BONGO LA BIASHARA: Achuma hela kibao kutokana na ustadi wake katika unyoaji jijini
Na CHARLES ONGADI
MARA tu baada ya kifo cha ghafla cha mama mzazi mwaka wa 2005 George Franck Bruno, 26, alilazimika kukatiza masomo yake katika kidato cha pili.
Ijapo hakupata elimu ya sekondari kijana Bruno anajichumia hela kibao kwa kunyoa, kurembesha nywele na ukandaji watu (massage) katika duka lake lililoko mita chache tu kutoka hoteli ya zamani ya Splendid katikati ya jiji la Mombasa.
Maisha yalianza kumwendea kombo na kumlazimisha kuanza kujisakia maisha kwa kufanya kazi za vibarua mitaani.
“Nilianza kufanya kazi za mjengo na kuchuuza vyombo vya nyumbani kutoka mtaa mmoja hadi mwingine hapa Mombasa ili kujikimu kimaisha,” asema Bruno.
Hata hivyo, tangu utotoni mwake Bruno alitamani sana kuwa kinyozi kazi ambayo wazazi wake hawakutaka afanye kutokana na kipato duni kitokacho kwa kazi hii.
Hata hivyo, mwaka wa 2015, Bruno alimtembelea kakaye aliyekuwa na banda la kinyozi mjini Ukunda kaunti ya Kwale.
Katika kipindi cha majuma mawili aliyokuwa huko, alijifunza mitindo mbali mbali ya kunyoa nywele inayopendeza na kuvutia wateja.
“Kakangu hakuweza kunipa nafasi ya kuwanyoa wateja wake kwa hofu kwamba nisingeweza kunyoa vyema kutokana na hali kwamba sikuwa na ujuzi kwa kazi hiyo,” asema Bruno.
Lakini siku moja kakaye alikuwa na safari ya ghafla na kumwacha kibandani na mara akatokeza mmoja kati ya wateja aliyeandamana na mtoto wake.
Alimfahamisha mteja huyo kwamba kaka yake alikuwa kaondoka lakini angerudi muda mfupi baadaye lakini baada ya kusubiri kwa muda, mteja huyo alimsihi kumnyoa tu.
Bruno anaiambia Akilimali kwamba ni hapo ndipo ndoto yake ilitimia baada ya kumhudumia mteja huyo kwa ufundi mkubwa.
“Mteja huyo alifurahia sana hasa jinsi nilivyomnyoa mwanawe na kuahidi kurudi siku nyingine na hapo ndipo maisha yangu yakaanza kubadilika,” aongeza Bruno huku akimhudumia mmoja kati ya wateja wake wakubwa.
Baada ya sifa hizo, kakaye alimruhusu kuwa msaidizi wake ambapo mtu mmoja walikuwa wakimnyoa kwa kiasi cha Sh50.
Kakaye alimpenda zaidi kutokana na kasi yake katika unyoaji ambapo alikuwa na uwezo wa kunyoa zaidi ya wateja 15 huku akichukua chini ya dakika moja kumhudumia mteja mmoja.
Mbali na kinyozi, Bruno pia alijifunza namna ya kurembesha nywele (hairdressing) kutengeza dreadlocks na kutengeneza mapambo mbali mbali ya nywele.
Ni hapo ndipo wazo la kufungua biashara yake kitovuni mwa mji wa Mombasa lilimjia hasa baada ya wateja wengi eneo la Ukunda kumwomba kufanya hivyo.
Mara baada ya kupata mtaji, Bruno aliamua kushirikiana na mwenzake kuanzisha duka maarufu la Urbano Lounge, Barber and Spa ambayo mbali na kinyozi pia linarembesha nywele na kufanya ukandaji mwili. Ni kituo kinachopendwa na watu wa tabaka zote kutokana na huduma zao nzuri.
Kwa mujibu wa Bruno, wananyoa mitindo mbali mbali ya nywele kwa Sh400 huku akiweka mapambo ya nywele (dye) kwa Sh6,000 kwa kila mteja nazo dreadlocks akizitengeneza kwa Sh2,500.
Hata hivyo, anaiambia Akilimali kwamba bei mara nyingine hutofautiana kulingana na huduma aliyohitaji mteja.
Kwa mwezi, Bruno hutia kibindoni kitita cha Sh80,000 kiasi anachosema kinaweza kuongezeka kulingana na msimu.
Anafichua kwamba msimu wa Krismasi, mwaka mpya na sherehe za Iddi, kazi yake hunoga sana na kwenda nyumbani na kiasi kikubwa cha hela.
Aidha, Bruno anakiri kuwa katika kila kazi ni lazima kuwe na changamoto japo amekabiliana nazo barabara.
Mojawapo ya changamoto ni pale mteja anapokosa kuridhika na huduma ama kutoa ahadi ya kulipa baadaye ila kuishia kuingia gizani. Pia jinsi ya kusaka wateja wapya jambo ambalo analifanya kupitia mtandao.
Tatizo jingine ni pale mteja anapotoa miadi ya kuja kuhudumiwa kisha apate wateja wakihudumiwa tayari jambo ambalo huwalazimu kusubiri kwa muda.
Bruno asema kwamba ijapo babake hakuweza kumsaidia kumaliza masomo yake ya upili, hana kinyongo naye kwani amekuwa akimsaidia kwa hali na mali akiwa mashambani.
“Kila mwezi mimi huhakikisha nimepeleka posho kwa vituo vya mayatima, nyumba za wazee na hata kutoa huduma za bwerere kwa kuwanyoa vijana wasio na makao hapa katikati ya jiji la Mombasa,” asimulia Bruno.
Anasema kila mtu ana uwezo wa kufanya jambo kulingana na kipaji alichopewa na Maulana ila cha muhimu ni kuomba kila mara na kuamini kwamba Mungu anaweza.
Bruno asema analenga kuwahudumia wateja wengi zaidi na kwa sasa anajizatiti kufungua duka kubwa la kinyozi , ukandaji miili na marembesho mengine katika mji wa Malindi.