• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 AM
Hakuna ruhusa kuzua vurugu, mashabiki EPL waonywa

Hakuna ruhusa kuzua vurugu, mashabiki EPL waonywa

GEOFFREY ANENE na MASHIRIKA

LIGI Kuu ya Uingereza imetangazia mashabiki wa soka nchini humo onyo kali ikisema visa vya utovu wa nidhamu havitakubalika.

Hapo Alhamisi, ligi hiyo ilisema kuwa yeyote atakayefanya kosa na kupigwa marufuku na klabu moja pia atatumikia marufuku hiyo kutoka kwa klabu zote 20.

Akizungumza baada ya sheria hiyo kupitishwa, Mwenyekiti wa West Ham United David Gold alisisitiza kuwa vitisho na vurugu za mashabiki dhidi ya viongozi wa klabu nchini Uingereza havitakubaliwa.

Onyo hilo limetolewa baada ya kundi la watu kuvamia Afisa Mkuu Mtendaji wa Manchester United Ed Woodward likimwimbia kuwa “atauawa.”

Gold anafahamu masuala ya maandamano ya mashabiki kwani aliwahi kuwa muathiriwa.

“Najua kabisa kile Ed anapitia. Nimepitia hali kama hiyo mara nne ama tano,” alisema. “Unachostahili kujua ni kuwa unaweza kwa ghafla kushtukia mamia ya watu waandamana dhidi yako.”

“Unaweza kupata idadi hiyo ya watu watundu ambao wanataka kuteketeza hata nyumba yako. Na utapata watu hao karibu 200 wamekusanya watu wanaowasikiliza ama wanaopita na kujiuliza kinachoendelea.”

Hapo Alhamisi ilitangazwa kuwa mashabiki watakaoonyesha tabia isiyokubalika dhidi ya wachezaji, mashabiki wengine, wafanyakazi wa klabu ama marefa watapigwa marufuku.

“Ligi itashikana kama kitu kimoja kulinda watu kama Ed na kuadhibu wakosaji. Tabia hiyo mbovu haiwezi kukubalika,” alisema Gold.

“Manchester United ni timu kubwa, Ed Woodward ni mtu mkubwa katika mchezo huu. Hawezi kuanza kuhofia maisha ya mke wake na watoto.”

Wakati wa usumbufu katika mechi kati ya West Ham na Burnley uwanjani London mwezi Machi 2018, ambao ulisababisha West Ham kupigwa faini ya Sh13 milioni, Gold alisema kuwa mjukuu wake alimuuliza kama yeye ni mwongo.

Alisema, “Mechi ya Burnley ilikuwa ya kuogofya. Mjukuu wangu alisema, “Babu, wanamaanisha nini? Wewe si mwongo sio babu?’ Ukiulizwa swali kama hilo utaeleza mtoto wa miaka 10 nini?”

West Ham inatarajia kushuhudia maandamano zaidi katika mechi zijazo.

Kuna hali ya kutoaminiana kati ya mashabiki na bodi ya klabu hiyo, hasa Gold, Sullivan na naibu mwenyekiti Karren Brady, ambao wanalaumiwa kwa kutotimiza ahadi walizotoa wakati West Ham ilihamia uwanjani London kutoka Upton Park (Boleyn Ground) mwaka 2016.

Klabu hiyo iko katika mduara hatari wa kutemwa kutoka Ligi Kuu kabla ya kumenyana na mabingwa watetezi Manchester City uwanjani Etihad hapo kesho.

Mwanzo huu wa mfuatano wa mechi ngumu ambao pia utashuhudia West Ham ikizuru Liverpool, Arsenal na Tottenham, pamoja na mechi za nyumbani dhidi ya Wolves na Chelsea, unaweka maisha ya West Ham kwenye Ligi Kuu hatarini chini ya kocha mpya David Moyes.

“Gumzo mitaani ni kuwa sisi ni waongo. Kuwa sisi tumechukua fedha zote. Huo si ukweli,” alisema Gold.

“Sisi si waongo. Tumefanya makosa. David Sullivan si mtu mbaya. Anataka klabu ipate mafanikio. Karren Brady anajitahidi sana kuona klabu hii inafanya vyema. Na kile unachosoma ni vitu vibaya.”

  • Tags

You can share this post!

Kenya Simbas kualika Morocco mjin Mombasa, Uganda mjini...

Wito jopo liundwe kuchunguza vifo vya wanafunzi 14

adminleo