Raila akemea ufisadi kanisani
CAROLINE WAFULA NA DICKENS WASONGA
KIONGOZI wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga, Ijumaa alikemea vikali viongozi wanaotumia pesa wanazopata kupitia ufisadi kutoa michango makanisani. Bw Odinga alisema ufisadi umekolea Kenya hivi kwamba viongozi wanaopora pesa za umma wanapeleka kuzificha makanisani.
“Tunataka kukabiliana na ukosefu wa ajira, ukosefu wa usalama, ufisadi na maovu mengine. Tunataka kujenga Kenya ambapo ikiwa ninatoa pesa kanisani, tunajua ninatoa nini na inatoka wapi,” Bw Odinga alisema.
Alisema kanisa halifai kugeuzwa mahali pa kuficha mali iliyopatikana kupitia ufisadi.
“Tabia hii inaendeleza ufisadi. Hii ndiyo sababu tunataka kupigana na uovu huu katika nchi hii,” alisema.
Akizungumza katika hafla ya kuadhimisha miaka 100 tangu shule ya wavulana ya Maranda ilipoanzishwa akiandamana na Jaji Mkuu David Maraga, Bw Odinga alihimiza mahakama kusaidia katika vita dhidi ya ufisadi kwa kuhakikisha kuwa kesi za washukiwa zinasikilizwa na kuamuliwa haraka.
“Wanasema dhamana ni haki ya kikatiba lakini haifai kutumiwa vibaya na hata wakipewa haifai kuwa mwisho wa kesi,” alisema Bw Odinga. Waziri huyo mkuu wa zamani alisema kwamba mchakato wa maridhiano (BBI) alioanzisha na Rais Uhuru Kenyatta, utaleta mwamko mpya Kenya.
“Tulikubaliana na ndugu yangu Uhuru kwamba tunataka kuunda Kenya mpya iliyoungana ambapo ukabila si kisiki cha kupata kazi na maendeleo,” alisema.
Miongoni mwa masuala tisa waliyoazimia kushughulikia kupitia mchakato wa maridhiano ni kupigana na ufisadi nchini.
Naibu Rais William Ruto amekuwa akihudhuria harambee makanisani na hata akaapa kuendelea nazo huku viongozi wanaompiga vita wakimtaka aeleze anakotoa pesa hizo.
Bw Maraga alisikitika kuwa licha ya Wakenya wengi kuwa Wakristo na walioelimika, ufisadi bado unaendelea kukita mizizi katika jamii.
“Kenya inahitaji wanaume na wanawake wenye maadili mema. Hali ilivyo kwa sasa ni kwamba waliosoma vyema wanashikilia nafasi za uongozi lakini kutokana na hali kwamba hawawezi kufanya chochote, ni ishara kwamba tunahitaji mabadiliko kama jamii,” alisema.
Alisema viongozi wa sasa hawawezi kutegemewa kuwa mfano mwema wa kuigwa na vizazi vijavyo.
“Tuna uhaba mkubwa wa viongozi wa kuigwa. Tunaogopa kuuliza chanzo cha utajiri wa watu na badala yake tunawafuata tu na kuutamani,” alisema.
Bw Maraga alisema kwamba chanzo cha changamoto zinazokabili nchi hii ni ukosefu wa maadili.
“Changamoto nyingi zinazotukabili kama nchi zinatokana na ukosefu wa maadili, bila maadili mema elimu pekee haitoshi, tunahitaji zaidi ya elimu nzuri, tunahitaji kujitolea na nidhamu ya hali ya juu,” alisema. Vita dhidi ya ufisadi vilishika kasi baada ya handisheki kati ya Bw Odinga na Rais Kenyatta. Hata hivyo, viongozi hao wawili wamekuwa wakilaumu mahakama kwa kulemaza vita hivyo kwa kuwaachilia washukiwa.
Jana, Bw Odinga alisema vita hivyo haviwezi kufaulu bila mahakama kutekeleza kazi yake na kuwafunga jela wahusika.
Hata hivyo, Bw Maraga amekuwa akitetea mahakama akisema kesi huamuliwa kutegemea ushahidi unaowasilishwa kortini.