutekelezwa na akina nani?

Kupitia kwa asasi zipi? Kwa kufuata utaratibu upi kuhakikisha kwamba mambo hayakwami au hayachukui miaka na mikaka kukamilika?

Nilimwomba Prof Njogu atueleze hatua ambazo yeye na wanataaluma wengine walizopiga katika mambo mawili. Kwanza, Rasimu ya Sera ya Lugha ya Kenya 2013 (Languages of Kenya Policy Framework 2013). Pili, Mswada wa Sheria Kuhusu Lugha 2013 (Languages of Kenya Bill 2013).

Prof Ngogu alisema, ingawa kazi kubwa imekwisha kufanywa katika kuandaa rasimu ya Sera na Mswada kuhusu Sheria hiyo, ni hatua chache mno zilizokwisha kupigwa katika kupulizia vipengee hivi cheche za pumzi.

Hali hii chambacho Njogu inasikitisha sana – ingawa Katiba ya Kenya inatambua Kiswahili kuwa rasmi sambamba na Kiingeeza. Rasimu ya Sera ya Lugha ya Kenya na Mswada wa Sheria Kuhusu Lugha awali iliandaliwa na Wizara ya Michezo, Utamaduni na Sanaa.

Hatimaye, ilihamishiwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia. Wakereketwa wa lugha waliamini kwamba hatua ya kuhamisha mchakato huo ingechapusha kipengee cha kuikita kwenye sheria.

Hili halikutimia. Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikwisha kubuniwa na kuanza utendajikazi. Mpaka sasa, Kenya haijabuni Baraza la Kiswahili la Taifa.

 

 

Habari zinazohusiana na hii