ICJ yataka maagizo ya korti dhidi ya serikali yachunguzwe
Na VALENTINE OBARA
BARAZA la Kimataifa la Wanasheria (ICJ) limependekeza uchunguzi ufanywe kuhusu maagizo ambayo mahakama hutoa dhidi ya maafisa wakuu wa serikali.
Pendekezo hilo ni miongoni mwa yale yaliyowasilishwa kwa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama ambayo inachunguza jinsi mwanaharakati wa upinzani, Dkt Miguna Miguna, alivyofurushwa nchini kwa mara ya pili wiki chache zilizopita.
Kulingana na stakabadhi za mapendekezo hayo, ICJ ilikosoa madai yaliyotolewa na Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i, kwamba mahakama imetekwa na wanasiasa wa upinzani na mashirika ya kijamii lakini ikasema inafaa madai hayo yachunguzwe zaidi.
“Madai aina hii yasiyo na msingi wala ushahidi yakiruhusiwa kuzidi kuenezwa kwa umma, imani ya wananchi kwa mahakama itapungua,” shirika hilo likasema, na kuongeza kuwa Dkt Matiang’i anafaa kuomba msamaha kwa madai aliyotoa.
Madai ya waziri huyo yaliendeleza mtindo ambao umekuwa ukionekana kutoka kwa viongozi wa Jubilee tangu mwaka uliopita ambapo walikuwa wakikashifu vikali majaji na hata kutishia kuwaadhibu kwa kutoa maagizo yasiyopendeza serikali, ikiwemo Mahakama ya Juu ilivyofutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8.
Baraza hilo lilitoa wito kwa serikali itii maagizo ya mahakama kikamilifu na endapo kuna malalamishi, serikali itumie sheria na kukata rufaa badala ya kutoa madai hadharani yanayodunisha uhuru wa mahakama.
ICJ pia ilisema matukio yaliyoshuhudiwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) wakati Dkt Miguna alipofurushwa yalitilia doa hali ya usalama katika uwanja huo na hivyo basi maafisa husika, wakiwemo wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Kenya (KAA) wanastahili kuchunguzwa.
Hii ni kutokana na jinsi polisi wenye bunduki walivyoonekana wakitumia nguvu dhidi ya Dkt Miguna, mawakili na wanahabari katika maeneo yanayofaa kuwa na usalama mkubwa na hata kwenye mlango wa ndege iliyokuwa na abiria.
Imependekezwa kuwa Chama cha Mawakili cha Kenya (LSK) kiagizwe kufika mbele ya kamati ya bunge kueleza hatua zilizochukuliwa kulinda usalama na uhuru wa mawakili ambao hutishiwa au kudhulumiwa wakati wanapotekeleza majukumu yao.
Mbali na Dkt Matiang’i, maafisa wengine wakuu wa serikali waliohusishwa na kisa hicho ni Inspekta Jenerali wa Polisi, Bw Joseph Boinnet, na Katibu wa Wizara ya Uhamiaji, Bw Gordon Kihalang’wa.
Kwenye kikao cha wanahabari Nairobi, Mkurugenzi Mkuu wa ICJ, Bw Samwel Muhochi, alisema pendekezo lao ni kuwa watumishi wa umma watakaopatikana na hatia wasimamishwe kazi.