• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
Kenya Simbas kualika Morocco mjin Mombasa, Uganda mjini Kakamega na Zimbabwe mjini Nakuru mwaka 2020

Kenya Simbas kualika Morocco mjin Mombasa, Uganda mjini Kakamega na Zimbabwe mjini Nakuru mwaka 2020

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI wa Mombasa, Kakamega na Nakuru watapata kufurahia mechi za kimataifa za raga ya wachezaji saba kila upande baada ya Shirikisho la Raga nchini (KRU) kutangaza Ijumaa kuwa miji hiyo itatumiwa kwa mechi za nyumbani za Kenya Simbas mwaka 2020.

Mashabiki wa raga mjini Mombasa watakuwa wa kwanza kupata burudani hilo wakati Simbas ya kocha Paul Odera itaalika Atlas Lions ya Morocco mnamo Mei 30 katika mechi ya Kombe la Afrika. Kenya na Morocco zimekutana mara nne katika historia yao.

Simbas ilipoteza 29-3 mwaka 2005 na kuchapwa 29-11 mwaka 2009 na inajivunia kuchabanga timu hiyo kutoka kaskazini mwa Afrika 23-16 mwaka 2007 na kuilemea 28-24 mwaka 2018. Inamaanisha kuwa mechi hiyo itakuwa ya kukata na shoka kwa sababu timu hizi zinakaribiana sana kimchezo. Katika viwango bora vya dunia, hata hivyo, Kenya inashikiia nafasi ya 32 nayo Morocco iko katika nafasi ya 48.

Simbas itaalika mahasimu wa tangu jadi Uganda mjini Kakamega mnamo Julai 11. Uganda inapatikana katika nafasi ya 40 duniani. Majirani hawa wawili wamekutana mara nyingi tangu mwaka 1954 ikiwemo mara 28 tangu milenia mpya mwaka 2000.

Simbas ililemewa 16-13 na Uganda mjini Kisumu mwezi Juni 2019 wakati KRU ilipeleka mechi ya kimataifa nje ya mji wa Nairobi kwa mara ya kwanza kabisa. Vijana wa Odera walizaba Waganda almaarufu Rugby Cranes 16-5 katika mechi ya marudiano ya Elgon Cup mnamo Julai 2019, mechi ambayo pia ilikuwa ya Kombe la Victoria baada ya Kombe la Afrika kukosa kufanyika kutokana na ukosefu wa mdhamini.

Kwa mwaka wa pili mfululizo, mechi kati ya Kenya na Sables ya Zimbabwe itachezewa mjini Nakuru. Kenya na Zimbabwe, ambazo zitamenyana Julai 18 mjini Nakuru, zinafahamiana sana. Mwaka 2019, Simbas ilizidiwa ujanja kwa alama 30-29 mjini Bulawayo mwezi Agosti kabla ya kulipiza kisasi 36-14 mjini Nakuru mwezi Septemba. Zimbabwe iliibuka mshindi wa kipute cha Victoria Cup baada ya kucharaza pia Zambia na Uganda nyumbani na ugenini.

Mechi ya Kenya dhidi ya Uganda itatumika pia kama ya Elgon Cup na Victoria Cup, huku ile ya Zimbabwe pia ikitumiwa katika kuamua mshindi wa Victoria Cup. Zimbabwe inashikilia nafasi ya 35 duniani.

You can share this post!

Mtunza bustani nyumbani kwa Moi asema kiongozi huyo...

Hakuna ruhusa kuzua vurugu, mashabiki EPL waonywa

adminleo