• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Maziko ya Moi kuibua kumbukumbu za Jomo

Maziko ya Moi kuibua kumbukumbu za Jomo

Na NYAMBEGA GISESA

SAFARI ya mwisho ya Rais mstaafu Daniel Moi itatoa kumbukumbu ya Mazishi ya Kitaifa ya mtangulizi wake Hayati Mzee Jomo Kenyatta, ambapo taifa zima liliungana kwa huzuni.

Mazishi ya Moi, sawia na ya mtangulizi wake yataendeshwa kulingana na kanuni za kijeshi. Hadhi kama hii pia hupewa marais waliostaafu wakuu wa majeshi waliostaafu na mtu mwingine yeyote kwa idhini ya Baraza la Ulinzi.

Hata hivyo, hafla za mazishi ya Moi itakuwa tofauti kidogo na ile ya Hayati Kenyatta iliyofanyika miaka 42 iliyopita, ikizingatiwa kuwa Kenyatta alifariki akiwa afisini ilhali Moi amefariki baada ya kustaafu.

Kwanza, mazishi ya Mzee Kenyatta yalifanyika siku moja mnamo Agosti 31, 1978 katika majengo ya bunge ambako mwili wake ulipumzishwa.

Lakini shughuli za mazishi ya Moi zitaanza kesho katika Uwanja wa Michezo wa Nyayo, Nairobi hadi Jumatano nyumbani kwake Kabarak, Kaunti ya Nakuru.

Jeneza lenye mwili wake lilisafirishwa kwa gari la kusafirisha silaha kutoka Ikulu ya Nairobi hadi majengo ya bunge huku wananchi waliojawa na huzuni wakisimama barabarani kuomboleza kiongozi ambaye wengi waliamini kuwa angeishi kwa miaka mingi.

Mazishi hayo yaliendeshwa na mseto wa makanisa, wazee wa kitamaduni na viongozi wa dini ya Kiislamu.

Sherehe ilianza pale jeneza lilipowasili katika Ikulu ya Nairobi kutoka nyumbani kwake Gatundu huku maelfu ya watu wakisimama barabarani nyuso zao zikijikunja kwa huzuni.

Kutoka Ikulu, jeneza lilisindikizwa hadi majengo ya bunge kwa gari la kijeshi la kusafirisha bunduki.

Jeneza lilipokuwa likipelekwa katika kaburi, Kasisi Meja S. Mwambire, ambaye alikuwa ni Kasisi wa Jeshi, alitamka maneno ya kufariji.

Muungano wa Kwaya kutoka madhehebu mbalimbali na Bendi ya Wanajeshi ziliimba kwanza kabla ya ibada kamili kuanza.

Baada ya waliohudhuria ibada hiyo kuketi, wimbo kwa jina “O God, Our Help in Ages Past” uliimbwa. Ni wimbo huo huo ulioimbwa wakati wa mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill mnamo Januari 1965.

Wimbo huo ulifuatwa na Wito wa Ibada uliotolewa na Pasta wa Kanisa la Kipresbiteri (PCEA) Kasisi John Gatu baada ya aya za Bibilia kusomwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana wakati huo Festus Olang na Askofu John Njenga ambaye ni Mkenya wa kwanza kutawazwa kama kasisi wa Kanisa Katoliki.

Wengine waliosoma vifungu vya Bibilia na kutekeleza wajibu mbalimbali katika mazishi hayo ni Askofu Zacheaus Okoth, aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana (ACK) nchini David Gitari, Askofu Lawi Imathiu wa Kanisa la Methodist na Askofu Wellington Mulwa.

Mahubiri yalifanywa na marehemu Kasisi Charles Kareri ambaye ni Modereta kwa kwanza wa Kanisa la PCEA, aliyemtaja Kenyatta kama ‘mtu aliyempenda Mungu maishani mwake’ ingawa Rais huyo hakuwahi kudhudhuria ibada kanisani miaka 15 alipokuwa mamlakani.

Baada ya mwili kuwekwa kwenye kaburi, mizinga 21 ilifyatuliwa na kikosi cha 66 Artilley cha Jeshi la Kenya ikifuatwa na gwaride la wanajeshi wa kikosi cha wanahewa.

Ndege za kivita pia zilitoa heshima zao angani. Baada ya jeshi kutoa heshima zao, bendera rasmi ya rais na Bendera ya Taifa ziliwasilishwa kwa wajane wa Mzee Kenyatta ambao ni Mama Ngina Kenyatta na Mama Wahu Kenyatta.

You can share this post!

Huenda pasitokee rais atakayempiku Moi katika kufadhili...

Moi atakavyozikwa kwa heshima ya kipekee

adminleo