• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
AIBU YA UBAGUZI: Moussa Marega wa FC Porto ajiondoa uwanjani

AIBU YA UBAGUZI: Moussa Marega wa FC Porto ajiondoa uwanjani

Na MASHIRIKA

GUIMARAES, URENO

MSHAMBULIAJI Moussa Marega wa FC Porto alijiondoa uwanjani dakika ya 69 ya mechi dhidi ya Vitoria Guimaraes katika Ligi Kuu ya Ureno baada ya kushindwa kuhimili matusi na vitendo vilivyoashiria ubaguzi wa rangi kutoka kwa mashabiki.

Marega ambaye ni mzaliwa wa Mali alianza kuondoka ugani dakika tisa baada ya kuwafungia waajiri wake bao la pili katika ushindi wa 2-1 waliousajili ugenini.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 28 alivielekeza vidole vyake vya gumba ardhini kisha kuwaonyesha mashabiki wa Guimaraes vidole vya kati vya mikono yake alipokuwa akitoka kuelekea chumba cha kubadilishia sare.

Licha ya wachezaji wenzake (Alex Telles, Sergio Oliveira na Ivan Marcano) na hata maafisa wa benchi ya kiufundi kambini mwa Porto kumzuia kuondoka, Marega alishindwa kabisa kujidhibiti na tukio hilo likamchochea kocha Sergio Conceicao kukifanyia kikosi chake mabadiliko.

Katika ujumbe alioupakia baadaye kwenye mtandao wake wa Instagram, Marega alisema, “mashabiki wa vikosi vya nyumbani wanaofika uwanjani kuwabagua wachezaji kwa misingi ya rangi ya ngozi zao ni wapumbavu”.

Akizungumza mwishoni mwa mechi, kocha Conceicao alikilaani kitendo hicho cha mashabiki wa Guimaraes na kusisitiza kwamba, “soka ni mchezo unaostahili kujenga undugu na kuwaleta pamoja watu mbalimbali bila ya kujali uraia, lugha, rangi ya ngozi au nywele.”

Katika taarifa iliyotolewa baadaye na Porto, vinara wa kikosi hicho walitaka usimamizi wa Guimaraes kuomba radhi na kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa kushindwa kudhibiti mienendo ya mashabiki wao.

Marega aliwahi kuhudumu kambini mwa Guimaraes kwa mkopo wa msimu mmoja mnamo 2016-17 ambapo alifunga mabao 15 kutokana na mechi 25.

Kwingineko, Real Madrid walipoteza fursa ya kupaa zaidi kileleni mwa jedwali la La Liga baada ya kulazimishiwa sare ya 2-2 kutoka kwa Celta Vigo ugani Santiago Bernabeu.

Mabao ya Real yalifungwa kupitia kwa Toni Kroos na Sergio Ramos huku ya Celta yakifumwa wavuni na Fedor Smolov na Santi Mina. Real ambao wamejivunia ubingwa wa La Liga mara moja pekee tangu 2012, sasa wanajivunia alama 53, moja zaidi kuliko Barcelona.

Katika mechi nyinginezo za ligi kuu za bara Ulaya, Juventus waliwapokeza Brescia kichapo cha 2-0 kwenye kivumbi cha Ligi Kuu ya Italia (Serie A) huku Bayern Munich ya Ujerumani wakiwapepeta FC Koln 4-1.

Juventus wanadhibiti kilele cha jedwali la Serie A kwa alama 57, moja zaidi kuliko Lazio waliowapiga Inter Milan 2-1. Bayern walifunga mabao matatu chini ya dakika 12 za ufunguzi katika ushindi uliowakweza kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kwa alama 46, moja mbele ya Leipzig.

You can share this post!

Kivumbi Atletico Madrid wakialika Liverpool leo Jumanne

AFYA: Cha kufanya ili kuzuia fangasi miguuni

adminleo