Serikali kupunguza matumizi yake katika mwaka wa kifedha wa 2020/2021
Na CHARLES WASONGA
SERIKALI inapanga kupunguza matumizi yake katika mwaka wa kifedha ujao unaoanza Julai 2020 kwa kiwango cha asilimia 23.6 ya jumla ya utajiri wa kitaifa (GDP) kutoka asilimia 26 mwaka huu wa kifedha, Wizara ya Fedha imetangaza katika hati ya kisera ya bajeti (Budget Policy Statement-BPS).
Hatua hiyo ya kupunguza matumizi inalenga kuisaidia serikali kupunguza pengo katika bajeti kwa kupindi hicho hadi asilimia 4.9 ya GDP. Katika mwaka huu wa kifedha pengo katika bajeti ni asilimia 6.3 ya GDP.
“Mapato yakilinganishwa na GDP yanakisiwa kusalia katika kiwango cha asilimia 18.4 katika mwaka ujao wa kifedha,” wizara ya fedha inasema.
Serikali inapanga kukopesha Sh222.9 bilioni kutoka mashirika ya kifedha ya humu nchini kuziba pengo katika bajeti.
Vilevile, inapanga kukopa Sh345.1 bilioni kutoka mashirika ya kifedha kutoka nje, taarifa hiyo inayojadiliwa na kamati mbalimbali za bunge ikasema.
Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imelaumiwa na raia kwa kukopa pesa nyingi zaidi tangu ilipoingia mamlakani mnamo 2013.
Na mwishoni mwa mwaka 2019 ilipandisha kiwango cha fedha ambazo inaweza kukopa kutoka Sh6 trilioni hadi Sh9 trilioni.
Kenya imekuwa ikikopa fedha nyingi kwa ajili ya kufadhili miradi ya ujenzi wa miundomsingi, ukiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kutoka Mombasa hadi Nairobi.
Mradi huo uligharimu Sh337 bilioni ambayo ilianza kulipwa mnamo Juni 2019.
Pengo katika bajeti ya kitaifa pia imesababishwa na hali kwamba Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA) hufeli kutimiza kiwango cha ukusanyaji mapato kilichokusudiwa.