• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 8:55 PM
MWANAMKE MWELEDI: Jina lake halikosi sekta ya biashara

MWANAMKE MWELEDI: Jina lake halikosi sekta ya biashara

Na KEYB

YEYE ni Mkurugenzi wa Mpango wa The Stanford Graduate School of Business East Africa’s Seed Transformation Programme.

Katika wadhifa huu, baadhi ya majukumu yake Patricia Ithau ni kusimamia na kuhakikisha kwamba mipango ya shirika hili inatekelezwa vilivyo. Pia, yeye huchagua na kutathmini washiriki wa mpango huu.

Bi Ithau ni Mkurugenzi msimamizi wa zamani wa shirika la L’Oreal East Africa, wadhifa aliouacha mwaka wa 2014 baada ya kuhudumu kwa miaka mitatu.

Katika kipindi chake cha kuhudumu, alihusika pakubwa katika kuimarisha mauzo ya bidhaa za mafuta za Nice & Lovely, suala lililoimarisha faida ya kampuni hiyo.

Aidha, wakati huo huo alikuwa akisimamia shughuli za kampuni za L’Oréal na Inter-consumer Products. Hatua hii ilikuwa muhimu hasa baada ya kampuni ya L’Oréal kuinunua ile ya Inter-consumer Products.

Januari mwaka wa 2016, Bi Ithau aliteuliwa kama mkurugenzi asiye na mamlaka wa Benki ya Barclays.

Alihudumu kama mkurugenzi wa mauzo wa shirika la East Africa Breweries (EABL) nchini Kenya kati ya mwaka wa 2005 na 2008, kabla ya kupandishwa madaraka na kuwa mkurugenzi msimamizi wa EABL nchini Uganda.

Alikuwa mkurugenzi msimamizi wa EABL International kati ya mwaka wa 2009 hadi 2011 ambapo alihusika pakubwa katika upanuzi wa shirika hili kufikia soko la Sudan Kusini. Aidha, aliwahi hudumu kama mkuu wa mashirika ya Head of Culinary Innovation Centre na Unilever, Afrika Kusini.

Mbali na hayo, Bi Ithau pia amehudumu katika bodi mbalimbali. Kwa mfano alikuwa mwenyekiti wa bodi ya hospitali ya Nairobi Women’s kati ya mwaka wa 2009 na 2012. Aidha, anahudumu katika bodi ya ushauri ya Chuo Kikuu cha Strathmore, na amewahi kuwa mwanachama wa bodi ya utalii nchini (Kenya Tourism Board) na ile ya Brand Kenya.

Kando na hayo Bi Ithau ni mwanabodi asiye na mamlaka katika mashirika kama vile Trade Mark East Africa (TMEA), shirika ambalo lengo lake limekuwa kuimarisha ustawi wa eneo la Afrika Mashariki na kuimarisha ushindani. Aidha, yeye ni mwanachama wa muungano wa mashirika katika sekta ya kibinafsi nchini (Kenya Private Sector Alliance (KEPSA).

Pia, amekuwa mkurugenzi wa ushauri wa shirika la Invest in Africa (IIA) tangu Februari 2016. Lengo la shirika hili limekuwa kuunda nafasi za ajira na kuimarisha mazingira ya kibiashara kwa wawekezaji na biashara ndogo.

Aidha, shirika hili lianuiwa kuimarisha mwunganisho baina ya mashirika ya kimataifa na kampuni ndogo humu nchini na kufanya iwe rahisi kwa soko na fedha kufikiwa.

Ana shahada ya digrii ya kibiashara kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, na shahada ya uzamili katika masuala ya kibiashara kutoka chuo kikuu cha United States International University.

You can share this post!

Mwili wa mvuvi aliyetoweka wapatikana Ziwa Victoria

DCI kumhoji Washiali kuhusu uvamizi videoni

adminleo