KIU YA UFANISI: Badala ya mbao anatumia miti kutengeneza fanicha maridadi
Na CHARLES ONGADI
NI vyombo vya nyumbani vinavyotengenezwa kwa kutumia miti na ambavyo vimeondokea kupendwa sana na watu wa tabaka mbalimbali Pwani.
Kandokando mwa barabara ya Mombasa kuelekea Kilifi katika steji ya matatu ya Saga, iliyoko mita chache tu kutoka Chuo cha Ualimu cha Shanzu, Mombasa, tunakuta vifaa kama meza, viti, viweko vya kuangika nguo na vyatu ambavyo vimeundwa kwa kutumia miti vikiwa vimepangwa kwa umaridadi tayari kuuziwa wateja.
Kwa upande wa pili, moshi mkali unafuka huku miti iliyokatwa vipande vipande ikichomeka chini ya uangalizi wa Julius Nyagah.
Nyagah, 50, ambaye ni mzaliwa wa Karangare, Embu, aliamua kuacha kazi yake ya muda mrefu ya ufundi wa kutengeneza jiko na kujitosa katika biashara hii ambayo anasema imebadilisha mno maisha yake.
Ijapo hapo awali wengi walikebehi biashara hii kama isiyo na faida, wengi hasa vijana wameanza kukubali kwamba ni biashara inayoweza kubadilisha maisha endapo itafanywa kwa umakini.
Wakati biashara inanoga, Nyagah ana uwezo wa kuvuna kiasi cha kati ya Sh25,000 hadi 30,000 kwa siku huku wakati wa kusi akiweza kurudi nyumbani na Sh1,000 ama hata patupu.
Kulingana na uchunguzi uliofanywa na Akilimali, wananchi wa Pwani hupenda kununua vyombo hivi hasa viti, meza na viweko vya kuangika viatu kutokana na kwamba vinapendeza na kuvutia na ikizidi bei ni nafuu kwao.
Nyagah anaungama kwamba wateja wake wengi huwa ni wananchi wa kawaida hasa vijana ambao huvutiwa na umaridadi wa vyombo hivi.
“Hapa ninachohitaji ni miti ambayo naichoma kisha kuipinda kulingana na muundo wa ninacholenga kuunda kisha baada ya kumaliza napaka rangi ili kuvutia zaidi na kuzizuia kuvamiwa na wadudu waharibifu,” asema Nyagah.
Hata hivyo, Nyagah anakiri kwamba ili kuunda vifaa vinavyopendeza, kunahitajika ujuzi wa hali ya juu na kujituma kila mara.
Alianza kazi hii mwaka wa 2006 kwa mtaji wa Sh500 pekee ambapo kwa siku alikuwa akiunda viti viwili na meza moja na kuviuza kwa kati ya Sh250 hadi 300.
Lakini baada ya kazi kuanza kunoga, akaongeza mwendo ambapo alikuwa akiunda viti vinne na meza moja na kutia kibindoni Sh1,500 kwa siku.
Mara baada ya kubaini ubora wa bidhaa zake wateja walianza kufurika kila siku kununua jambo lililompelekea kuwaza na kuwazua jinsi ya kupanua zaidi biashara hii.
Na kama wasemavyo wavyele kwamba mkono mmoja hauvunji chawa, aliamua kuwaleta wenzake zaidi ili kufikia malengo ya wateja wake.
Akiwa na wenzake wanne, Jackson Mwendwa, Josphat Muthee, Daniel Musyoka na Michael Wambua walisaka mtaji zaidi na kupanua biashara yao.
“Niliamua kushirikiana na wenzangu hao na kugawanyana majukumu kwa lengo la kufikia mahitaji ya wateja wetu,” asimulia Nyaga.
Nyanga anasema kwamba kwa sasa wanauza kiweko kimoja cha kuangika viatu kwa kiasi cha Sh800 wakati kiangika nguo kikienda kwa Sh2,500 na kishikilia bidhaa kwa kati ya Sh1,200 hadi Sh1,500.
Wakati meza na kiti wakiuza kwa Sh500.
Aidha, kati ya changamoto wanazopitia wa sasa ni kuadimika kwa miti hasa baada ya serikali kutoa onyo dhidi ya ukataji wa kiholela wa miti.
Pia huwa ni vigumu kwao kufanya kazi msimu wa mvua na pia wakati mwingine uhangaishwa na askari wa kaunti ya Mombasa.