• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
Kalonzo ageuza wimbo, asema hataki Waziri Mkuu mwenye mamlaka

Kalonzo ageuza wimbo, asema hataki Waziri Mkuu mwenye mamlaka

Na VALENTINE OBARA

KIONGOZI wa Chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, amegeuza msimamo wake kuhusu mamlaka ya Waziri Mkuu katika mapendekezo ya ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI).

Tangu mwaka uliopita wakati ripoti ya BBI ilipozinduliwa, Bw Musyoka alikuwa akisema jopo lilikosea lilipopendekeza kuwe na Waziri Mkuu asiye na mamlaka makubwa kumliko Rais.

Msimamo wake ulikuwa kwamba, kama kutakuwa na Waziri Mkuu basi awe mwenye mamlaka makubwa katika utawala wa nchi kuliko mamlaka yatakayoshikiliwa na Rais.

Lakini alipowasilisha maoni Jumatano katika kikao cha jopo la BBI linalokusanya maoni ya umma Nairobi kwa awamu ya pili, Bw Musyoka aligeuka akasema, Rais ndiye anafaa kuwa na mamlaka makubwa kumliko Waziri Mkuu.

Kulingana na Bw Musyoka, Chama cha Wiper kimependekeza endapo kutakuwa na mabadiliko ya katiba kuleta cheo cha Waziri Mkuu, atakayeshikilia wadhifa huo achaguliwe na Rais.

Kazi yake itakuwa ni kuratibu na kusimamia shughuli za kawaida za serikali, mbali na kuwa kiongozi wa shughuli za serikali bungeni.

“Waziri Mkuu atateua manaibu wawili ili waajiriwe na Rais. Atakuwa ndiye kiongozi wa chama au muungano wa vyama ulio na wanachama wengi zaidi bungeni,” akaeleza.

Hata hivyo, Rais hatakuwa na mamlaka ya kumfuta kazi Waziri Mkuu. Bw Musyoka amependekeza jukumu hilo lifanywe na theluthi mbili ya wabunge katika Bunge la Taifa na Seneti.

Wiper pia imependekeza mamlaka ya kuchagua mawaziri yawe mikoni mwa Rais, ambaye atakuwa huru kuchagua mawaziri walio wabunge au kutoka nje ya bunge.

Ijapokuwa Kiongozi wa ODM Raila Odinga hajajitokeza wazi wazi kueleza msimamo wake kuhusu mamlaka ambayo Waziri Mkuu anafaa kupewa, baadhi ya viongozi katika chama hicho hutaka wadhifa huo ukabidhiwe mamlaka makubwa kuliko ya Rais.

Vile vile, chama hicho kinataka mgombeaji urais na mgombea mwenza wake wanaoibuka wa pili uchaguzini wapewe wadhifa wa viongozi rasmi wa upinzani katika seneti na bunge la taifa mtawalia.

Bw Musyoka amependekezea jopo la BBI kuongeza idadi ya kaunti kutoka 47 hadi 50, ambapo kaunti tatu mpya zitakuwa ni Gucha, Maua na Mwingi.

Vile vile, ametaka idadi ya wadi zipunguzwe kutoka 1,500 hadi 700 lakini madiwani waongezwe mishahara na pia wao ndio wawe wakiteuliwa kuwa mawaziri wa kaunti.

You can share this post!

Kaunti ya Nyeri yatenga kipande cha ardhi kufanyia miradi...

Matiang’i azimwa kufukuza Wachina waliochapa raia wa...

adminleo