• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
PATA USHAURI WA DKT FLO: Uvimbe kwenye tezi huletwa na nini?

PATA USHAURI WA DKT FLO: Uvimbe kwenye tezi huletwa na nini?

Na DKT FLO

Mpendwa Daktari,

Kwa wiki kadhaa sasa mume wangu amekuwa akikumbwa na uvimbe kwenye tezi zake za uume. Amekuwa akiona aibu ya kutafuta matibabu na sijui nifanye nini. Tatizo nini?

Mama Liz, Mombasa

Mpendwa Mama Liz,

Wanaume huwa na kiungo kidogo kiitwacho tezi kilicho chini ya kibofu cha mkojo na ambacho huzingira mrija unaondoa mkojo mwilini (urethra). Hili ni tatizo ambalo hukumba sana wanaume wenye umri zaidi ya miaka 45. Haijulikani nini hasa kinachosababisha tatizo hili, japo ni shida ambayo hushuhudiwa sana miongoni mwa wanaume walio na matatizo ya tezi za uume, au wale ambao jamaa zao wa kiume wanakumbwa na matatizo haya.

Ishara ni pamoja na kushindwa kuondoa mkojo wote kwenye kibofu unapokojoa, kukojoa kila mara; hata wakati wa usiku, mtiririko dhaifu wa mkojo wakati wa kwenda choo, kuvuja mkojo, kulazimisha mkojo kutoka, maumivu wakati wa kukojoa na wakati mwingine damu kwenye mkojo. Ni rahisi kukumbwa na maambukizi kwenye mfumo wa mkojo (Urinary Tract Infection-UTI), njia ya kupitisha mkojo ikizibwa. Tatizo la njia ya mkojo kuzibwa likiwa kubwa zaidi, mkojo hukusanyika na kurejea kwenye figo na hii yaweza sababisha matatizo ya figo.

Itakuwa vyema ikiwa atapata huduma ya daktari wa mfumo wa mkojo (urologist) ili afanyiwe uchunguzi zaidi wa mkojo, tezi za uume, utaratibu wa prostate specific antigen (PSA), uchunguzi wa miyale ya sauti (ultrasound), uchunguzi wa seli (prostate biopsy) na uchunguzi wa ukuta wa kibofu na mrija unaondoa mkojo mwilini (cystoscopy). Huenda baadhi ya dawa kama vile za kukabiliana na msongo wa mawazo, dawa za kutibu mzio na dawa za kupunguza shughuli za ubongo pia zikachangia tatizo hili. Tiba inahusisha dawa au upasuaji kulingana na kiwango cha tatizo.

Nyumbani, anapaswa kukojoa pindi anapohisi kufanya hivyo, na pia anaweza unda ratiba ya kwenda choo hata ikiwa wakati huo hahisi kufanya hivyo. Anapaswa kujiepusha na pombe na kafeini. Aidha, anapaswa kuhakikisha kwamba anadumisha joto mwilini, utulivu na kufanya mazoezi.

 

Mpendwa Daktari,

Nitajuaje mimba ambayo mpenzi wangu amebeba ni yangu pasipo kumpa vidokezi kwamba namshuku?

Njesh, Nairobi

Mpendwa Njesh,

Njia ya pekee ya kutambua iwapo mimba hiyo ni yako ni kwa kufanyiwa uchunguzi wa DNA, ambapo bila shaka mwenzio atahusika. Aidha, unaweza jaribu kukumbuka iwapo mlijamiiana tarehe ambazo huenda alishika mimba. Wahudumu wa kimatibabu huhesabu kipindi cha ujauzito kutoka siku ya mwisho ambayo hedhi ilianza, sio siku ambayo mwanamke alishika mimba. Kwa mfano, ikiwa mwanamke alishika mimba wiki nne zilizopita lakini alishuhudia hedhi wiki mbili kabla ya wakati huo, mimba hiyo inahesabiwa kuwa ya wiki sita. Mfumo huu hata hivyo sio kamili na hivyo hauwezi kutambua iwapo mimba ni yako kwa huo msingi.

 

Mpendwa Daktari,

Mwanangu amekuwa akikumbwa na choa (ringworms) kila mara. Nimejaribu kumpa matunda na mboga kwa wingi, vile vile kumpa dawa za minyoo bila mafanikio. Nitapata vipi suluhisho la kudumu?

Nancy, Eldoret

Mpendwa Nancy,

Choa hutokana na maambukizi ya ukuvu na hivyo zinapaswa kutibiwa na dawa za kukabiliana na ukuvu (anti-fungal medication). Dawa hizi zaweza kuwa tembe, krimu, shampuu au mwunganisho wa hizi zote. Kutokana na sababu kuwa maambukizi haya hutokea kila mara, huenda akahitaji tembe za kukabiliana na ukuvu, dawa ambazo atatumia angaa kwa mwezi mmoja. Aidha, itakuwa bora iwapo utamuona daktari na ikiwezekana mtaalamu wa ngozi ili atibiwe. Huenda pia anapata maambukizi mapya kutoka kwa watu walio karibu naye, na hivyo pia wao wanapaswa kupokea matibabu ili kukomesha maambukizi. Dawa za minyoo hazitibu choa. Dawa hizi huondoa minyoo ambayo huenda imo kwenye mfumo wake wa utumbo. Aidha, mabadiliko ya lishe hayasaidii katika kuondoa maambukizi ya ukuvu.

You can share this post!

Kifo cha Moi na biashara jijini Nairobi

Babangu alipenda nyama hasa ya mbavu, Gideon hatimaye...

adminleo