• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Ingwe waagizwa walipe Sh2m ili watumie Nyayo

Ingwe waagizwa walipe Sh2m ili watumie Nyayo

Na CECIL ODONGO

AFC Leopards wameamrishwa walipe Sh2 milioni kugharimia uharibifu uliosababishwa na mashabiki wao katika uwanja wa MISC Kasarani miezi mitatu iliyopita kabla waruhusiwe kuandaa mechi zao ugani Nyayo.

Uharibifu huo ulitekelezwa kwenye kipute cha debi ya Mashemeji dhidi ya Gor Mahia mnamo Novemba mwaka jana. Mashabiki hao walikasirika kisha wakazua vurumai kwa kuharibu viti na vifaa vingine vya uwanja huo kutokana na kichapo cha 4-1 mikononi mwa K’Ogalo.

Ingwe ilikuwa imetuma barua kwa bodi ya michezo kupitia wizara ya michezo ikiomba iruhusiwe kutumia uwanja huo lakini ombi hilo halijaridhiwa wakitakiwa kugharimia uharibifu walioutekeleza Kasarani mwanzo.

Mwenyekiti wa bodi ya michezo nchini Fred Muteti alithibitisha kwamba ameipokea barua ya Ingwe lakini akasema wataruhusiwa tu kutumia Nyayo inayoendelea kukarabatiwa baada ya kulipa gharama ya Sh2 milioni.

“Haja yetu kuu ni kutokomeza ghasia kwenye soka ndiyo maana tuliwaambia walipie uharibifu waliousababisha Kasarani kabla hatujazingatia ombi lao. Naendelea kutathmini hatua zilizopigwa kwenye ukarabati wa Nyayo lakini tutawapa sikio wakishalipia hasara waliyosababisha,” akasema Muteti kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’.

Katibu Mkuu wa Leopards Oliver Shikuku alisema marufuku ya kutotumia Nyayo kumewaathiri vibaya na hawana Sh2 milioni zinazohitajika kugharimia hasara jinsi bodi ya michezo ilivyowaamrisha.

“Ndiyo wametueleza kwamba tulipe Sh2 milioni lakini hatuna fedha hizo kwa sababu hatuna mfadhili. Tumewapendekezea waturuhusu tulipe Sh100,000 kwa kila mechi tunayosakata Nyayo hadi msimu huu umalizike lakini wamekataa,” akasema Shikuku.

Ingwe ambao walishinda Elim 1-0 mnamo Jumapili ili kufuzu raundi ya 16 ya Kombe la Betway FKF, watakita kambi Magharibi mwa Kenya kwa majuma mawili yajayo na Shikuku anasema hawana fedha za kutosha kugharimia mahitaji mbalimbali.

“Kwa kuwa tumenyimwa uwanja wa Nyayo, tutakita kambi Mumias kwa mechi zetu za Ligi dhidi ya Sofapaka na Chemelil Sugar. Mambo ni magumu zaidi kwetu kwa sababu hatuna fedha za kujikimu kwenye kambi hiyo,” akaongeza Shikuku.

Afisa huyo sasa ametoa wito kwa mashabiki na wahisani kusaidia timu hiyo kuchangisha Sh400,000 ambazo zinahitajika kuwakimu Mumias kwa siku 14 zijazo.

Mabingwa hao mara 13 wa Ligi Kuu (KPL) waligoma kutumia uwanja wa Kenyatta, Machakos wakisema wamekuwa wakipata fedha chache sana kutokana na ada za kiingilio.

  • Tags

You can share this post!

Spurs wana mtihani dhidi ya RB Leipzig Uefa

GWIJI WA WIKI: Nderitu Wanjohi

adminleo