Madoya ahakikishia Zoo kuwa itasalia ligini
Na CECIL ODONGO
KIUNGO wa Klabu ya Zoo Kericho Michael Madoya amewahakikishia mashabiki wa timu hiyo kwamba hawatateremshwa ngazi mwisho wa msimu.
Madoyo ambaye alituzwa kama kiungo bora mbunifu mwaka 2017, alisikitikia matokeo mabaya ambayo yamekuwa yakisajiliwa na timu hiyo lakini akasema bado mwanya wa kujiimarisha upo.
Zoo Kericho Jumapili walionyesha kwamba si wanyonge katika ligi jinsi inavyodhaniwa baada ya kutoka nyuma na kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya miamba wa soka AFC Leopards.
Hadi sasa klabu hiyo kutoka Kaunti ya Kericho imeweza kushinda mechi mbili kati ya kumi iliyocheza na wanashikilia nafasi ya 17 kwenye msimamo wa jedwali la ligi inayoshirikisha timu 18.
“Kila timu huwa na wakati wake mgumu ambapo huwa wanalemewa lakini sisi kipindi hicho kinaelekea kuisha haswa baada ya sare dhidi ya AFC Leopards,” akasema kiungo huyo ambaye kando na talanta ya soka alisomea uanahabari.
Aidha alisisitiza kwamba hana presha zozote za kufikia kiwango chake cha mwaka 2017 na cha muhimu anacholenga ni kuisaidia timu kupata matokeo bora.
“Mimi sizingati kuibuka bora katika hiki ama kile lengo langu kuu ni kusaidia timu hii iepuke kuteremshwa ngazi,” akasema katika mahojiano baada ya mechi yao na Ingwe.
Zoo walipandishwa ngazi mwisho wa msimu jana baada ya kumaliza wa kwanza katika ligi ya daraja la pili na wanakibarua kigumu cha kuhakisha wanashinda mechi nyingi zilizosalia ili kutoka katika hatari ya kuteremshwa ngazi kufikia mwisho wa msimu.