MakalaSiasa

Vita vya Kieleweke na Tangatanga sasa vyaelekea Bungeni

February 9th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta anapanga kudhibiti bunge la kitaifa na lile la seneti ili kuendeleza agenda ya serikali bungeni litakaporejelea vikao vyake Jumatatu baada ya likizo ndefu ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Anapanga kufanikisha udhibiti huo kwa kufanya mabadiliko katika uongozi wa Jubilee katika mabunge hayo mawili kwa kuwapokonya wandani wa Naibu Rais William Ruto nyadhifa zao ili kuzima uasi katika chama hicho.

Wadadisi wanasema hatua hiyo huenda ikadhoofisha zaidi uhasama ambao umekuwa ukitokota kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto, haswa baada ya kufutwa kazi kwa aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri.

Duru zinasema kuwa Rais Kenyatta amekasirishwa na baadhi ya viongozi wa Jubilee wanaoshikilia nyadhifa za uongozi bungeni, na kamati zake, ambao wamekuwa wakimkosoa hadharani tangu aliporidhiana kisiasa na kiongozi wa ODM Raila Odinga Machi 9, 2018.

Tangu wakati huo, wabunge wa Jubilee wamegawanyika kuwili. Kuna wafuasi wa kundi la Tangatanga, ambao wanaunga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu 2022 na wale wa kundi la Kieleweke, inayounga mkono maridhiano hayo, maarufu kama handisheki.

Katika bunge la Seneti, maseneta wanakabiliwa na hatari ya kupoteza nyadhifa zao ni pamoja na kiongozi wa wengi Kipchumba Murkomen na kiranja wa wengi Susan Kihika.

Kwa mfano, wawili hao mwezi jana waliowaongoza wenzao 10 kupambana kwa jino na ukucha kumwokoa aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu hoja ya kumwondoa mamlakani ilipojadiliwa katika seneti juzi.

Hata hivyo, juhudi zao ziligonga mwamba baada ya maseneta wa mrengo wa Kieleweke kuungana na wenzao wa upinzani kuidhinisha hoja hiyo.

Hoja hiyo ilipitishwa na bunge la kaunti ya Kiambu mnamo Desemba 19, 2020.Hatua hiyo ilidaiwa kumkasirisha Rais Kenyatta ikizingatiwa kuwa baadhi ya mashtaka yaliyomkabili Bw Waititu yanahusiana na ufisadi, uovu ambao Rais Kenyatta amejitolea kupambana nao ili kuacha sifa bora atakapoondoka uongozini mnamo 2022.

Aidha, vita dhidi ya ufisadi ni mojawapo ya changamoto tisa ambayo Rais Kenyatta na Bw Odinga waliafikia kupambana nayo chini ya mpango wa maridhiano (BBI).

Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu ambaye ni mwanachama wa mrengo wa Kieleweke amethibitisha uwepo wa mpango wa Jubilee kufanya mabadiliko ya uongozi wake katika mabunge yote mawili.

“Ni kweli kabisa, mipango hiyo ipo na mabadiliko yatatekelezwa tutakaporejelea vikao baada ya likizo. Wenzetu wanaoshikilia nafasi za uongozi katika mabunge yote mawili waliteuliwa kuendeleza ajenda ya rais bunge ilivyoelezwa katika mkutano wa kwanza wa kundi la wabunge wa chama tawala mnamo Agosti 30, 2017.

“Wale ambao hawako tayari kutii ajenda hizo hawana sababu ya kuendelea kushikilia nafasi hizo,” akasema.

Akaongeza, “Hatutawaruhusu wale ambao wametwikwa jukumu la kuendeleza na kutetea ajenda ya serikali kuihujumu walivyofanya mwaka jana. Wale ambao wamekuwa wakimkosea heshima Rais na kuendelea kuhujumu ajenda yake ndani na nje ya bunge sharti wapokonywe afisi hizo mara moja.”

Naye Mbunge wa Tiaty William Kamket anasema Naibu Rais Dkt Ruto analindwa na Katiba na hawezi kufutwa, wandani wake wanaoshikilia nyadhifa kuu katika mabunge yote mawili wataandamwa.“Wakati ni huu, sio mwingine.

