• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Abidal amulika Auba’ baada ya kuponea kisu

Abidal amulika Auba’ baada ya kuponea kisu

Na MASHIRIKA

BARCELONA, Uhispania

BAADA ya kuponea kuangukiwa na shoka, Eric Abidal amedokeza huenda Barcelona wakatafuta huduma za mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang mwisho wa msimu huu.

Abidal ataendelea kuhudumu kama Mkurugenzi wa michezo wa Barcelona licha ya kukosolewa vikali na Lionel Messi.

Mfaransa huyo amenukuliwa na vyombo vya habari nchini Uingereza akimsifu Mgabon Aubameyang.

“Ninamfahamu Aubameyang. Yeye ni mchezaji stadi. Yeye ni muhimu na katika timu yake, amekuwa akitegemewa,” alisema Abidal.

“Ni kitu kizuri kuleta mchezaji mwenye talanta kubwa kama yake. Acha tuone kitakachotokea mwisho wa msimu.

Licha ya kuwa tunatarajia Luis Suarez arejee kwa kishindo, tunahitaji mchezaji stadi mwisho wa msimu,” alisema.

Messi, ambaye ni mshindi mara sita wa tuzo ya mwanasoka bora duniani ya Ballon d’Or, alimlaumu Abidal baada ya Mfaransa huyo kudai kuwa wachezaji hawakujitolea kwa dhati chini ya kocha wa zamani Ernesto Valverde.

Valverde alitemwa mwezi uliopita na nafasi yake kujazwa na Quique Setien.

Barcelona iliitisha mkutano wa dharura na beki wa zamani wa Ufaransa Abidal mnamo Jumatano kujadili suala hilo.

Baada ya saa mbili za mazungumzo, iliamuliwa kuwa Abidal, 40, atasalia na majukumu yake uwanjani Nou Camp.

Abidal, ambaye aliwahi kuwa mchezaji mwenza wa Messi, alitoa matamshi hayo alipohojiwa na gazeti la Diario Sport nchini Uhispania.

Hata hivyo, raia wa Argentina Messi, 32, alijibu, “Unapozungumzia wachezaji, lazima utoe majina kwa sababu usipofanya hivyo, inatoa picha ambayo si sahihi.”

Valverde alipigwa teke Barcelona ikishikilia nafasi ya kwanza kwenye Ligi Kuu nchini humo.

Katika mahojiano na Diario, Abidal alisema, “Wachezaji wengi hawakuridhishwa ama hawakutia bidii na matatizo yalikuwepo katika mawasiliano.

“Uhusiano kati ya kocha na wachezaji ulikuwa mzuri, lakini kama mchezaji wa zamani niliona kuna moshi hapa. Niliambia klabu kile niliwazia kuhusu hali hii na tukafikia uamuzi wa kumtimua Valverde.”

Messi, kisha, alichapisha kwenye mtandao wake wa kijamii kuwa, “Ukweli ni kuwa mimi sipendi kufanya vitu hivi, lakini nadhani watu wanafaa kuwajibikia kazi zao na uamuzi wao.

“Wachezaji wanawajibika kwa kile wanachofanya uwanjani na sisi huwa katika mstari wa mbele kukiri kama hatujafanya vizuri. Viongozi wa idara za michezo wanafaa pia kuwajibika na kuwa tayari kubeba msalaba wao wanapofanya uamuzi.”

Katika mahojiano na gazeti la Diario, Abidal pia alisema alidhani kuwa Messi alikuwa na furaha katika klabu hiyo na kuwa mazungumzo kuhusu kandarasi mpya yanaendelea.

Inasemekana kuwa Messi hakufurahia maelezo ya Abidal ambayo yaliashiria kuwa wachezaji walisababishia Valverde kupigwa kalamu.

  • Tags

You can share this post!

KOMBE LAJA? Spurs waanza kuota taji baada ya kupiga hatua...

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Thawabu anazopata Muumin...

adminleo