• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Uhuru afichua alivyomhepa Moi kwa wiki nzima

Uhuru afichua alivyomhepa Moi kwa wiki nzima

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatano aliibua kicheko katika ibada ya mazishi ya Rais Mstaafu Daniel arap Moi aliposimulia jinsi Moi alivyokuwa mkali.

Rais Kenyatta alifichua kuwa aliwahi kumhepa Mzee Moi kwa wiki nzima baada ya kufanya kosa.

Kulingana na Rais Kenyatta, Mzee Moi alimpigia simu saa kumi na moja alfajiri lakini kwa vile alifahamu kosa alilofanya siku iliyotangulia, akamwambia mkewe, Bi Margaret Kenyatta ajibu simu.

Alidhani ameponyoka mkewe alipomdanganya Moi kwamba hakuwa karibu.

“Baada ya dakika nyingine tano simu ikalia tena, mama akaniambia ‘hiyo sichukui’, nikasema basi acha nichukue,” akasimulia.

Mzee Moi alipomuuliza alikuwa wapi alipompigia simu mara ya kwanza, Rais Kenyatta alimwambia akioga.

Licha ya kuomba msamaha mara kadhaa, alisema Moi alizidi kuchemka na kumwagiza afike Nakuru kabla katika muda wa saa moja.

“Nilijua mjinga peke yake ndiye anayeweza kujipeleka kwa moto. Ilibidi nikapotea kwa karibu wiki moja nikajiambia simkaribii mpaka hilo joto liishe,” akaeleza.

Hata hivyo, alisema Mzee Moi alikuwa na moyo wa kusamehe watu licha ya ukali wake.

Huku akimtaja marehemu kuwa mlezi wake tangu babake Mzee Jomo Kenyatta alipofariki mnamo 1978, Rais Kenyatta aliwaambia Wakenya waige maisha aliyoishi Moi.

“Tuzo kuu tunaloweza kumpa ni kuendelea kuiga maisha yake kwa kila tunachofanya kila siku,” akasema.

Rais alieleza kuwa Mzee Moi ndiye alimfunza mambo mengi ya kimaisha tangu alipokuwa kijana hadi akajitosa katika siasa.

“Huyu Mzee alisimama nasi na akatushika mkono mpaka tukafika mahali ambapo tumefika. Kwa hivyo nikisema ya kwamba niko hapa kusema kwaheri kwa baba, hiyo ni haki,” akasema.

Aliongeza: “Nilipata mawaidha kutoka kwa Mzee Moi ambayo nimeyatumia maisha yangu yote.”

Alimtaja Mzee Moi kama Profesa na mwalimu nambari moja wa siasa za Kenya.

Katika mwaka wa 2002, Mzee Moi alimtangaza Rais Kenyatta kuwa mrithi wake wa ugombeaji urais kupitia chama cha KANU alipostaafu.

Rais Kenyatta aliahidi kuwa serikali itashirikiana na familia ya Mzee Moi kukamilisha miradi aliyoanzisha akiwa hai ikiwemo ujenzi wa hospitali ya rufaa ya Kabarak.

Pia alitangaza kuwa serikali ina mpango wa kujenda mradi wa kuzalisha kawi inayotokana na jua.

You can share this post!

Rais Mstaafu Daniel Arap Moi azikwa nyumbani Kabarak

Hatimaye Moi alazwa

adminleo