• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Huyo Mo Farah sio tishio tena, yasema AK

Huyo Mo Farah sio tishio tena, yasema AK

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa timu ya taifa katika Shirikisho la Riadha Kenya (AK), Julius Kirwa, asema kurejea kwa nyota Mo Farah katika mbio za mita 10,000, hakutayumbisha matumaini ya Kenya kutawala fani hiyo kwenye Olimpiki za 2020 jijini Tokyo.

Farah wa Uingereza ndiye mtimkaji anayejivunia ufanisi mkubwa zaidi katika ulingo wa riadha. Amethibitisha kwamba atashuka ugani kuwania nishani ya dhahabu katika mbio za 10,000m jijini Tokyo.

Hii ni licha ya kustaafu miaka miwili iliyopita na kujibwaga katika mbio za masafa marefu za marathon, ambako hajafanikiwa huku akiambulia nafasi ya nane katika Chicago Marathon mwishoni mwa mwaka uliopita.

Michezo ijayo ya Olimpiki itampa Farah nafasi maridhawa ya kujizolea nishani ya 11 ya dhahabu katika historia yake ya mbio za 10,000.

“Nina kiu ya kutetea ufalme wa mbio za mita 10,000 nchini Japan. Nimekuwa nikishiriki mazoezi ya kuboresha kasi yangu na ninahisi kwamba niko tayari kabisa kutifua kivumbi jijini Tokyo,” alisema.

Farah, 36, anajivunia dhahabu nne za Olimpiki baada ya kutawala mbio za mita 5,000 na 10,000 katika makala yaliyopita ya London, Uingereza (2012) na Rio, Brazil (2016).

Kocha Kirwa amesisistiza kuwa Kenya iko tayari kutesa nchini Japan licha ya kudorora pakubwa kwa makali ya wanariadha wake katika nyanja ya kimataifa kwa upande wa wanaume.

Tangu 2005 ambapo Benjamin Limo alitawala fani hiyo katika Riadha za Dunia jijini Helsinki, Finland, Kenya haijawahi tena kunyakua medali ya dhahabu.

Kwa zaidi ya miakja 10 sasa, medali hiyo imetwaliwa na Kenenisa Bekele wa Ethiopia na Mo Farah, ambaye ni mzaliwa wa Somalia.

Rekodi ya Kenya katika mbio hizo hususan michezo ya Olimpiki haijakuwa ya kuridhisha, katika kipindi cha miaka 31 iliyopita.

John Ngugi ndiye Mkenya wa mwisho kuwahi kutia kapuni dhahabu katika mbio hizo kwenye Olimpiki za Seoul, Korea Kusini, mnamo 1988.

Tuwei na Kirwa wanashikilia kwamba vikao kadhaa ambavyo wamekuwa navyo na wanaridha wa Kenya vimebaini tatizo lililopo, na hivyo wanatarajia makubwa kikosi kinapojiandaa kwa Olimpiki.

“Hakika, mbio za mita 10,000 zimekuwa zikiwaumiza vichwa mashabiki, wanariadha na vinara wa AK kwa kipindi kirefu. Lakini tumefanya vikao na kubuni suluhu la kudumu,” Kirwa alieleza.

Wakenya wanaotazamiwa kutoa ushindani mkali kwa Farah nchini Japan ni Geoffrey Kamworor, Alex Oloitiptip wa KDF, chipukizi Rhonex Kipruto na Rodgers Kwemoi aliyeibuka mfalme wa dunia kwa vijana wasiozidi miaka 20 mnamo 2016.

Mwingine atakayekuwa sehemu ya kikosi hicho nchini Qatar ni mwanaridha wa masafa marefu Alex Oloitiptip wa KDF.

You can share this post!

Fifa yabuni hazina ya kulinda masilahi ya wachezaji soka

Jose Mourinho awakasirisha Man-United

adminleo