Wale ambao wamekuwa wakimkaidi Rais Kenyatta hawafai kuachiwa nafasi ya kutetea ajenda ya serikali bungeni kwa sababu wataihujumu kama ambavyo walifanya mwaka jana,” anasema mbunge huyo aliyechaguliwa kwa tiketi ya chama cha Kanu.

Bw Kamket anasema wenzao wa Tangatanga ambao wanashikilia nyadhifa za uongozi wa kamati za bunge “wasubiri kuunda serikali yao iwape nafasi hizo wala sio serikali hii ya Rais Kenyatta ambayo wamekuwa wakiihujumu kila mara.”

Kando na Murkomen na Kihika, kunao Seneta wa Nandi Samson Cherargei ambaye ni mwenyekiti Kamati ya Seneti kuhusu Haki na Masuala ua Kikatiba na mwenzake wa Bomet Christopher Lang’at ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Elimu.Wawili hawa ni wandani sugu wa Naibu Rais ambao wamekuwa mstari wa mbele kukosoa baadhi ya maamuzi ya serikali wanayohisi yanahujumu nafasi ya Dkt Ruto kuingia Ikulu.

Katika bunge la kitaifa wanaokabiliwa na hatari ya kuangukiwa na shoka ni pamoja na Benjamin Washiali (kiranja wa wengi), naibu wake Cecily Mbarire, Kimani Ichung’wa (mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu Bajeti) miongoni mwa wandani wengine wa Dkt Ruto.

Hata hivyo, duru zinasema kuwa kiongozi wa wengine Aden Duale atasazwa kwa sababu licha ya kuwa mwandani wa Dkt Ruto, “amekuwa mtetezi wa ajenda za serikali ndani na nje ya bunge.”

Kamati ya Bajeti, ambayo ndiyo ya kipekee yenye wanachama 51, ina usemi mkubwa katika mchakato wa utayarishaji bajeti ya kitaifa na ugavi wa fedha kwa wizara na idara mbalimbali za serikali.Jukumu la bunge katika utayarishaji wa bajeti hutekelezwa kupitia kwa uongozi wa kamati hii.

Vilevile, kamati hii ina uwezo wa kuchambua miswada yote ya serikali inayohusisha matumizi ya fedha za umma, hali inayoifanya kuwa wenye umuhimu mkubwa wa serikali ya kitaifa.

Ni kwa msingi huu, ambapo serikali inahisi kamati hiyo haiwezi kuongozwa na mtu “ambaye ametangaza vita dhidi ya Rais”.

Duru zinasema kuwa Mbunge wa Kipipiri Amos Kimunya ambaye aliwahi kuhudumu kama Waziri wa Fedha katika utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki, anapigiwa upatu kuchukua nafasi ya Bw Ichung’wa.

Ingawa utaratibu wa kumwondoa mwenyekiti wa kamati ya bunge ni rahisi, mchakato wa kuwaondoa wanaoshikilia nyadhifa za uongozi bungeni sharti uidhinishwe kwenye mkutano wa kundi la wabunge wa chama husika (PG).

Kwa mujibu wa sheria za bunge, ili mbunge apokonywe wadhifa wa mwenyekiti au naibu mwenyekiti wa kamati, mmoja wa wanachama anahitajika kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani naye.

Na endapo hoja hiyo itaungwa mkono na wanachama wengi wa kamati hiyo, mwenyekiti huyo atakuwa amevuliwa wadhifa wake.Lakini kabla ya kuondolewa kwa Murkomen, Washiali, Kihika na Mbarire kutoka nyadhifa zao sharti uamuzi huo uidhinishwe katika mkutano wa PG ya Jubilee.

Na kumbukumbu za mkutano huo, pamoja na uamuzi wenyewe sharti ziwasilishwe kwa Spika wa Bunge la Kitaifa ndiposa majina yaondolewe kwenye orodha ya uongozi wa Jubilee Bungeni.

Ingawa mrengo wa Tangatanga umekuwa ukiitisha mkutano wa PG kujadili masuala yanayoibua migawanyiko ndani ya Jubilee, Rais Kenyatta amekuwa akipuuzilia mbali shinikizo hizo.

Sasa inasubiriwa kuonekana ikiwa Rais anapiga moyo konde na kuitisha mkutano huo ili kuifanikisha mabadiliko anayotaka bungeni.