• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
NDIVYO SIVYO: ‘Mapua’ ni neno linalotumiwa kimakosa katika mawasiliano

NDIVYO SIVYO: ‘Mapua’ ni neno linalotumiwa kimakosa katika mawasiliano

Na ENOCK NYARIKI

SHULENI ni mahali mwafaka si tu katika kujifunzia lugha ya pili bali pia kuisarifu lugha yenyewe.

Shule hukuza na kuendeleza matumizi ya lugha sanifu. Aidha, hukosoa matumizi mabaya ya lugha ambayo chanzo chake ni nyumbani na kwenye jamii pana.

Majukwaa mawili tuliyoyataja – nyumbani na jamii pana – yana uhuru wa kuitumia lugha yapendavyo. Kwa hivyo, msingi thabiti wa kuhimiza matumizi sanifu ya lugha ukikosekana shuleni, makosa mbalimbali huendelea kujirudia katika mazungumzo.

Nimewahi kulisikia neno ‘mapua’ kwenye tangazo la biashara kuhusu sabuni ya kufulia nguo. Tangazo hilo lililitumia neno hilo kwenye muktadha uliokusudiwa kuibua ucheshi. Kwa hivyo, badala ya kuwasilisha dhana ya kiungo cha mwili wa binadamu au mnyama kilicho juu ya midomo na kinachotumiwa kuvutia hewa au kunusia, liliibua maana ya harufu ya shombo.

Shombo ni harufu kali ya samaki akiwa mbichi. Baadhi ya wanajamii hulitumia neno ‘mapua’ wanapokusudia kurejelea tundu mbili zilizo kwenye pua. Tundu hizo, bali si kiungo chenyewe, hudhaniwa kuwa pua. Kwa hivyo, matumizi ya kiambishi {ma} mwanzoni mwa neno ‘pua’ hutarajiwa kuibua dhana ya wingi – kwamba binadamu ana pua mbili.

Ukweli wa mambo hata hivyo ni kuwa viumbe wana pua moja yenye tundu mbili.

Tundu hizi huitwa mianzi ya pua. Neno mwanzi linatokana na sifa ya kimaumbile ambapo pua huwa na uwazi mwembamba kama ule unaopita ndani ya mmea unaofanana na mua ambao huitwa mwanzi.

Kosa jingine ambalo hutendwa na watu ni kuiweka nomino pua kwenye ngeli ya Li- Ya. Kwa hivyo watu hao hupenda kusema ‘pua lake’ badala ya pua yake.

Aghalabu nomino ambazo hupatikana katika ngeli ya Li-Ya huonyesha sifa ya ukubwa. Hata hivyo, pua ni kiungo ambacho kina ukubwa wa kawaida, jambo ambalo linatufanya kukirejelea kama pua yake.

Neno jingine ambalo limezoeleka katika matumizi ni mdomo. Neno hili hutumiwa kwa maana ya kinywa ingawa kusema kweli hivi ni viungo viwili tofauti. Mdomo ni sehemu ya nje ya kinywa ambayo hufunguliwa ili kuingiza chakula kinywani. Maana ya pili ya mdomo ni uwazi wa kitu kama vile mtungi au chupa ambao hutumiwa kuingiza vitu ndani ya vitu hivyo. Maana hii ya pili imetokana na maana ya kwanza.

Alhasili, binadamu na viumbe wengine huwa na pua moja yenye mianzi miwili.

Ni kosa kusema kuwa harufu kutoka kwenye jaa la takataka inaumiza *mapua!

You can share this post!

FAO yaonya uvamizi wa nzige unahatarisha upatikanaji wa...

GWIJI WA WIKI: Mwalimu Namanda

adminleo