• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Moi alipotoweka kwa wiki moja…

Moi alipotoweka kwa wiki moja…

Na PETER NGARE

TAHARUKI ilizuka nchini mnamo Februari 1995 wakati aliyekuwa rais Daniel arap Moi alipotoweka hadharani kwa wiki moja.

“Huku wananchi wakihofia jambo mbaya limempata Mzee Moi, watoto waliondolewa shuleni, ofisi zikafungwa mapema, watu wakaanza kusafiri mashambani, akina mama wakaanza kununua vyakula kwa wingi na kuviweka manyumbani huku matajiri wakinunua tiketi za ndege tayari kuondoka Kenya mambo yakiharibika,” aliandika Andrew Morton kwenye kitabu kuhusu maisha ya Mzee Moi.

Taharuki hii ilitokea baada ya Mzee Moi kukosa kuonekana hadharani ikiwemo kuhudhuria ibada ya Jumapili ambayo hakuwa akikosa, na habari zake kukosa kusikika kwenye vyombo vya habari.

Kilichofuata ni uvumi wa kila aina uliozuka kote nchini baadhi ya waenezaji wakidai Mzee Moi alikuwa amekufa na wengine wakisema alikuwa hali mahututi hospitalini.

Wasiwasi huo ulizuka kwa sababu Wakenya walikuwa wamezoea kumuona kwenye hafla nyingi kila pembe ya nchi, pamoja na kusikia na kutazama habari kumhusu kwenye redio na televisheni.

Kulingana na mwanahabari Kamau Ngotho, Mzee Moi alikuwa na mbinu zake za kuhakikisha habari zake zimo kwenye vyombo vya habari kila mara, ndiposa alipokosa kuonekana ama kusikika kwenye redio, magazetini na televisheni uvumi na wasiwasi zilizuka nchini.

“Wakati hakuwa na hafla rasmi, angetafuta jambo ambalo lingehakikisha ameangaziwa na wanahabari. Wakati mwingine angesimama kwenye soko kama vile la Kangemi ama Soko Mjinga lililoko Kijabe kununua ndizi, ama kujitokeza katika vibanda eneo la Industrial Area kujumuika na wananchi wa kawaida kunywa chai. Jumamosi ambazo hakuwa na kazi rasmi alihudhuria harusi,” asema Bw Ngotho.

Kwenye kitabu kilichoandikwa na Andrew Morton kuhusu maisha ya Mzee Moi, taharuki iliyozuka wakati huo ilikuwa sawa na hali ilivyokuwa baada ya Mzee Jomo Kenyatta kuaga dunia mnamo 1978 na wakati wa jaribio la mapinduzi ya serikali ya Mzee Moi mnamo 1982.

Viongozi wa upinzani, mabalozi pamoja na wakuu wa kidini walianza kutoa mwito wa serikali kutoa habari kuhusu alikokuwa Mzee Moi ili kuzima uvumi na taharuki, huku vigogo wa Kanu wakiwakemea waliokuwa wakieneza uvumi kuwa Mzee Moi amefariki ama alikuwa hali mahututi.

Ghafla Moi alitokea jijini mchana akitembea katika barabara za Nairobi kutoka ofisini mwake katika Harambee House hadi Majengo ya Bunge huku akishangiliwa na wananchi waliokuwa wamejawa furaha.

Pia alichukua fursa hiyo kuwakejeli waliokuwa wakieneza uvumi kumhusu: “Mkinitazama mnaona kama mimi ni mtu mahututi? Nakaa kama mtu ambaye alikuwa amekufa akafufuka?”

Kulingana na Morton, Mzee Moi alikuwa akiugua kisigino cha mguu wake wa kushoto, hali iliyofanya iwe vigumu kwake kutembea.

Morton anasema kuwa Mzee Moi kutokana na kiburi chake alikuwa amekataa ushauri wa daktari kuwa alifaa kupumzika ndipo aweze kupona akisisitiza hilo lilikuwa jambo ndogo.

Hatimaye daktari wake David Silverstein alifanikiwa kumshawishi kupumzika kwa siku chache.

“Kama alivyokuwa hapendi kuonekana amevaa miwani hadharani kwani kwake ilikuwa ishara ya unyonge, Mzee Moi hakutaka kuonyesha ulimwengu alikuwa anaugua ndiposa akaamua kutoonekana hadharani alipokuwa akipata nafuu,” aeleza Morton.

Kulingana na Morton, Mzee Moi pia alitumia fursa hiyo kuona jinsi watu wangechukulia habari zake kutoonekana hadharani.

Morton anasema kuwa wasiwasi uliokuwa nchini ulihusu hasa hali ya kung’ang’ania uongozi ingekuwa iwapo kweli Moi angekuwa amekufa kama ulivyosema uvumi.

You can share this post!

Baadhi ya madereva wadai hafla ya kitaifa imewaondolea...

Wakazi wa mtaa wa Landless walalama kuhusu ongezeko la visa...

adminleo