• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 4:25 PM
Hezekiah Oyugi: Katibu aliyepigiwa saluti na wakuu wa wilaya wakipokea simu zake

Hezekiah Oyugi: Katibu aliyepigiwa saluti na wakuu wa wilaya wakipokea simu zake

Na PETER NGARE

ALIYEKUWA Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani wakati wa utawala wa Mzee Daniel Arap Moi, Hezekiah Oyugi anakumbukwa na waliokuwa maafisa wa utawala kama vile wakuu wa mikoa, wilaya na machifu kutokana na jinsi walivyomwogopa.

“Aliogopwa kiasi kuwa alipopigia simu wakuu wa wilaya, wengi walikuwa wakisimama na kupiga saluti wakipokea simu zake mara waliposikia sauti ya Oyugi,” asimulia Andrew Morton kwenye kitabu chake kuhusu maisha ya Mzee Moi.

Morton anaeleza kuwa Oyugi alikuwa mwenye nguvu wakati akihudumu kama katibu wa usalama wa ndani na watu pekee waliomtisha ni aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Simeon Nyachae na Nicholas Biwott aliyekuwa Waziri wa Kawi.

Wakati Bw Nyachae alipoingia katika siasa, Bw Oyugi na Bw Biwott walishukiwa kuhusika katika kuzima azma yake ya kuchaguliwa Mbunge, na hapo akawa amemwondoa mmoja wa watu wawili waliomtisha.

Morton anaeleza kuwa Mzee Moi alipenda sana kupiga ngumzo na Bw Oyugi kutokana na vicheko na mzaha wake, na alimwamini kwani mnamo 1982 baada ya jaribio la mapinduzi alikuwa ameapa kuwa alikuwa tayari kufa kwa ajili ya Mzee Moi.

Ushawishi wake unaripotiwa ulikuwa mkubwa zaidi katika utumishi wa umma na polisi alikuwa na maono ya kuwa rais siku moja, jambo ambalo alikuwa akisema mara kwa mara.

“Alikuwa akitaka kwanza kuwa kiongozi wa Waluo ili ateuliwe makamu wa rais na kuwa katika nafasi bora ya kumrithi Mzee Moi,” mmoja wa washirika wake aliripotiwa.

Katika uchaguzi wa mlolongo mnamo 1988, Bw Oyugi, ambaye alikuwa akithibiti wakuu wa mikoa, wilaya na machifu, alihakikisha wanasiasa kutoka Luo Nyanza waliokuwa na ushawishi wameondolewa.

Pia alihakikisha hilo limefanyika maeneo mengine kwa kuwaondoa vigogo kama Charles Rubia na Kenneth Matiba eneo la Kati na Masinde Muliro wa Magharibi.

Morton anaeleza kuwa kutokana na kupungua kwa ushawishi wa Jaramogi Oginga Odinga katika siasa za Nyanza, Bw Oyugi aliona kuwa mtu pekee aliyetishia ndoto zake ni aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni, Robert Ouko, ambaye alielezwa kuheshimiwa sana na Mzee Moi.

Miezi michache baadaye mnamo Februari 13, 1990. Bw Ouko aliuawa na Bw Oyugi akawa akitajwa miongoni mwa washukiwa wakuu.

Mauaji hayo yanaelezwa yalimsikitisha sana Mzee Moi ndiposa akaalika wapelelezi wa Scotland Yard kutoka Uingereza wakiongozwa na John Troon.

Morton anasema Bw Oyugi alikuwa akiingilia uchunguzi wa Troon kwa kuwatumia maafisa wa polisi waliovaa kiraia.

Vitendo vya Bw Oyugi vilizua tetesi zaidi kuhusu jukumu lake katika mauaji hayo hasa alipotuma mshukiwa mwenzake Jonah Anguka, ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Nakuru kupokea Troon jijini Nairobi.

Kitendo hicho kilimfanya Mkuu wa Mkoa wa Rift Valley wakati huo Yusuf Haji kulalamika kwa Bw Oyugi.

Baada ya uchunguzi, Troon alikabidhi ripoti yake kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Matthew Muli ambapo aliwataja Bw Biwott na Bw Oyugi kama washukiwa wakuu.

Bw Oyugi ndiye aliyempatia Mzee Moi mukhtasari wa matokeo ya ripoti ya Troon ambapo alipuuza mapendekezo yaliyokuwemo na badala yake akazua nadharia kuwa Dkt Ouko alikuwa amejitoa uhai.

Mzee Moi alibuni kamati ya uchunguzi lakini Bw Oyugi akaripotiwa kuingilia shughuli zake.

Mnamo Novemba 1991, Oyugi, Biwott, Anguka na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Nyanza Julius Kobio miongoni mwa wengine walitiwa mbaroni kwa madai ya kumuua Dkt Ouko.

Siku chache baadaye wengine waliachiliwa isipokuwa Biwott, Oyugi na Anguka ambao waliachiliwa baada ya wiki mbili isipokuwa Anguka ambaye alishtakiwa kwa mauaji ya Dkt Ouko lakini hata naye aliachiliwa baadaye.

Baada ya sakata hiyo Mzee Moi aliwafuta kazi Biwott, Oyugi na Kobia.

Morton anasema Oyugi alikuwa mpweke baada ya kufutwa kazi na sakata ya mauaji ya Dkt Ouko. Aliaga dunia mwaka mmoja baadaye jijini London alikokuwa akitibiwa.

Kulingana na Morton, mauaji ya Dkt Ouko yalimsumbua sana Mzee Moi kwani alimpoteza waziri na rafiki aliyekuwa mwaminifu na mchapa kazi, na uvumi kuwa alihusika kwenye mauaji hayo ulimuumiza zaidi moyoni.

“Ningewezaje kumuua waziri niliyemwamini sana,” Mzee Moi alinukuliwa na Morton.

Anasema kuwa tangu hapo Mzee Moi alianza kukosa imani na washirika wake wa karibu.

“Baada ya sakata ya Oyugi, Moi alianza kuwashuku wote waliokuwa karibu naye. Kila alipoona unamkarabia sana alikuwa akijindoa kwa sababu hakuwa akimwamini yeyote tena,” akasema Prof Philip Mbithi aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma kati ya 1992 na 1996.

You can share this post!

Serikali kusafirisha waombolezaji hadi Kabarak

Mabasi 34 kusafirisha wakazi wa Baringo kuaga Moi

adminleo