• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
ANA KWA ANA: Mbona kaamua kuvaa uhusika ‘M-Pesa Lady’?

ANA KWA ANA: Mbona kaamua kuvaa uhusika ‘M-Pesa Lady’?

Na THOMAS MATIKO

GEORGE Kagwe ni miongoni mwa Vloggers wa vichekesho wanaofanya vizuri nchini Kenya.

Unapoamua kuwaorodhesha hao bora wa vichekesho nchini, hutakosa kuwataja watu kama vile Njugush, Terrence Creative, Eric Omondi, Kagwe miongoni mwa wengine.

Kagwe alipata umaarufu sana baada ya kusambaa video yake akiwachongoa wahudumu mademu wa Mpesa. Toka wakati huo, ameendelea kupiga shughuli hizi na kwa sasa ni miongoni mwa ‘Influencers’ wakubwa wanaoangukia dili za biashara matangazo kila kukicha kutoka kwa kampuni mbalimbali. Nilikutana naye na kupiga stori.

Tofauti na kwenye video zako, unapovua uhusika unaonekana mtu mpole, uliyetulia sana. Hivi George Kagwe ni mtu wa sampuli gani?

Kagwe: Hahaha watu wengi wanapokutana na mimi hushangazwa sana na utulivu niliona nao na hii ni kwa sababu wameshanizoea nikiwa kwenye uhusika kwenye zile video zangu. Wanasahau kwamba ule ni uhusika tu na lazima niwe vile. Ni tofauti na ninapokuwa mimi.

Ukiachia mbali sifa hizo, mimi ni mume na baba wa binti mmoja. Nilijaliwa watatu lakini kwa bahati mbaya wawili wakafariki.

Pole sana.

Kagwe: Asante kaka nishapoa, ndivyo maisha yalivyo.

Safari hii ya kuwa Vlogger ilianza vipi na wakati upi?

Kagwe: Nilianza 2014 ikiwa ni miaka mitatu baada ya kifo cha babangu aliyefariki kutokana na ugonjwa wa saratani. Kabla ya hapo nilikuwa nimejaribu masuala ya uigizaji lakini hayakuniendea poa.

Kwa hiyo uigizaji ulipokwama ndipo ukageuka na kuwa Vlogger?

Kagwe: Kipindi nikijihusisha na uigizaji, nilikuwa nafanya kazi pia kama mtaalamu wa IT, ila mapenzi yangu makubwa zaidi yakawa kwenye uigizaji. Nilikuwa nimeshiriki kwenye usaili wa uhusika mbalimbali lakini kila mara nilipofanikiwa, ilipofikia siku ya kuanza kushuti, nikawa napokonywa ule uhusika na unapewa mtu mwingine. Hili lilinitokea mara kadhaa 2012, moja kati ya vipindi vigumu katika maisha yangu. Baadaye nilifanikiwa kupata kazi kwenye kampuni iliyojihusisha na masuala ya uandaaji tamasha. Ni pale nilikutana na bosi wa kampuni hiyo aliyenipa maarifa ya kuwa Vlogger. 2014 rafiki yangu mmoja aliyekuwa akifanya kazi na kampuni ya Google akaanza kunisihi sana nianzishe chaneli yangu YouTube akinihakikisha kwamba nitatengeneza hela kupitia video za vichekesho kwa sababu ni mtu aliyekuwa akinifahamu na hapo ndipo nikajitosa kimasomaso.

Ile shuka ya kimaasai na kile kicheko, sifa ambazo sasa zinahusishwa na uhusika wako, zilikujaje?

Kagwe: Nilipoanza shughuli hizi, mtu wa kwanza niliyewazia kumwigiza ni hao wahudumu wa kike wa M-Pesa. Kuna baadhi yao hakika huudhi kwa namna ambavyo hutoa huduma. Wana usumbufu na dharau fulani.

Hivyo nilifanya utafiti na kugundua wengi wao walikuwa wanapendelea ile shuka ya Maasai kwa sababu ya kuwa mara nyingi wapo sehemu ya wazi wakiendelea na biashara yao. Kuhusu kicheko, ilitokea wakati mmoja nikiwa Mcee ambapo niliwaona mabinti kama vile wakisengenya, nikaamua kuwatania kwa kucheka jinsi ambavyo mademu wengu hucheka. Nilipoangua kile kicheko, kila mmoja pale akaisha kinoma. Hapo ndipo nikaona bora niiongeze kwenye uhusika.

Kuna mtu atakuwa anajiuliza hivi kuwa Vlogger kunalipa kweli?

Kagwe: Kunalipa ilmuradi unaandaa mada itakayopendwa na inayohusiana na maisha ya watu wa kawaida. Kwa mfano pale YouTube unapokuwa na video zinazovutia utazamaji mkubwa, basi kutakuwepo na matangazo ya kibiashara ambayo mwisho wa siku utalipwa asilimia 55% ya kipato kile. Kando na hilo, kuwa Vlogger kunaweza kukusaidia ukawa ‘Influencer’ na ukaishia kupiga dili zaidi za matangazo ya kibiashara na kampuni mbalimbali. Cha msingi ni kujipanga.

Unaweza kumshauri mtu awache kazi ili awe Vlogger?

Kagwe: Mwanzo kabisa iwe hali hii imetokana na msukumo wa kutaka kufanya hili sio kwa sababu ana tamaa ya kuunda hela.

Pili lazima ajipange sababu kuwa Vlogger unahitaji mkwanja wa maana. Kingine lazima awe mvumilivu sababu huchukua muda. Kwa kuzingatia haya, anaweza akafanya maamuzi yake.

Labda tugeuze mada kidogo, maisha yako ya ndoa vipi?

Kagwe: Namshukuru Mungu tupo tunaingia mwaka wa saba sasa ingawaje nimemfahamu mke wake Karimi Kagwe kwa miaka 11 sasa.

Tunapendana, tunagombana. Tunaishi kwa kuvumiliana, tunaelewana, hatufichani na ndiyo sababu tunazidi kusonga tu.

Umewahi kuchongolewa kutokana na namna ulivyokula ukashiba?

Kagwe: Ni jambo la kawaida sana na wala huwa halinishtui. Najiamini na najipenda nilivyo; hivyo mwenye tatizo na mwili wangu sio mimi ni mahasidi.

You can share this post!

KIKOLEZO: EMB kama ‘ndrama’, kunani?

DOMO KAYA: Kumbe ni kutuchocha tu!

adminleo