Habari

Afungwa jela miaka miwili kwa kupatikana akimiliki nyoka

February 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na BRIAN OCHARO

MWANAMUME aliyepatikana na hatia ya kumiliki nyoka bila kibali, Ijumaa alifungwa jela miaka miwili.

Karisa Iha alifungwa na mahakama ya Mombasa alipokiri shtaka la kupatikana na nyoka huyo mwenye urefu wa mita 2.3.

Akitoa hukumu, Hakimu Mkaazi Vincent Adet alisema kuwa mshukiwa huyo anafaa kufahamu kuwa ni hatia kumiliki mnyama huyo bila kuwa na kibali kutoka kwa Shirika la Wanyamapori Nchini (KWS).

Aliongezea kuwa mshukiwa huyo alikosa kuelezea nia ya kumiliki mnyama huyo.

“Mshtakiwa lazima alipe kiwango cha Sh1 milioni au atumikie kifungo cha miaka miwili,” Bw Adet alisema.

Hakimu huyo pia alielekeza kuwa nyoka huyo apelekewe KWS.

Bw Iha alijitetea akisema kuwa hakuwa na nyoka huyo kwa nia mbaya bali alikuwa anaipeleka katika eneo la Ukunda ambapo Wanyama hao wanafugwa.

Bw Iha ambaye anadai kuwa amewahi kufanya na shirika la KWS alielezea kuwa alipokea simu kuwa nyoka huyo alionekana katika eneo la Mombasa.

Baada ya kupokea simu hiyo, mshtakiwa alielezea kuwa alienda moja kwa moja hadi eneo hilo na kuikamatwa kwa ajili ya kuipeleka katika eneo la hifadhi huko Ukunda.

Mshtakiwa huyo alisema kuwa ilikuwa ni bahati mbaya kupatikana na huyo nyoka na kuwa nia yake ilikuwa ni kumpekeleka katika hifadhi.

Mtuhumiwa anadaiwa kufanya kosa hilo mnamo Februari 11.