Makala

KAULI YA WALIBORA: Shauku kubwa ya Sheikh Abeid Karume kuiandika katiba katika Kiswahili sanifu

April 12th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na PROF KEN WALIBORA

MJINI Arusha kuna uwanja wa michezo uitwao Sheikh Abeid Aman Karume. Hapo ndipo nilipowahi kuona kwa mara ya kwanza mtanange wa watani wa jadi nchini Tanzania Yanga na Simba.

Ulikuwa mwaka 2000 nafikiri. Baadaye hivi karibuni nilihutubu uwanjani humo kusisitiza umuhimu wa mshikamano baina ya watu wa Afrika Mashariki.

Ila tangu mwaka 2000 nimekuwa nikiwazia yule mtu ambaye uwanja ulipewa jina lake: Sheikh Abeid Aman Karume. Alikuwa nani na kwa nini uwanja huo ulipewa jina lake?

Kwa nini uwanja hupewa jina fulani. Huku kwetu ukiona jina la barabara, skuli, uwanja wa ndege au wa michezo, ujue aghalabu umepewa jina la mwanasiasa. Au umepewa jina lisilomwenzi yoyote.

Kwa nini kwa mfano, uwanja wa City Stadium, haukupewa jina la sogora wa kandanda nchini Kenya mzee Joe Kadenge? Au kwa nini haukupewa jina la beki maarufu wa enzi za kale, Jonathan Niva, ambaye nilisoma na binti yake Umaasaini nilipokuwa Mmaasai wa kupanga.

Mbona uwanja wa michezo Mombasa ukaitwa uwanja wa Manispaa Mombasa badala ya kupewa jina la mlinda lango hodari wa timu ya taifa Mahamoud Abbas au kiungo matata Ali Breik?

Kila nionapo jina la uwanja, barabara, jengo, shule, au chochote kile kinachopewa jina kwa heshima ya mtu fulani, siishi kujiuliza maswali mengi. Kuhusu uwanja wa mjini Arusha, Sheikh Abeid Aman Karume hakuwa mtu vivi hivi tu kama mimi.

Alikuwa makamu wa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na rais wa kwanza ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.

Sijui siasa vizuri lakini unaweza kuona kwamba mzawa huyu wa Zanzibar kapewa heshima ya uwanja wa Tanganyika kuitwa kwa jina lake labda kama mkakati wa kuimarisha muungano wa Tanzania. Sijui, nakisikia tu.

Hayati Karume aliuawa kwa kupigwa risasi mnamo 7, Aprili 1972. Anakumbukwa kwa mengi, ila moja muhimu kwangu ni kwamba alisisitiza kwamba Kiswahili kutumike katika mikataba na katiba ili wananchi wengi wapate kuelewa yaliyomo.

Kama katiba na mikataba ikiandikwa kwa Kiingereza tu, wananchi walio wengi wanakuwa mbumbumbu wa yaliyomo ingawa yanawahusu moja kwa moja.

Miaka hamsini baada ya uhuru katiba za nchi nyingi za Afrika Mashariki bado zimeandikwa katika Kiingereza au lugha nyinginezo za kikoloni.

Nchini Kenya hali ni mbaya zaidi kwa vile ingawa katiba yenyewe inasema Kiswahili ni lugha ya taifa na lugha rasmi na kwamba sharti katiba itafsiriwe rasmi, hili halijawahi kufanyika.

Je, Tanzania ndiko kwema? Hata kidogo. Katiba ya Tanzania hata haihitaji lugha ya Kiswahili. Kiswahili kinazungumzwa Tanzania tu kwa sababu kimo mioyoni mwa Watanzania; katika katiba hakimo.

Hilo linamaanisha kwamba miaka zaidi ya hamsini baada ya kifo uhuru, maneno ya Sheikh Abeid Aman Karume hayajatimizwa kwao Tanzania au katika mataifa jirani.

 

Prof. Ken Walibora ni msomi wa fasihi, mwanahabari na mwandishi mtajika katika ulimwengu wa Kiswahili.