Makala

MUTUA: Bashir atapigwa mnada duniani apende asipende

February 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na DOUGLAS MUTUA

KUNA msemo maarufu wa eneo la Mlima Kenya unaosema kwamba mnyama yeyote anayetembea ardhini hakosi mwindaji hodari wa kumnasa.

Kawaida msemo huo hutumika kumuonya mkaidi anayejiona sugu sana hivi kwamba anafanya ya ovyo kwa raha zake na kuepuka adhabu kwamba siku yake itafika.

Nimekumbuka msemo huo baada ya kusikia aliyekuwa Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, atakabidhiwa kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) na serikali mpya ya Sudan.

Amekuwa mtoro kwa miaka mingi kwani mahakama hiyo ilitoa vibali viwili vya kumkamata ili apandishwe kizimbani kwa tuhuma za dhuluma dhidi ya binadamu.

Inadaiwa kwamba Bashir alichochea, akapanga na kufadhili ufurushaji wa watu kutoka makwao, ubakaji na mauaji eneo la Darfur. Alipinduliwa na majeshi mwaka jana, lakini vibali vya kumkamata vilitolewa miaka mingi tu akiwa uongozini ila akashupaa shingo na kusema hajisalimishi ng’o!

Alipokuwa uongozini, wapambe wake walitishia kwamba iwapo yeyote angethubutu kumkamata popote pale, basi ufyatulianaji risasi ungetokea na watu wangekufa!

Mahakama Kuu ya Kenya ilitoa kibali cha kumkamata kwa niaba ya Hague mnamo 2011, lakini kiliondolewa na Mahakama ya Rufaa miaka miwili iliyopita.

Kiongozi huyo aliyepindua serikali mnamo 1989 alijiamini mno hivi kwamba alikuwa akizuru mataifa ya Kiafrika na ya Kiarabu.

Hakujua ingekucha siku moja ajipate korokoroni, awe wa kupigiwa bei kati ya watawala wapya wa Sudan na yeyote anayemtaka.

Tishio la milio ya risasi halipo tena, si hatari kumkabidhi kwa watu kwani amevishwa pingu, sikwambii atapelekwa kwenye mahakama hiyo iliyo jijini Hague bila hiari.

Serikali mpya ya Sudan imeahidi kwamba haitamkabidhi kwa ICC peke yake bali pamoja na wapambe wake wawili ili wajibu mashtaka hayo mabaya zaidi duniani.

Tayari anatumikia kifungo cha miaka miwili hivi kwa kupatikana na hatia ya ufisadi na utakatishaji pesa na ninashuku kwamba Sudan itashikilia kuwa akimalize kwanza.

Muda huo utatosha kuwapa watawala wapya wa nchi hiyo fursa ya kupiga bei na mataifa ambayo labda yanataka kumuona Bashir kizimbani Hague.

Kumbuka ni wakati wa utawala wake ambapo Sudan iliingizwa kwenye orodha mbovu zaidi kuwahi kuingiwa na mataifa machafu duniani. Mathalan, kila orodha ya mataifa ambayo hufadhili ugaidi duniani ilipotolewa na Marekani, Sudan ya Bashir haikukosekana.

Uchunguzi uliofanywa miaka kadhaa iliyopita, ulionyesha jinsi silaha hatari zilivyokuwa zikisafirishwa kutoka Sudan hadi Mashariki ya Kati kuhujumu taifa la Israel, rafiki mkuu wa Marekani.

Makosa ya Sudan chini ya utawala wa Bashir yalikuwa mengi hivi kwamba iliwekewa vikwazo vya kiuchumi, silaha na kadhalika, maisha yakawa magumu mno kwa raia.

Wakati huo wote, Bashir na marafiki zake wa karibu waliendeleza ufisadi kimyakimya, wakatakatisha pesa chafu za silaha na biashara nyingine haramu.

Sasa muda wao umefika wa kulipia makosa yao. Lakini bado wana bahati kwa kuwa, kinyume na maelfu ya watu ambao waliuawa Darfur, wao wataponea kitanzi.

Mahakama ya ICC haina hukumu ya kifo, hivyo Bashir na wenzake wanaweza ama kufia jela au warejee Sudan wakiwa raia huru ikiwa watashinda kesi huko Hague.

Nilijua siku za Bashir zimehesabiwa pale Sudan ilipowajibikia mashambulio ya bomu dhidi ya balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania kwa kuahidi kuwafidia waathiriwa.

Ilikubali makosa kwa sababu kiongozi wa magaidi wa al-Qaeda, Osama bin Laden, aliishi Sudan akipanga mashambulio hayo.

Mambo yakiendelea yanavyoonekana, kufikishwa kwa Bashir ICC kutaizalia Sudan matunda matamu sana siku za usoni kwani wimbi la mabadiliko lililotanda nchini humo mnamo 2017 lingali kali.

Hili ni onyo kwa watawala ambao huongoza nchi zao kana kwamba ni visiwa binafsi ambavyo haviko chini ya sheria za kimataifa.

Siku ya siku ikifika, watakuwepo watu wengi watakaokuwa radhi kumkabidhi nduli yeyote kwa watakaomhitaji, ama kwa manufaa binafsi au ya nchi nzima.

 

[email protected]